Viashiria vya Kosa la Jinai

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa makala za Sheria Leo ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Katika makala iliyopita kwenye ukurasa huu tulianza kuangalia namna mbalimbali za utetezi kutokana na makosa ya kijinai. Leo tunakwenda kuangalia juu ya Viashiria vya Kosa la Jinai.

Historia ya Adhabu kwa Makosa ya Kijinai

Sheria kuhusiana na makosa ya kijinai ina historia ndefu sana katika ulimwengu huu. Awali mtu alikuwa anaadhibiwa tu endapo itadhibitika ni yeye aliyefanya kitendo ambacho jamii ilikuwa inaona ni cha kijinai. Adhabu haikutofautisha mtu yule aliyefanya kosa ikiwa ni kwa makusudi au kwa bahati mbaya wote hatma yao ilikuwa moja yaani kuadhibiwa kwa vitendo vyao walivyofanya.

Hatahivyo, baada ya muda na maendeleo katika masuala ya sheria za jinai na adhabu zake suala la kosa likaanza kutazamwa kwa mtazamo tofauti ili kutofautisha kati ya makosa yale yanayofanywa kwa bahati mbaya na yale ambayo yanafanyika kwa makusudi.

Hapa ndipo ilipozaliwa dhana ya kuwa mtu hawezi kuadhibiwa kutokana na kitendo alichofanya mpaka pale itakapodhibitishwa kuwa alikuwa amekusudia kutenda kitendo hicho.

Dhana hii inaelezwa kwa lugha ya kilatini kama ifuatavyo;

‘Actus non facit reum nisi mens sit res’

Msemo huu wa lugha ya kilatini unatafririwa kwa lugha ya kiingereza kama ifuatavyo;

 ‘the act itself does not constitute guilt unless done with a guilty intent’

Hii ina maana kwamba ‘kitendo peke yake hakiwezi kudhibitisha hatia ya mtu aliyetenda mpaka pale itakapodhibitishwa kuwa kilifanyika kwa makusudi ndani ya fikra za yule aliyetenda’.

Dhana hii ya kisheria imekuja kuleta suluhu kwa makosa ambayo yanafanyika na watu kuadhibiwa pasipo kupima endapo makosa husika yalifanyika na mtu aliyekuwa amedhamiria au la.

Hivyo sheria inatambua kuwa kosa ili lionekane kuwa ni kosa ni lazima viashiria vya kosa vidhibitishwe

  • Nia au dhamira ya kutenda kosa. Hii ni kiashiria kikubwa ambacho mahakama kabla haijamtia hatiani mtuhumiwa ni lazima idhibitishe kuwa kulikuwa na nia ya kutenda kosa
  • Kitendo ambacho kimezuiwa na sheria. Hiki ni kiashiria cha pili ambacho kitaonesha kuwa mkosaji alitenda jambo fulani ambalo ni kosa kisheria.

Katika makala zinazofuata tutaendelea kuchambua kwa undani juu ya viashiria hivi vya makosa ya kijinai ambavyo ni lazima vidhibitishwe na mahakama kabla ya kumtia mtuhumiwa hatiani.

Hitimisho

Leo tumeendelea kujifunza mambo ya msingi katika sheria za jinai kwa kuangalia suala zima la viashiria vya kosa la jinai. Kama nilivyoeleza kwenye makala zilizotangulia juu ya jamii kutoendelea na tabia za kujichukulia sheria mkononi kwani jamii inakuwa haina kipimo cha kuweza kujua suala fulani au kitendo fulani kilichofanywa na mtuhumiwa alikuwa na nia gani. Ni vyema kuchukua hatua za kisheria na kufuata mkondo wa kisheria wakati wote tunapokutana na masuala ya jinai ili vyombo husika vipate nafasi ya kuutafuta na kubaini ukweli na kila mmoja apate haki yake.

‘Anzisha na fuata mchakato wa kisheria katika kushughulikia masuala ya uhalifu katika jamii’

Kumbuka kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili

 

2 replies

Comments are closed.