Hatua za Kuchukua endapo Msimamizi wa Mirathi hatimizi wajibu wake.

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunaendelea kujifunza na mfululizo wa makala zinazohusu masuala ya mirathi. Karibu tujifunze kwa pamoja.

Msimamizi wa Mirathi

Msimamizi wa mirathi ni mtu anayeteuliwa na familia au ukoo kwa ajili ya kutelekeleza majukumu ya kuhakikisha mali ya marehemu inakusanywa na madeni yake yanalipwa kisha kugawanywa kwa warithi halali wa marehemu. Msimamizi wa mirathi anateuliwa na familia kisha anadhibitishwa na Mahakama ambapo shauri la mirathi linakuwa limefunguliwa.

Katika makala iliyopita tumeweza kuangalia kwa kirefu baadhi ya kazi za msimamizi wa mirathi. Kazi hizo anapaswa kuzitekeleza kwa uaminifu na uadhilifu ndani ya muda mwafaka.

Hatahivyo tumeshuhudia katika kutekeleza usimamizi wa mirathi aidha kwa kutokujua wajibu wao au kwa makusudi tumeona wasimamizi wa mirathi wakitenda vitendo kinyume na utaratibu na hivyo kusababisha hasara na upotevu wa haki kwa warithi halali wa marehemu.

Changamoto tunayoiona ya wasimamizi wengi wa mirathi wale amabo pia ni warithi na hata wale ambao si warithi wanashindwa kusimamia kwa haki na kujikuta wakifanya vitendo kama vile;

  • Kugawa mali kwa upendeleo. Hapa kama msimamizi ni miongoni mwa warithi anatafuta kupata mali zaidi ya warithi wenzake au endapo yeye si mrithi anagawa mali kwa mrithi ambaye ana maslahi naye.
  • Kuchukua muda mrefu kukamilisha zoezi la ugawaji wa mali. Wasimamizi wengine wanachelewesha zoezi la kugawa mali na kuzidi miezi 6 kama sheria inavyoelekeza. Unakuta shauri limefunguliwa lina miaka zaidi ya 10 zoezi la ugawaji halijakamilika.
  • Wasimamizi kutumia mali za marehemu kwa manufaa yao. Wapo ambao wakiteuliwa ingawa si warithi wanageuza mali husika kuwa yao na familia zao badala ya kufanya mgao kwa warithi halali.
  • Wasimamizi kuuza au kuweka rehani mali pasipo kushirikisha warithi. Tumeshuhudia migogoro mingi ikiibuka baada ya msimamizi kuchukua hatua ambazo warithi hawana taarifa nazo na kuleta hasara kwa warithi halali.

Haya ni baadhi ya matatizo yanayosababishwa na wasimamizi wa mirathi katika mchakato mzima wa usimamizi wa mirathi.

Hatua za Kuchua dhidi ya Msimamizi wa Mirathi

Vitendo vya msimamizi wa mirathi ambavyo ni kinyume cha sheria vinaweza kuadhibiwa endapo warithi watachukua hatua dhidi ya msimamizi wa mirathi.

  1. Shauri la jinai

Endapo msimamizi wa mirathi atashindwa kuonesha taarifa sahihi na kuziwasilisha mahamamani basi anaweza kuchukuliwa hatua za kijinai. Msimamizi wa mirathi akipatikana na hatia anaweza kufungwa kifungo kisichozidi miaka 7.

  1. Shauri la madai

Endapo itabainika msimamizi wa mirathi hakutimiza wajibu wake wa kugawa mali ipasavyo na baadhi au warithi wakakosa sehemu yao kutokana na matendo ya msimamizi wa mirathi. Warithi wanaweza kufungua shauri la madai dhidi yake na akipatikana na hatia basi atawajibika kulipa kiasi cha mali kilichopotea kwa warithi halali.

  1. Msimamizi kuondolewa katika usimamizi wa mirathi

Warithi wanayo haki ya kuomba mahakama imuondolee msimamizi haki ya kusimamia mirathi ya marehemu endapo wataona hatekelezi wajibu wake ipasavyo. Warithi wanapaswa kurudi katika mahakama iliyomteua msimamizi na kuwasilisha lalamiko lao ambapo litasikilizwa na kuamuliwa. Ikiwa msimamizi ataondolewa katika wajibu wake, basi atateuliwa msimamizi mwengine kuchukua majukumu yake.

Hitimisho

Ni rai yangu kwa watu wote wanaopata nafasi ya kusimamia mirathi kuwa waangalifu na kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria na taratibu. Ni vyema kama msimamizi na hujafahamu majukumu yako, tafuta ushauri kwa wanasheria ambao wataweza kukusaidia kwa ushauri namna bora ya kutimiza wajibu. Warithi pia ambao kwa njia moja au nyingine wamedhulumiwa urithi wao kutokana na matendo ya wasimamizi wa mirathi wanayo haki ya kwenda mahakamani na kuomba kutenguliwa uteuzi wa msimamizi au kudai fidia kutokana na matendo ya msimamizi wa mirathi.

‘Andika wosia sasa, maadam unaishi leo’

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Karibu kwenye darasa la sheria 2018 kufuata link hiiDARASA LA ULIZA SHERIA 2018 

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili