Wajibu wa Kutii Sheria za Nchi

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa www.ulizasheria.co.tz . Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya Katazo la Kazi za Shuruti. Leo tunaendelea na mfululizo makala juu ya wajibu wa kila mwanajamii kama uilivyoanishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Karibu tujifunze.

Maana ya Wajibu wa Kutii Sheria za Nchi

Wajibu ni jambo ambalo mtu anawajibika au analazimika kulifanya. Katiba ya JMT inaeleza wazi kuwa kila mwananchi anawajibu wa kutii sheria na Katiba ya nchi Ibara ya 26 (1) ya Katiba ya JMT inasema

Kila mtu ana wajibu wa kufuata na kutii Katiba hii na sheria za Jamhuri ya Muungano’

Ufafanuzi

Kama tulivyoeleza juu ya sheria katika nchi ni lazima wananchi wazitii wakati wote. Sheria haina mbadala zaidi ya kuitii. Sheria ina tabia ya kushurutisha hivyo ni lazima kuitii hakuna hiyari. Watu wote wasioitii sheria wanaingia kwenye makosa ambayo wakipelekwa katika vyombo vya kisheria wakitiwa hatiani wanapata adhabu.

Ibara ya 26(2) inaendelea kufafanua zaidi juu ya utii wa sheria

‘Kila mtu ana haki, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria, kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha hifadhi ya Katiba na sheria za nchi’

Hapa Katiba inatoa wajibu wa kila mwananchi ambaye kwa njia moja ama nyingine anaona upo ukiukwaji wa Katiba au Sheria, anaweza au anayo fursa ya kufuata taratibu za kisheria kuhakikisha Katiba inatunzwa na sheria za nchi zinafuatwa kikamilifu.

Kutii sheria ni jukumu la msingi la mwananchi ambalo anapaswa kulitekeleza. Ikiwa kuna sheria ambayo inaonekana si nzuri katika mazingira ya sasa, upo utaratibu ambao unafanyika kupitia vyombo husika ambapo wadau wanaweza kujadili na hatimaye mswada kupelekwa Bungeni kwa marekebisho au kuifuta sheria husika.

Hitimisho

Ni muhimu kwako mwananchi kuifahamu vyema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na sheria zake zinazotungwa na Bunge au sheria ndogo mbali mbali. Kwa vyovyote vile mtu hawezi kutii sheria ambazo hazijui, hivyo jitihada binafsi kama mwananchi zinahitajika katika kuhakikisha unazifahamu sheria mbali mbali na misingi ya uendeshaji wa shughuli zako binafsi na shughuli za umma kwa mujibu wa sheria.

 ‘timiza wajibu wako wa kutii sheria upate haki yako’.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili