Mgawanyo wa Mirathi ya Kikristo

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu  kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunaendelea kujifunza na mfululizo wa makala zinazohusu masuala ya mirathi. Karibu tujifunze kwa pamoja.

Mirathi ya Kikristo

Mgawanyo wa mali kwa kufuata dini ya Kikristo ni mwongozo kwa wale wenye kuishi maisha kwa kufuata dini na mwongozo wa Kikristo. Mgawanyo huu unatokana na sheria ya Urithi ya India ya mwaka 1865 ambayo inatumika Tanzania hata sasa. Sheria hii iliingia Tanzania kupitia wakoloni wa Kiingereza

Mfumo wa ugawanyaji wa mirathi kufuata dini ya Kikristo unatokana na familia hasa yaani mume/mke na watoto wa marehemu kabla ya kuwafikia warithi wengine.

Msingi wa  Mgawanyo wa Mirathi ya Kikristo

  • Kwamba urithi ni kwa wote yaani wanaume wanaweza kurithi mali ya wanawake na hali kadhalika wanawake kurithi mali ya wanaume.
  • Urithi unatoa kipaombele kwanza kwa familia ya marehemu ikiwa marehemu ameacha mke na watoto basi urithi utakwenda kwa hao.
  • Mirathi ya kufuata dini ya Kikristo inaweza kuwagiwa yote kwa wosia au sehemu kwa wosia na sehemu nyingine pasipo wosia.

Utaratibu wa mgawanyo wa mirathi

Kwa kawaida endepa marehemu ameacha mali ambayo inapaswa kugawanywa katika mirathi basi mali hiyo inaweza kuhusika katika kulipia

  • Gharama za mazishi
  • Madeni
  • Kugawa kwa warithi kwa wosia
  • Kugawa mali kwa warithi pasipo wosia

Mahakama au msimamizi wa mirathi kabla ya kuchukua hatua za kugawa mirathi ni lazima kujiridhisha juu ya imani au mwenendo wa marehemu ikiwa alikuwa mwamini wa dini ya Kikristo au la. Hii itaepusha mgongano baina ya wanafamilia ambao ni warithi na wale ambao si warithi.

Mfano wa mgao wa mirathi ya Kikristo pasipo wosia

  • Endapo mume atafariki pasipo kuacha mtoto basi mke atapata ½ ya mali yote na wazazi wa mume watapata ½ ya mali yote.
  • Pale mume akifariki akiwa na watoto basi mke atapata ½ ya mali yote na watoto watapata ½ ya mali yote.
  • Endapo mke atafariki pasipo kuacha mtoto basi mume atapata ½ ya mali yote na wazazi na ndugu wa mke watapata ½ ya mali yote.
  • Endapo mke atafariki akiwa na watoto basi mume atapata ½ ya mali yote na watoto watapata ½ ya mali yote.

Hata hivyo matumizi ya sheria ya Urithi ya India yanamruhusu mtu kuusia mali yake yote, tofauti na mfumo wa mirathi kwa dini ya Kiislam.

Hitimisho

Leo kwa mara nyingine tumejifunza juu ya mirathi kufuata dini ya Kikristo na namna sheria ya Urithi ya India inavyoongoza mirathi husika. Msingi wa mgao wa mirathi hii ni kulenga hasa wategemezi wanaobaki baada ya mtu kufariki yaani mwenzi na watoto iwapo watakuwepo. Ikiwa mtu amefariki pasipo mwenzi au watoto basi mali yake itaenda kwa wazazi wake na ndugu zake wa karibu kama kaka na dada zake.

‘Andika wosia sasa, maadam unaishi leo’

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili