54. Utendaji chini ya Kiwango

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala iliyopita tumeona juu yaUzembe Unaoathiri Utendaji wa Kazi. Leo tunaangalia juu kosa la Utendaji chini ya Kiwango. Karibu tujifunze.

Utendaji wa Kaza chini ya Kiwango

Sheria ya Kazi na Ajira inatambua kuwa mfanyakazi anaweza kuachishwa kazi kwa utendaji usioridhisha ‘poor work perfomance’.

Utendaji wa mfanyakazi usioridhisha ni hali ya kiwango cha utendaji chini ya viwango vya kazi vilivyowekwa na mwajiri. Sheria ya ajira inatambua haki ya mwajiri kuweka viwango vya kazi, hivi ni viwango ambavyo wafanyakazi wanapaswa kuvizingatia katika utendaji wao.

Utendaji chini ya kiwango ina maana kuwa mfanyakazi anashindwa kufanya kazi kwa mujibu wa viwango au vigezo vilivyowekwa na mwajiri. Kila mwajiri ana vigezo anavyozingatia katika utendaji na kutimizwa kwa majukumu ya kazi, endapo mfanyakazi ataajiriwa katika nafasi fulani anatarajiwa kufikia viwango hivyo. Kushindwa huko kufikia viwango kunaweza kusababisha kusitishwa kwa ajira yake.

Sheria ya Kazi na Ajira kupitia Kanuni za Utendaji Bora ‘Employment and Labour Relations (Code of Good Prictice)’ inaeleza kuwa mfanyakazi anaweza kuachishwa kazi kwa kosa la utendaji chini ya viwango vilivyowekwa na mwajiri.

‘Unacceptable work performance, behaviour or consistent work performance below average despite at least two written warnings’

Maana yake mfanyakazi anaweza kuchukuliwa hatua za kuachishwa kazi kutokana na utendaji chini ya viwango vilivyowekwa na mwajiri.

Hatua dhidi ya mfanyakazi kwa utendaji chini ya kiwango.

Vipo vigezo vya kisheria vinavyopaswa kuzingatiwa na mwajiri ili kuweza kuchukua hatua dhidi ya mfanyakazi katika suala la utendaji chini ya kiwango cha kazi. Kanuni za Utendaji Bora mahali pa kazi zinaeleza utaratibu huo.

  1. Uwepo wa viwango vya utendaji wa kazi

Sheria inamtaka mwajiri kabla ya kumchukulia hatua mfanyakazi kwa ajili ya utendaji chini ya viwango ni lazima viwepo viwango vya kikazi. Viwango hivi anavyoweka mwajiri vinapaswa kuwa vinafikika na vinafahamika na mfanyakazi husika.

  1. Uchunguzi wa Utendaji chini ya viwango

Kwamba kabla mwajiri hajamchukulia hatua mfanyakazi kwa utendaji chini ya kiwango ni lazima afanye uchunguzi ili kujua ni sababu zipi zinasababisha utendaji huo kuwa chini ya kiwango. Hapa mwajiri anapaswa kupata majibu kuhusu viwango alivyoweka ikiwa ni sahihi vinaweza kufikiwa, sababu za kushindwa kwa mfanyakazi, na endapo mfanyakazi alikuwa na ufahmu juu ya uwepo wa viwango.

  1. Kutoa mwongozo au mafunzo ya ziada

Baada ya kujiridhira kuhusu utendaji chini ya kiwango, mwajiri anapaswa kutoa mafunzo na mwongozo kwa mfanyakazi ili aweze kuboresha utendaji wake. Mwongozo na mafunzo yana lengo la kuimarisha mfanyakazi ili kuweza kumudu majukumu yake ipasavyo. Mwajiri hapaswi kuchukua hatua za kusitisha ajira pasipo kutoa nafasi ya mfanyakazi kuwa bora zaidi kwenye utendaji.

  1. Barua za Onyo

Kama hali ya utendaji wa mfanyakazi inazidi kuwa chini ya viwango, mwajiri anayo fursa ya kutoa barua za onyo kwa mfanyakazi husika akieleza kuwa endapo utendaji wake hautaridhisha basi anaweza kuchukuliwa hatua za kuachishwa kazi. Kanuni zinaeleza kuwa mwajiri anaweza kumwonya mfanyakazi juu ya utendaji wake chini ya viwango hata mara mbili. Ni muhimu kuwa maonyo haya yawe kwa maandishi ili iwe ushahidi kwa upande wa mwajiri kwamba alichukua kila hatua kama sheria inavyotaka.

  1. Kusitisha ajira

Hii ni hatua ya mwisho kabisa inayoweza kuchukuliwa na mwajiri endapo utendaji wa mfanyakazi utaendelea kuwa chini ya viwango. Mwajiri anapaswa kufuata taratibu zote za usitishaji wa ajira kwa kuitisha kikao pamoja na mfanyakazi ambaye atapewa fursa ya kujitetea au kuwakilishwa na mfanyakazi mwenzake au kiongozi wa chama cha wafanyakazi mahali pa kazi. Mwajiri anapaswa kuzingatia utetezi utakaowasilishwa na mfanyakazi na kutoa maamuzi. Uamuzi wa usitishwaji wa ajira utafanyika kwa maandishi.

Huu ndio utaratibu wa kusitisha ajira ya mfanyakazi kutokana na utendaji chini ya viwango vilivyowekwa na mwajiri mahali pa kazi

Hitimisho

Waajiri wengi wanawatuhumu wafanyakazi kuwa hawatendi kazi kama inavyotakiwa, ila cha ajabu hakuna viwango vya kikazi vilivyowekwa ambavyo mfanyakazi anapaswa kuvisikia. Hivyo hatua zozote anazochukua mwajiri kusitisha ajira au kumwadhibu mfanyakazi kwa kigezo cha utendaji mbovu pasipo kuwa na viwango husika vya kuzingatia ni kinyume cha sheria ya Ajira. Muhimu sana mwajiri kuweka vigezo na mfanyakazi ajitahidi kufikia vigezo husika ili kupatikane ufanisi mahali pa kazi.

Kwa ushauri zaidi usisite kuwasiliana nasi kama inavyoelekezwa hapo chini katika makala hii.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com

1 reply

Comments are closed.