59. Je, Mwajiri ana haki ya kukata mshahara bila utaratibu?

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala ya Uchambuzi wa Sheria .9 tuliangalia kwa mapana juu ya haki ya Ujira ambayo anastahili mfanyakazi. Haki hii hutokana na kazi ambayo anaifanya mfanyakazi na makubaliano waliyoafikiana na mwajiri. Hata hivyo kumekuwa na malalamiko mbalimbali ya wafanyakazi juu ya waajiri kukata mishahara yao au hata kuizuia kabisa pasipo sababu za msingi. Leo tunakweda kujibu swali hili, iwapo mwajiri ana haki ya kuzuia au kukata mshahara wa mfanyakazi pasipo utaratibu. Karibu tujifunze.

Haki ya Ujira

Mfanyakazi yeyote aliyeajiriwa ana haki ya kulipwa mshahara wake ndani ya muda uliokubaliwa na pande zote na si vinginevyo. Kifungu cha 27 cha Sheria ya Ajira kinaeleza wazi juu ya jukumu la mwajiri kumlipa mfanyakazi mshahara wake. Endapo makubaliano baina ya pande mbili ya kwamba mshahara ulipwe kwa kutwa basi unapaswa kulipwa hivyo, ikiwa ni kwa wiki au kwa mwezi basi unapaswa kulipwa hivyo.

Mwajiri haruhusiwi kufanya makato yoyote katika mshahara wa mfanyakazi isipokuwa aina ya makato ambayo yanaruhusiwa kisheria;

  • Kwa mujibu wa sheria kama vile kodi, michango ya pensheni n.k
  • Kwa amri ya mahakama au Tuzo ya Mwamuzi
  • Marejesho ya mkopo iwapo mfanyakazi ameelekeza au kuridhia kwa maandishi
  • Ada ya Chama cha Wafanyakazi baada ya kutoa idhini kwa Fomu TUF

Pia mwajiri anayo haki ya kukata mshahara wa mfanyakazi endapo ni kwa ajili ya kufidia hasara iliyojitokeza na uzembe au makosa ya mfanyakazi kuhusiana na mali ya mwajiri. Hatahivyo waajiri wengi hutumia mwanya huu kukandamiza haki ya mfanyakazi na kumkata mshahara pasipo kuonesha ni hasara kiasi gani na mfanyakazi endapo amepatiwa fursa ya kupinga ukataji huo wa mshahara.

Sheria inaongoza hata hivyo kabla ya kuchukua hatua husika ya kumkata mfanyakazi mshahara kutokana na uzembe mambo ya msingi kuzingatiwa;

  • Mwajiri lazima azingatie utaratibu wa haki
  • Hasara au uharibifu umetokea wakati mfanyakazi akiwa kazini na kwa sababu ya kosa la mfanyakazi
  • Mwajiri anampa mfanyakazi maelezo ya maandishi ya kiasi cha hasara, chanzo cha uharibifu au hasara na hesabu za namna deni hilo lilivyofikiwa
  • Mfanyakazi anapewa nafasi ya kujitetea na kupinga deni hilo, chanzo na namna hesabu za deni hilo zilivyofikiwa
  • Jumla ya deni isizidi kiwango halisi cha hasara au uharibifu
  • Makato yasizidi ¼ ya mshahara wa mfanyakazi

Kama tulivyoona katika maelezo ya makala hii, hizi ndizo sababu kuu zinazoweza kusababisha mwajiri amkate mshahara mfanyakazi na si vinginevyo kama waajiri wengi wanavyowafanyia wafanyakazi. Wapo waajiri ambao wanawakata wafanyakazi mishahara zaidi ya ¼ kama sheria inavyoonesha. Wengine hawalipi kabisa mshahara kwa kisingizio cha kufidia hasara ambayo mwajiri anadai imesababishwa na mfanyakazi.

Hitimisho

Ni muhimu sana kwa mwajiri kuzingatia matakwa ya kisheria katika suala zima la mishahara ya wafanyakazi kwa kuhakikisha mshahara unalipwa kwa wakati na si vinginevyo. Pia wafanyakazi wanapaswa kuwa makini katika kuzijua sababu zinazoweza kusababisha mishahara kukatwa endapo ni sababu za kisheria na zenye haki.

Endelea kufuatilia mfululizo wa makala hii ambapo tutaeleza hatua zinazoweza kuchukuliwa dhidi ya mwajiri anayekata mishahara au kuzuia mshahara kinyume cha sheria.

Kwa ushauri zaidi usisite kuwasiliana nasi kama inavyoelekezwa hapo chini katika makala hii.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com