74. Kwa Nini vigezo hivi 2 ni muhimu zaidi?

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala zilizotangulia tumeangalia mambo mbalimbali yanayohusu sheria za kazi na namna zinavyoathiri mahusiano baina ya mfanyakazi na mwajiri. Tumeanza kujifunza kanuni mbalimbali ambazo mwajiri anapaswa kuzingatia pale anapokusudia kuajiri mfanyakazi. Makala iliyopita tulianza kujifunza Kanuni ya tatu juu ya Namna bora ya kupata mwajiriwa mwenye vigezo. Tumeona juu ya vigezo vya kisheria na vigezo vya ziada katika kupata mwajiriwa bora zaidi miongoni mwa waombaji mbalimbali.

Leo tunakwenda kuangalia vigezo 2 muhimu zaidi vya ziada vya kupata mwajiriwa bora. Karibu tujifunze.

Vigezo vya Ziada

Katika makala iliyopita tumeweza kujifunza juu ya vigezo muhimu vya ziada anavyoweza kutumia mwajiri ili kupata mwajiriwa bora zaidi. Vigezo hivyo ni;

  • Kigezo cha kitaaluma
  • Kigezo cha uzoefu
  • Kigezo cha ubunifu
  • Kigezo cha uaminifu
  • Kigezo cha ushirikiano
  • Kigezo cha kujifunza

Vigezo hivi si kuwa ndivyo vyote au vimeisha kwa mwajiri kuzingatia la hasha vipo vigezo vingine vingi ambavyo mwajiri anaweza kuvitumia kupata mwajiriwa bora, mfano kigezo cha nidhamu na bidii katika kazi n.k

Hatahivyo kuna vigezo muhimu sana kati ya hivi 6 ambavyo nilianisha katika makala iliyopita vinavyopaswa kupewa kipaombele cha hali ya juu zaidi katika kuchagua aina ya mwajiriwa bora zaidi kati ya wengi walio bora.

Moja kati ya changamoto zinazowakuta waajiri, ni pale wanapotatizwa na waombaji ambao wamefungana maksi katika usaili iwe wa kuandika na mdomo. Wanapata changamoto ya kujua ni mwajiriwa yupi kati yao wamwajiri. Inafikia mahali wanaamua kwa kupiga kura au kutazama jinsia ya mtu na kufanya uamuzi. Bado mwajiri anao uwanda mkubwa sana wa kuongeza vigezo na kuwapa fursa waombaji kuonesha uwezo wao katika kazi husika.

Vigezo ambavyo vinapaswa kupewa umuhimu wa ziada katika kufanya uchaguzi wa mwajiriwa ni kigezo cha Kujifunza na Ubunifu mahali pa kazi. Nitaeleza umuhimu wa vigezo hivi.

Kwa nini kigezo cha kujifunza ni muhimu zaidi?

Wahitimu wengi katika ngazi mbalimbali za vyuo pindi wanapomaliza shule hitaji lao la kwanza ni kutafuta ajira. Kipindi chote wanapokuwa vyuoni wanahangaika kuhakikisha wanafaulu mitihani yao. Kile ambacho hawajui ni kwamba kwa sehemu kubwa elimu wanayoipata mashuleni au vyuoni haina uhusiano wa moja kwa moja na kazi wanazopaswa kufanya. Hii ina maana uwezo wa kufaulu darasani haimaanishi utaweza kukusaidia katika kufanikisha majukumu ya kazi unayotaka kufanya. Kigezo cha kujifunza ninachoeleza hapa si suala la kujifunza na kupata vyeti bali hali ya mtu kuendelea kutafuta maarifa zaidi kila siku kwa lengo la kuboresha kazi yake.

Unaweza kusema sasa mtu hana kazi au hajaajiriwa, je atajifunza kitu gani wakati hajui kazi atakayoifanya? Ni swali zuri, lakini ukiona mtu anakosa cha kuendelea kujifunza katika maisha yake ujue hata alichokuwa anasoma hakuwa na hakika nacho huko shule au chuo. Maana yake hakujua kwa nini alienda kusoma kozi au aina ya masomo aliyosoma. Hii ni changamoto kubwa sana watu wengi wanaenda shule kwa lengo la kupata cheti ili watumie cheti kupata ajira, wakati mfumo wa ajira unataka watu wanaoweza kutatua matatizo ya leo bora zaidi kuliko yalivyokuwa yanatatuliwa siku zilizopita.

Hii ndio sababu kubwa ya waajiri wengi wanaweka kigezo cha uzoefu kazini. Wahitimu wanalalamika kuwa ndio kwanza wametoka shule au chuo hawana uzoefu wa kutosha katika kuifanya ile kazi. Lakini wasichojua uzoefu wanaweza kuupata kwa njia ya kujifunza kwa wenye uzoefu wa maeneo hayo ya kazi kwa kusoma vitabu. Utamaduni wa kujisomea vitabu katika nyakati hizi umepotea sana. Watu ni wavivu sana kusoma na kutafuta maarifa ila wana bidii sana kusoma na kupata cheti, wakidhani cheti ni tiketi ya kazi wakati maarifa ndio msingi.

Ni ushauri wangu kwa mwajiri yeyote nchini akitaka kuondoa utata juu ya nani amwajiri aweke kigezo cha mtu anayejifunza kwa kusoma vitabu vya maarifa mbalimbali ya kuboresha kile anachofanya. Mwajiri usiangalie sana juu ya uzoefu wa mtu aliyefanya kazi hiyo kwani wengine wana uzoefu mbaya na wanaweza kuwa chanzo cha kupungua ufanisi. Weka kigezo cha watu wanaojifunza, uliza maswali mtu anasoma vitabu vingapi kwa mwezi au mwaka, kwenye usaili wa maandishi atoe muhtasari wa vitabu alivyosoma, watu wa aina hiyo ni wachache sana na ndio bora. Wanaojenga tabia ya kujifunza ni watu wanaoweza kutoa tija zaidi mahali pa kazi kwa sababu wanapata mawazo mapya kila siku kutokana na uzoefu wanaoupata katika kujifunza.

Kwa nini kigezo cha ubunifu ni muhimu ziadi?

Kama tulivyoona katika makala iliyopita juu ya kuweka vigezo vya ziada kwa waajiriwa, tulizungumza kigezo cha ubunifu kama kigezo kimojawapo muhimu katika kupata mwajiriwa bora zaidi miongoni mwa waombaji bora. Ubunifu ni uwezo wa mtu binafsi kufanya mambo yale yale kwa njia mpya au namna bora zaidi kuliko yalivyokuwa yakifanywa hapo awali. Naamini ni lengo la kila taasisi kupiga hatua za kimaendeleo katika shughuli au huduma wanazotoa. Changamoto kubwa hatuoni maendeleo mahali pa kazi ni kwa sababu ya waajiriwa ambao miaka nenda miaka rudi wanafanya kitu kile kile kwa namna ile ile. Hali hii hudumaza kabisa shughuli au huduma za mwajiri. Kila siku zinaibuka changamoto mpya duniani ambazo zinahitaji namna mpya ya kuzishughulikia. Wale ambao wana akili au rasilimali watu wenye hali ya ubunifu wanapiga hatua kubwa zaidi ya wengine.

Ni ushauri wangu kwa waajiri kuhakikisha ya kuwa kigezo cha ubunifu mahali pa kazi ni muhimu sana uoneshwe na mtu anayetaka kuifanya kazi husika. Katika usaili ni lazima mtu aulizwe juu ya nafasi anayotaka kufanya kazi na kitu gani cha tofauti anachoweza kutoa kwa taasisi ambacho taasisi haijawahi kufanya au namna bora zaidi ya kutoa huduma. Waombaji wengi hawafikirii ni kitu gani wanaenda kufanya tofauti na waliopo mahali pa kazi. Wanaajiriwa kazini baada ya muda wanafanana na wale waliowakuta. Hakuna ufanisi, tija wala maendeleo katika kazi. Katika usaili waombaji wa kazi waulizwe maswali ya namna ya kuonesha ubunifu wao katika mahali pa kazi kwa lengo la utatuzi wa changamoto zinazowakuta.

Waajiri waache kuzingatia vigezo ambavyo haviwezi kutoa ufanisi kwa muhusika bali wazingatie vile muhimu kabisa ili kupata mtu bora zaidi.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Isaack Zake, Wakili

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com