Sheria Leo. Mambo 5 Muhimu ya Kisheria Kuzingatia 2019

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Leo kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tumeukaribisha mwaka mpya wa 2019, tunamshukuru Mungu aliyetupa kibali kuvuka salama hata sasa. Makala ya leo ni kwa ajili ya kujiandaa na maisha yetu katika kuishi kwa mujibu wa sheria siku ambazo Mungu atatujalia katika mwaka huu. Karibu sana katika makala yetu ya msingi kwa siku ya leo.

Umuhimu wa Sheria

Katika makala nyingi zilizotangulia na hasa msingi wa kutoa mafunzo haya ya kisheria ni kusisitiza kwa jamii nzima kutambua umuhimu wa sheria katika maisha yetu ya kila siku. Sheria ndio kiongozi wa maisha yetu ndio mfumo na kanuni tunazopaswa kuzingatia kila iitwapo leo. Sheria zinatungwa na mamlaka za Bunge, kusimamiwa na Serikali na kupata tafsiri kutoka Mahakamani.

Naamini ni makusudi ya kila mmoja wetu kuishi kwa mujibu wa sheria, yaani asipatwe na matatizo ya kuvunja sheria. Hatahivyo, ni miongoni mwetu katika mwaka huu tunaweza kujikuta tumevunja sheria au kupata matatizo ya kisheria na hatimaye kupata adhabu. Wapo watu wengi magerezani au katika mahakama au vituo vya Polisi kwa kutokuzingatia mambo ya msingi ambayo katika siku ya leo ningependa kukushirikisha ili angalau yakusaidie kupunguza hatari ya kuvunja sheria na kujikuta katika adhabu.

Mambo 5 ya Kisheria ya Msingi kuzingatia 2019

Katika makala yetu ya leo, ninakuletea mambo 5 ya msingi ambayo mimi na wewe tunapaswa kuyazingatia katika kuishi kwa mujibu wa sheria ndani ya mwaka huu wa 2019. Karibu tujifunze.

  1. Tafuta Elimu ya Kisheria

Taaluma ya kisheria ni mojawapo ambayo ina watu wachache sana ambao wameisoma na kuifanyia kazi japokuwa sheria inapaswa kutumiwa na kila mmoja wetu. Si wananchi wote ambao wamepata nafasi ya kujifunza masuala ya kisheria ingawa ni wananchi wote wanapaswa kuishi kwa mujibu wa sheria. Katika zama hizi za sayansi na teknolojia ikiwa mtu unataka au una nia ya kujifunza jambo lolote inawezekana kwa kupitia vitabu mbalimbali, makala au mitandao ya intaneti. Kwa vyovyote vile mwaka huu weka nia na malengo ya kujifunza mambo mbali mbali ya kisheria kwa ajili ya maisha yako. Kumbuka usemi usemao ‘kutokujua sheria si utetezi endapo utafanya kosa kinyume na sheria’. Mahakama au washitaki wako hawatakubali sababu yako ya kusema hukujua kama matendo yako yalikuwa kinyume cha sheria. Hivyo chukua hatua madhubuti kujipanga mwaka huu kwa kupata elimu ya kisheria kwa gharama yoyote.

  • Tafuta Ushauri wa Kisheria

Kila mmoja wetu katika maisha yetu anakuwa na nafasi ya kufanya maamuzi. Wakati mwengine maamuzi tunayofanya hatujui athari zake za mbele au za karibu. Wengi tunafanya maamuzi kwa mazoea kwa kuwa jana tulifanya maamuzi kama hayo na hatukuona madhara. Jambo muhimu sana la kuzingatia katika kuishi maisha kwa mujibu wa sheria mwaka huu ni kupata ushauri wa kisheria endapo unahitaji kufanya maamuzi ya msingi. Mathalani unataka kununua eneo au kuingia makubaliano yoyote, tafuta ushauri wa kisheria kwanza kabla hujafanya maamuzi yanayoweza kuleta hasara. Wengi wanaogopa gharama za kupata ushauri na wanaishia kufanya maamuzi yenye hasara kubwa kwa kukosa ushauri. Kama unafanya jambo ambalo unajua litahitaji utaalamu wa kisheria ni vyema kutafuta ushauri kwanza ndipo ufanye maamuzi.

  • Fuata Sheria

Sheria ni kiongozi. Sheria imewekwa kwa ajili yetu sote ili tuishi kwa amani na ustahimilivu pasipo kukwazana. Kutokana na jamii yetu kuwa na watu wenye utashi tofauti sheria ni muhimu. Unapojua sheria basi chukua hatua kwa kufuata sheria usitafute njia ya mkato katika kutimiza kazi zako au wajibu wako. Wapo wengine wanasema ‘sheria zipo ili zivunjwe’ huu si msemo mzuri kwako kwani gharama ya kuivunja sheria inawezekana kupoteza uhuru wako au kupata hasara kubwa. Tujifunze kufuata sheria katika kila jambo tunalolifanya ili maisha yetu yaendelee kuwa bora siku kwa siku.

  • Weka mambo yako Kisheria

Ni tabia ya watu wengi kutokuwa na maandalizi ya kutosha hasa kwa mambo muhimu sana kwa maisha yao. Unakuta mtu anazo mali lakini hazina nyaraka za uthibitisho kuwa ni zake au amezipata vipi. Hatujui kama tumeingia mwaka huu 2019 endapo tutaumaliza au la. Moja ya eneo lilaloleta migogoro ni masuala ya mirathi ambapo husababishwa na watu kutoandika wosia kueleza juu ya mali zao endapo watafariki. Kama una mali au makubaliano yoyote hakikisha unayaweka kimaandishi na yanajulikana na watu wako wa karibu unaowaamini ili chochote kitakachotokea basi haki yako isipotee.

  • Tafuta Usaidizi wa Kisheria

Hii ni hatua muhimu sana katika kufanikisha maisha yako kwa mujibu wa sheria mwaka huu 2019. Tunafahamu kuwa wataalamu wa kisheria si wengi katika nchi yetu, hata hivyo endapo mtu unayo nia ya dhati ya kupata usaidizi wa kisheria basi utaweza kupata. Wananchi wengi wanaogopa gharama, lakini zipo taasisi zinazotoa usaidizi wa kisheria bure katika masuala ya kisheria. Chukua muda kutafuta usaidizi kuliko kuamini tu akili zako na mwisho wa siku unaweza kujikuta unaingia matatizoni na hata kupoteza uhuru wako kwa kukosa usaidizi wa kisheria au uwakilishi kwenye mashauri mbalimbali. Uzoefu unaonesha wengi wanaofungwa gerezani ni kukosekana uwakilishi wa wanasheria katika mashauri yao.

Hitimisho

Ndugu msomaji wa mtandao wa uliza sheria, hayo ndiyo mambo 5 ya msingi ambayo nimependa kukushirikisha mwaka mpya huu wa 2019 ambayo unapaswa kuyazingatia siku kwa siku. Kwa kuzingatia mambo haya haimaanishi kuwa hautapata misukosuko bali utakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kubabiliana na matatizo au changamoto za kisheria ambazo utakutana nazo.

Nikutakie heri ya mwaka mpya wa 2019 wenye mafanikio katika malengo yako yote, na Mungu atujalie kuanza salama na kuumaliza kwa kupiga hatua kubwa zaidi.

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com

4 replies
  1. edson.G.mdesa
    edson.G.mdesa says:

    nashukuru kwa maelezo manzuri naomba shirikiano wa hali na mali kwa maana kunakitu nakihitaji kukijua na nini nifanye

Comments are closed.