Hali ya Hatari

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya Hifadhi ya Haki na Wajibu. Leo tunajadili juu ya Hali ya Hatari kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Karibu tujifunze.

Maana ya Hali ya Hatari

Katiba ya JMT inaeleza juu ya madaraka ya kutangaza Hali ya Hatari na kama inavyoonekana katika Ibara ya 32 (1) ya Katiba ya JMT inaeleza

Bila kuathiri Katiba hii, au sheria iliyotungwa na Bunge kwa ajili hiyo, Rais aweza kutangaza hali ya hatari katika Jamhuri ya Muungano au katika sehemu yake yoyote’

Ufafanuzi

Hali ya hatari inazungumzia juu ya taifa au sehemu ya Tanzania kuwa katika tishio ambalo linaweza kuleta madhara makubwa kwa nchi. Hivyo tangazo la hali ya hatari ni kusudio la mamlaka za nchi kuchukua hatua madhubuti kuikabili hatari hiyo.

Mazingira ambayo Rais anaweza kutangaza hali ya hatari

Katiba ya JMT inaeleza mazingira ambayo Rais anaweza kutangaza hali ya hatari kwa mujibu wa Ibara ya 32(2) kama ifuatavyo;

‘Rais aweza tu kutangaza kuwa kuna hali ya hatari iwapo;

  • Jamhuri ya Muungano iko katika vita;
  • Kuna hatari hasa kwamba Jamhuri ya Muungano inakaribia kuvamiwa au kuingia katika hali ya vita; au
  • Kuna hali halisi ya kuvurugika kwa amani ya jamii au kutoweka kwa usalama wa jamii katika Jamhuri ya Muungano au sehemu yake yoyote kiasi kwamba ni lazima kuchukua hatua za pekee ili kurejesha amani na usalama; au
  • Kuna hatari dhahiri na kubwa, kiasi kwamba amani ya jamii itavurugika na usalama wa raia kutoweka katika Jamhuri ya Muuungano au sehemu yake yoyote ambayo haiwezi kuepukika isipokuwa kwa kutumia mamlaka ya pekee; au
  • Karibu kutatokea tukio la hatari au tukio la balaa au la baa ya kimazingira ambalo linatishia jamii au sehemu ya jamii katika Jamhuri ya Muungano; au
  • Kuna aina nyingineyo ya hatari ambayo kwa dhahiri ni tishio kwa nchi.

Rais atakapotangaza juu ya hali ya hatari kwa taifa au sehemu ya Jamhuri ya Muungano anapaswa kutuma nakala ya tangazo kwa Spika wa Bunge ambaye atapaswa kuitisha kikao maalum ndani ya siku 14 kujadili na kupitisha azimio la kuunga mkono tangazo au kutokuunga mkono. Hii ni kwa mujibu wa Ibara ya 32 (3) ya Katiba.

Tangazo la hali ya hatari litakoma kutumika

  • Iwapo litafutwa na Rais
  • Endapo zitapita siku 14 tangu tangazo lilipotolewa kabla ya kupitishwa azimio la Bunge kuunga mkono
  • Baada ya kupita miezi 6 tangu tangazo hilo lilipotolewa. Hata hivyo Bunge linaweza kabla ya kumalizika kipindi cha miezi 6 kuongeza kwa vipindi vya miezi 6 kwa kuungwa mkono kwa wajumbe wasiopungua theluthi mbili
  • Wakati wowote ambapo mkutano wa Bunge utalitangua tangazo hilo kwa azimio

Hii ni kwa mujibu wa Ibara ya 32 (5) ya Katiba ya JMT.

Hitimisho

Tangazo ya hali ya hatari ni madaraka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo kama amiri jeshi mkuu wa vikosi vya ulinzi na usalama, dhamana ya hali ya amani na utulivu ipo katika mikono yake. Hata hivyo kama tulivyoona Bunge kama chombo cha uwakilishi wa wananchi lina wajibu wa kujadili na kutafakari maamuzi ya Rais juu ya tangazo lolote la hali ya hatari na kuchukua hatua stahiki.

Muhimu kwetu wananchi kuhakikisha tunailinda nchi yetu dhidi ya vitendo vyovyote ambavyo vinaweza kulisababishia taifa kuingia katika mgogoro wowote na kuleta hali ya hatari. Wananchi na viongozi waishi kwa kutenda haki siku zote ndipo amani na utulivu utakavyostawi katika taifa letu.

 ‘Tafuta haki, tenda haki kwa kila mmoja wetu tuepushe migogoro ndani ya taifa’

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili

1 reply

Comments are closed.