Biashara Sheria.1. Karibu Ukurasa Mpya wa Biashara Sheria

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa mtandao wa uliza sheria katika ukurasa huu mpya ambao unahusu masuala mbalimbali ya biashara sheria. Ukurasa huu ni mwitikio wa maswali ya wengi miongoni mwa wasomaji wetu wa mtandao wa uliza sheria. Katika kipindi cha miezi mitano ya kuwepo mtadao wa uliza sheria pamoja na mambo mengine mengi, maswali kadhaa yamekuwa yakiulizwa yanahusiana na maswala ya biashara na sheria. Tumepokea maswali au maombi ya ushauri katika maeneo ya mikataba, maswala ya kuanzisha biashara kisheria na kuendesha biashara au shughuli mbali mbali kwa mujibu wa sheria, n.k.

Kwa kuona umuhimu huu wa wasomaji wetu kupenda kufahamu mambo ya msingi  ya kisheria katika shughuli zao za uzalishaji mali na fedha basi tumeamua kuanzisha ukurasa maalum ambao utahushisha uchambuzi wa sheria na dhana mbali mbali za kisheria zinazohusiana na biashara au shuguli mbali mbali za uzalishaji.

Malengo ya ukurasa wa Biashara Sheria

  • Kutoa elimu ya kutosha kwa wasomaji wetu kuhusu uhusiano uliopo kati ya sheria na biashara au shughuli wanazofanya
  • Kutoa ushauri wa namna bora ya kutumia sheria kama nyenzo ya kustawisha biashara au shughuli za wasomaji wetu
  • Kutoa ushauri na mwongozo bora katika kuhakikisha biashara na shughuli zetu zipo kwa mujibu wa sheria.

Changamoto

Katika mfumo wa uzalishaji mali na uendeshaji wa shughuli mbalimbali katika nchi yetu ya Tanzania, ni shughuli au baishara chache sana ambazo zinaendeshwa katika mfumo rasmi yaani zimeundwa na kuendesha shughuli zake kwa mujibu wa sheria. Zipo sekta kadhaa za uzalishaji kama kilimo, viwanda, migodi, n.k. kwa ujumla zipo sekta za umma na zile binafsi. Uzalishaji mkubwa zaidi upo katika sekta binafsi ambazo ni shughuli za wananchi kwa ujumla.

Changamoto kubwa ni kuwa watu wengi wanaojihusisha katika uzalishaji kupitia sekta binafsi wapo katika kundi la sekta zisizo rasmi yaani hawajaweka mazingira kamili ya kisheria ili kile wanachofanya kiweze kutambuliwa na kuongeza tija kwa taifa kwa ujumla. Kwa lugha nyingine shughuli nyingi sana bado zipo kwenye ‘informal sector’. Sababu za kuendelea shughuli hizi za uzalishaji kuwa kwenye mazingira yasiyo rasmi zinaweza kuwa nyingi lakini moja wapo ni kutokufahamu mifumo ya kisheria ambayo ipo kwa ajili ya kuzirasimisha.

Ni kazi yetu kama uliza sheria kuendelea kutoa elimu kwa wadau na wasomaji wetu juu ya uhusiano wa sheria na biashara au shughuli mbalimbali wanazofanya kuzalisha mali ili kuendelea kuleta tija, ufanisi na manufaa kwa wafanyabiashara na Taifa letu kwa ujumla.

 

Faida za Kurasimisha Biashara/Shughuli katika mfumo wa Kisheria

Zipo faida nyingi sana kwa wafanyabiashara au watu wenye shughuli zao binafsi kufanya taratibu za kurasimisha na kuzifanya kwa mujibu wa sheria. Baadhi ya faida zinazopatikana ni kama ifuatavyo;

  • Biashara au shughuli kupata utambulisho rasmi kutoka katika mamlaka husika na kuwa na uhalali wa kuifanya pasipo usumbufu wa mara kwa mara
  • Wafanyabiashara zilizorasimishwa kujengewa mazingira bora ya kisera na kisheria kusaidia uendeshaji wa biashara zao
  • Wafanyabiashara kupata fursa zaidi za kuongeza mitaji kupitia mikopo au ubia na watu au wafanyabiashara wengine
  • Baishara zilizorasimishwa kuongeza thamani ya mauzo katika masoko yake
  • Biashara kufungua fursa za kufanyika hata nje ya mipaka ambayo kwa kawaida ilizoeleka
  • Taifa kuongeza wigo wa mapato ya kikodi kutoka katika biashara au shughuli zilizorasimishwa.

Ni rai yangu kwa wadau na wasomaji wetu kuendelea kutufuatilia katika kujifunza maeneo mbali mbali ya Sheria na Biashara ambayo tutakuwa tukiyachambua walau mara mbili kwa kila wiki. Pia rai yangu kwa mamlaka husika kuendelea kutafuta njia bora na rafiki kwa watu wengi ambao wanashughuli zao lakini hazipo kwenye mfumo rasmi. Nieleze wazi kuwa wakati mwengine urasimu wa kuanzisha biashara unasababisha usumbufu mkubwa kwa wale wenye nia njema lakini wanakwamishwa kutokana na mfumo kutokuwa rafiki au kukosa elimu ya kutosha na taarifa sahihi wakati wote.

Nikukaribishe sana ndugu yangu katika ukurasa huu mpya tukiendelea kujifunza.

Kumbuka kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili