Biashara Sheria.4. Biashara ya Mtu Binafsi

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa ukurasa wetu wa Biashara Sheria. Katika makala iliyopita tumeona mfumo wa uendeshaji biashara na mamlaka inayohusika na usajili wa biashara hizo. Tumeona juu ya makundi makuu 3 ya uendeshaji wa biashara kisheria na usajili wake. Leo tunakwenda kuchambua mojawapo ya aina ya biashara ya Mtu Binafsi. Karibu tujifunze.

Mfumo wa Biashara ya Mtu Binafsi

Huu ni mfumo wa biashara ya ngazi ya chini kabisa na imezoeleka kwa watu wengi. Mfumo huu wa biashara unafahamika kama ‘Sole Proprietorship’. Hii ni aina ya biashara binafsi inayoendeshwa na mtu mmoja ambaye anahusika kuzifanya shughuli zake au kwa usaidizi wa watu wengine kama waajiriwa wake.

Mifano ipo mingi ya aina ya shughuli kama hizi za biashara au huduma ya mtu binafsi kama maduka ya jumla na rejareja, wakala wa mitandao kama tigopesa, M-pesa, Airtel money, magenge, maduka ya vifaa mbalimbali, huduma za kitaalam za ushauri n.k.

Hii ni aina au mfumo wa biashara uliozoeleka ambao ni rahisi sana kwa kila mmoja wetu kuanzisha na kutekeleza tofauti na mifumo mingine.

Tofauti kubwa kati ya biashara binafsi na mifumo mingine ya biashara ni kwamba biashara ya aina hii haina utofauti wa kisheria kati ya mmiliki na biashara yenyewe. Hii ina maana kuwa mmiliki anawajibika kisheria kwa biashara yake kwa mambo yote ikiwa ni faida au hasara. Tofauti na mfumo wa kampuni ambao kisheria kampuni anajiendesha mbali na wamiliki wake.

Faida za Biashara Binafsi

Zipo faida nyingi za kuendesha biashara binafsi ambazo mwenye hiyo biashara anaweza kuzipata;

  • Hii ni aina ya biashara rahisi kimfumo na kuanzisha. Haiitaji masuala mengi ya kisheria ya kuzingatia bali unaanzisha na ukipenda kutumia jina lako binafsi au kusajili jina la biashara kwa wakala wa usajili unaweza kufanya hivyo kwa kujaza fomu maalum na kupata jina la biashara. Watu wengi wanaoanza biashara huanza kwa mfumo huu kwani ni nafuu kwa gharama na masharti ya uanzishwaji wake.
  • Katika mfumo wa biashara binafsi mmiliki anakuwa na umiliki wake kwa 100% hivyo anayo nafasi kubwa ya kufanya maamuzi yote yanayohusiana na biashara yake au huduma yake.
  • Katika mfumo wa kodi na mahesabu aina ya biashara binafsi ni rahisi sana na nafuu kuweza kulipa kodi kulinganisha na mifumo mingine ya biashara.
  • Gharama za mtaji wa unzishwaji wa biashara binafsi ni nafuu kutokana na malengo aliyonayo mfanyabiashara au mtoa huduma husika kulinganisha na aina nyingine za biashara.

Changamoto za Biashara Binafsi

Pamoja kuwa na mfumo rahisi wa uanzishwaji na faida nyingine ndani ya biashara binafsi, zipo changamoto ambazo zinaikumba aina ya mfumo huu wa biashara ambazo tungependa kuzijadili;

  • Kwa kuwa biashara hii haina utofauti na mmiliki wake, endapo itajitokeza hasara basi hatua za kisheria au madeni yanaweza kuathiri hata mali za mmiliki ambazo hazikuwepo kwenye biashara husika. Hii ina maana kwamba kama kutajitokeza madeni ambayo biashara imeshindwa kuyalipa basi si biashara tu itakayohusika kulipa bali hata na mali nyingine za mmiliki zinaingizwa katika sehemu ya njia za kulipa madeni husika.
  • Wakati mwengine katika masuala ya kodi biashara binafsi zinajikuta zinapaswa kulipa kodi hata katika mazingira ya kutokufanya vizuri katika biashara. Hii inatokana na mfumo wa wafanyabiashara wadogo kutokuwa na uwezo wa kutunza kumbukumbu vizuri za kimahesabu. Tofauti na mfumo wa kampuni endapo biashara haikufanyika ni rahisi kuonekana na kutolipishwa kodi kwa kiwango kile kilichokadiriwa.
  • Mara kwa mara mashirika au makampuni au serikali hupendelea zaidi kufanya kazi na makampuni kuliko watu binafsi, hivyo mfumo huu wa biashara binafsi unaweza kumnyima fursa mfanyabiashara au mtoa huduma kwa sababu ya udogo wa biashara yake na mfumo wake wa maamuzi kuwa ya mtu mmoja.
  • Endapo mfanyabiashara binafsi au mtoa huduma atakaposhindwa kuendelea na biashara kwa sababu ya ugonjwa au kifo au sababu nyingine yoyote ile mara nyingi biashara hiyo hufa pia.
  • Biashara binafsi ina changamoto ya kushindwa kuongeza mtaji kwani mtaji ni wa mtu binafsi tofauti na mfumo mwengine ambao wanaweza kupata mkopo kirahisi au kuuza hisa za kampuni.
  • Ni ngumu kuuza biashara binafsi kwa sababu hakuna utofauti wa mali za biashara na zile za mmiliki kutokana na umoja wa kisheria kati ya biashara na mmiliki. Hivyo ni ngumu sana kufahamu thamani halisi ya biashara husika.
  • Mara nyingi katika biashara binafsi kwa kukosa uzoefu na utaalam wa uendeshaji wamiliki wanashindwa kujua namna ya kujilipa ingawa wanafanya kazi katika biashara husika, hii inaathiri ukuaji wa biashara kwani wakati mwengine fedha za biashara zinaingizwa katika matumizi binafsi na pia zile binafsi zinaingizwa kwenye biashara.

Haya ni baadhi tu ya maeneo ya msingi ya kufahamu juu ya faida na changamoto zinazoikumba aina ya biashara binafsi.

Hitimisho

Muhimu kufahamu kuwa biashara na huduma ambazo wewe unakusudia au unataka kuanzisha unaweza kuanza kidogo kidogo. Wengi wanashindwa kuchukua hatua wakisubiri kitu kinachoitwa ‘mtaji’ hii wana maana ya fedha, lakini kwa aina ya mfumo huu gharama zake ni za chini kabisa. Wengi tayari wapo kwenye biashara lakini hawana msumkumo wa kuzisajili, kwa maarifa haya uchukue hatua za kufanya usajili kwani zipo faida nyingi sana ambazo zinaambatana na usajili wa biashara yako ambazo zitakufungulia fursa ya kufanya kwa mujibu wa sheria pasipo hofu huku ukitoa mchango wa ujenzi wa taifa lako.

Usikose tena kufuatilia katika makala ya Biashara Sheria wakati ujao tunapoendelea kuchambua mifumo hii ya kibiashara. Karibu.

Kumbuka kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili

4 replies
  1. Benedictor Richard
    Benedictor Richard says:

    Nashukuru sana kwa ushauri na elimu bora ya biashara….naomba kujua jinsi ya kugawana faida katika biashara ya ubia endapo mitaji au hisa katika ubia hazikua saw a.

    Asante.

Comments are closed.