Mipaka ya Utendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya Uhuru wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora. Leo tunaendelea na mfululizo makala juu ya Tume hii kama uilivyoanishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Karibu tujifunze.

Mipaka ya Utendaji wa Tume

Katiba ya JMT kama kwenye vyombo vingine vilivyoundwa na Katiba Tume nayo imewekewa mipaka ya utendaji wake, hii inaainishwa na katika Ibara ya 130(3) inayosema;

‘Masharti ya ibara ndogo ya (2) yasihesabiwe kuwa yanamzuia Rais kutoa maagizo au amri ya Tume, wala hayatoi haki kwa Tume kutofuata maagizo au amri, endapo Rais ataona kuwa, kuhusiana na jambo lolote au hali yoyote, masilahi ya taifa yahitajia hivyo’

Ufafanuzi

Kipengele hiki cha Katiba kinaeleza juu ya mipaka ya Tume kwamba pamoja na uhuru uliopewa katika kufanya shughuli zake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayo haki ya kutoa maagizo na amri kwa Tume endapo yatahusisha maslahi ya taifa.

Aidha Ibara ya 130(5) ya Katiba inazidi kufafanua juu ya mipaka ya Tume kuhusisha na madaraka ya Rais kuagiza

‘Tume itafanya uchunguzi kwa kufuata masharti ya ibara hii na masharti ya sheria iliyotungwa na Bunge kwa ajili hiyo, na itafanya uchunguzi juu ya mtu yeyote anayehusika au taasisi yoyote inayohusika kila itakapoagizwa na Rais kufanya uchunguzi, vilevile, isipokuwa kama Rais ameagiza Tume isifanye uchunguzi wakati wowote  inapoona inafaa kuchunguza mwenendo wa mtu yeyote anayehusika, na masharti ya ibara hii anayetuhumiwa au inayotuhumiwa kwa kukiuka madaraka ya kazi yake, kutumia vibaya madaraka ya kazi yake au majukumu ya taasisi hiyo au kwa uvunjaji wa haki za binadamu au misingi ya utawala bora’

Mipaka ya Tume

Mipaka ya madaraka ya Tume imeanishwa katika Ibara ya 131(2) ya Katiba ya JMT kama inavyoelekeza;

‘Tume haitachunguza mambo yafuatayo, kwa madhumuni ya kutekeleza majukumu yake, yaani-

  • Jambo lolote ambalo liko mbele ya Mahakama au chombo kinginecho cha kimahakama;
  • Jambo lolote linalohusu uhusiano au mashirikiano kati ya Serikali na Serikali ya nchi yoyote ya nje au shirika la kimataifa;
  • Jambo linalohusu madaraka ya Rais kutoa msamaha
  • Jambo lingine lolote lililotajwa na sheria yoyote.

 

Hitimisho

Mipaka ya Tume inaonekana wazi katika kazi za Tume ambazo kisheria zinapaswa kufanywa na zile ambazo Tume haiwezi kufanya. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ni chombo huru na chenye mamlaka kamili ya kuchunguza masuala yote ya haki za kibinadamu na utawala bora. Hatahivyo kama tulivyosisitiza kwenye makala nyingine zilizotangulia kuwa hakuna uhuru usio na mipaka, hivyo chombo hiki pia kina mipaka katika kutekeleza madara

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili