Utaratibu wa Umiliki wa Ardhi kwa njia ya Familia au Ukoo

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika makala iliyopita tuliangalia juu ya njia mbalimbali za umiliki wa ardhi katika nchi yetu ya Tanzania. Leo tunaendelea na mfululizo wa uchambuzi wa njia moja moja ambazo tulizianisha hapo awali. Karibu tujifunze.

Umiliki wa Ardhi kwa njia ya Familia au Ukoo

Katika jamii za kitanzania zimejengwa katika hali ya ushirikiano kwa njia za kifamilia na ukoo. Jamii nyingi zimeanzishwa vijijini na wengi wanamiliki maeneo katika ardhi ya vijiji.

Msingi wa umiliki ardhi kwa ngazi ya familia au ukoo unatokana na mfumo wa kimaisha ya kimila uliojengwa katika koo au makabila mbalimbali katika Tanzania.

Umiliki huu wa ardhi kwa njia ya familia au ukoo unafahamika kama umiliki wa Kimila.

Sheria ya Ardhi na ile sheria ya Ardhi ya Vijiji inatambua uhalali wa umiliki wa ardhi kwa njia ya kimila.

Utaratibu wa umiliki ardhi kwa njia ya Familia au Ukoo

Pamoja na kufahamika kuwa utaratibu huu wa umiliki wa ardhi kwa familia au ukoo unaainisha umiliki wa ardhi kimila, taratibu au namna watu wanavyopata umiliki huu wanatofautiana kutokana na asili ya mila za maeneo au koo wanazotoka. Kila ukoo au familia au jamii ina mfumo wake wa kumilikisha eneo au ardhi kwa mwanafamilia au mwanaukoo.

Hatahivyo, katika makala hii tutaenda kuangalia mambo kadhaa ya msingi ambayo yanatekelezwa na koo mbalimbali au familia katika kumilikisha ardhi kimila.

  1. Uwepo wa ardhi ya familia au ukoo

Katika utaratibu mzima wa umiliki wa ardhi ya familia au ukoo ni lazima iwepo ardhi inayotambulika kwa familia au ukoo kuwa ni ya familia. Ardhi hii inaweza kuwa imetafutwa na baba wa familia au kiongozi wa ukoo na imekuwa ikirithishwa vizazi baada ya vizazi.

  1. Usimamizi wa ardhi ya familia au ukoo

Usimamizi wa ardhi ya familia au ukoo kwa kawaida inakuwa chini ya usimamizi wa mkuu wa familia au mkuu wa ukoo. Mkuu huyu ndiye aliye na dhamana ya ulinzi wa ardhi na mipaka yake na kwa kupitia vikao vya kifamilia au kiukoo ndiye anayeweza kushirikiana na wanafamilia au wanaukoo katika kugawa au kutatua changamoto zozote zinazojitokeza kuhusiana na ardhi husika.

  1. Vigezo vya kumilikishwa ardhi ya familia au ukoo

Vipo vigezo muhimu ambavyo mwanafamilia au mwanaukoo anapaswa kuwa navyo ili kuweza kupata nafasi ya kutumia au kumiliki sehemu ya ardhi ya familia au ukoo.

  • Lazima idhibitike kuwa mtu anayetaka kutumia ardhi ya familia au ukoo ni mwanafamilia husika au mwanaukoo
  • Lazima mwanaukoo au mwanafamilia asiwe katika adhabu fulani kwa mfano kutengwa na familia au ukoo kutokana na makosa.
  1. Masharti yanayoambatana na umiliki na matumizi ya ardhi ya familia au ukoo

Yapo masharti yanayoambatana na umiliki wa ardhi na matumizi yake kwa mwanafamilia na wanaukoo. Mfano wa masharti hayo;

  • Lazima mmiliki awe mwanafamilia au mwanaukoo
  • Ardhi husika hairuhusiwi kukodishwa au kuuzwa kwa mtu asiye mwanafamilia au mwanaukoo.
  • Kwa mila nyingi za kiafrika wanafamilia wa jinsia ya kiume wanapewa kipaombele cha umiliki wa ardhi hiyo kuliko wanawake.
  • Ikiwa mmiliki ni mwanamke anaweza asiwe na haki ya kurithisha ardhi hiyo kwa watoto wake kwani kufanya hivyo ardhi itahamishiwa kwa familia au ukoo mwengine.

Hitimisho

Umiliki wa ardhi kwa familia au ukoo ni umiliki wa kimila ambapo sheria na taratibu za kimila zinatumika kulingana na asili ya makabila mbalimbali. Hatahivyo ni vyema kuzingatia kuwa mila na taratibu za kifamilia au ukoo zinazopingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 hazipaswi kuendelezwa hasa zile za ubaguzi wa umiliki wa wanawake. Raia wote wanayo haki ya kumiliki ardhi iwe kwa njia za kimila au kwa taratibu za kiserikali.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili