72. Namna bora ya kupata Mwajiriwa mwenye vigezo

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala zilizotangulia tumeangalia mambo mbalimbali yanayohusu sheria za kazi na namna zinavyoathiri mahusiano baina ya mfanyakazi na mwajiri. Tumeanza kujifunza kanuni mbalimbali ambazo mwajiri anapaswa kuzingatia pale anapokusudia kuajiri mfanyakazi. Makala iliyopita tujifunza Kanuni ya pili juu ya Kufanya uamuzi wa aina ya mkataba wa kiajira pamoja na uchambuzi wa athari za kisheria kwa kila aina ya mkataba.

Leo tunakwenda kuangalia juu ya Kanuni ya namna bora ya kupata mwajiriwa mwenye vigezo. Karibu tujifunze.

Mfumo wa kupata mwajiriwa

Kwa sehemu kubwa hasa kwenye taasisi au Serikali nafasi za kazi hutangazwa kwa lengo la kupata waombaji wenye kukidhi vigezo vya kuweza kuajiriwa katika nafasi husika.

Katika nyakati za karibuni, tumeshuhudia hali ya ukosefu mkubwa wa ajira hasa kwa kundi kubwa la vijana ambao wamehitimu mafunzo katika ngazi mbalimbali. Hali hii imechangia zoezi la usaili kwa lengo la kupata mwajiriwa au waajiriwa wanaokidhi vigezo kuwa gumu zaidi na kuchukua muda mrefu.

Hata hivyo bila kujali changamoto hizi, zoezi la kupata mwajiriwa bora wa kujaza nafasi ambayo taasisi au mwajiri anaona inamhitaji mtu ni lazima lifanywe kwa weledi mkubwa sana pasipo kuhusianisha aina yoyote ya upendeleo kwa wale wanaotaka kujaza nafasi hiyo.

Kanuni ya 3

Namna bora ya kupata Mwajiriwa

Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Na.6 ya 2004 inatamka wazi ya kuhusiana na mchakato mzima wa usimamizi katika kutafuta na kumpata mtu anayestahili kujaza nafasi ya kuajiriwa mahali pa kazi sawa na Kifungu cha 7(1),(9) (a) (b) na (c) cha Sheria ya Ajira ya 2004

(1)‘Kila mwajiri atahakikisha kwamba anakuza fursa sawa katika ajira na kupambana kutokomeza ubaguzi katika Sera yoyote ya ajira au katika utendaji’

(9) Kwa maudhui ya kifungu hiki;-

  • ‘mwajiri’ ni pamoja na wakala wa ajira;
  • ‘mwajiriwa’ ni pamoja na anayeomba kuajiriwa;
  • ‘sera au utaratibu wa ajira’ ni pamoja na sera au utaratibu wowote unaohusiana na taratibu za kuajiri, vigezo vya utangazaji na uchaguzi, uteuzi na mchakato wa uteuzi, uainishaji wa kazi na madaraja, ujira, faida za ajira na kanuni na masharti ya ajira, upangaji wa kazi, mazingira ya kazi na vifaa, mafunzo na maendeleo, mifumo ya tathmini, unadishaji vyeo, kushusha cheo, kuachisha kazi na hatua za nidhamu

Vifungu hivi tulivyonukuu vinaanisha wazi kuwa ni lazima mwajiri azingatie matakwa ya kisheria katika kuhakikisha kwenye zoezi zima la kuajiri hakuna viashiria vya ubaguzi.

Mambo ya msingi kuzingatia

  • Zoezi la kupata mwajiriwa lazima liendeshwe kwa usawa bila kujali rangi; utaifa; kabila au mahali anapotoka mwajiriwa; mbari/ukoo; taifa atokako; asili ya jamii; mwelekeo wa kisiasa au udini; jinsi; jinsia; ujauzito; hali ya ndoa au majukumu ya kifamilia; ulemavu; VVU/UKIMWI; umri au hali ya maisha. Hii ni kwa mujibu wa Kifungu cha 7 (4) cha Sheria ya Ajira.
  • Masharti ya kuajiri hayambani tu mwajiri bali hata wakala wa mwajiri. Tunafahamu kuwa zipo taasisi ambazo zinafanya kazi ya uwakala wa kuajiri kwa niaba ya waajiri. Sheria inawabana pia mawakala kuzingatia taratibu za kuajiri kwa haki.
  • Masharti haya ya ajira yanamlinda mwombaji wa ajira. Ni mara nyingi tunafikiri mwenye haki ya kulalamika kuhusiana na masuala ya ajira ni mwajiriwa tu. Sheria ya Ajira imeweka wazi kuwa hata mwombaji wa ajira ana uwezo wa kulalamika dhidi ya mwajiri au wakala wake endapo kutadhibitika vitendo vya ubaguzi vimefanyika katika zoezi la kuajiri. Tume au Mahakama ina mamlaka ya kusikiliza malalamiko ya waomba ajira endapo misingi ya kuajiriwa au zoezi au sera zilionesha ubaguzi.
  • Sera na utaratibu wa ajira. Sheria ya Ajira inamtaka mwajiri yeyote kuhakikisha sera kuhusiana na namna ya kuajiri ipo wazi kwa watu wote na yenye kuzingatia usawa wakati wote. Masuala yote ya msingi ni lazima yajulikane na vigezo vitakavyotumiwa kuhakikisha anapatikana mtu aliye bora zaidi.

Haya ndio masuala ya msingi ya kisheria anayopaswa mwajiri kuzingatia pindi anapoanzisha mchakato wa kutafuta mwajiriwa kwenye nafasi ya kazi. Ni muhimu sana kuzingatia masharti haya wakati wote kwani kinyume na hapo waleta maombi ya ajira wanaweza kufungua mgogoro wa ubaguzi dhidi ya mwajiri.

Katika makala ijayo, tutaelezea juu ya masharti mengine ambayo mwajiri anaweza kuzingatia ili kuhakikisha anapata mwajiriwa bora zaidi.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com

2 replies
  1. Hillary Mrisso
    Hillary Mrisso says:

    Kazi nzuri sana Zake, mambo haya wanatakiwa wayafahamu waajiri pamoja na waajiriwa, jukosekana kwa elimu ya msingi kama hii kumezaa malalamiko, uzembe, na kukosekana kwa ufanisi kazini.Hali hii ndio husababisha migogoro mingi kwenye maeneo ya kazi, hats pale mtu anaposhindwa kuelewa majukumu yake na haki sake za msingi ni chanzo cha migogoro pia.

Comments are closed.