Sheria Leo. Je, wazijua tabia kuu 3 za sheria?

Utangulizi

Habari za leo ndugu msomaji wa ukurasa wa Sheria Leo. Naamini tupo pamoja katika kuendelea kujifunza juu ya sheria kupitia makala hizi za maarifa ya kisheria. Leo nakuletea somo linalosema Zijue Tabia Kuu 3 za Sheria ili uweze kushirikiana nayo vizuri. Ndugu msomaji ni muhimu sana kwetu kufahamu mambo haya wakati tunajenga msingi wa maarifa ya kisheria. Kama ilivyo kwa mahusiano ya kibinadamu kwa kadri unavyomfahamu mtu kwa tabia yake inakurahisishia namna ya kushirikiana naye. Watu wengi hawapendi kusikia chochote kuhusu sheria, wengi wanaona sheria ni kama adui yao, lakini sivyo inavyotakiwa kuonekana bali sheria inaweza kuwa rafiki yako kama ukiifahamu tabia zake na lengo lake kwa maisha yako ya sasa na baadae. Fuatana nami tena katika darasa hili la sheria leo.

Kabla hatujaingia kwenye somo letu la leo ni vyema nikakukumbusha juu ya lengo la sheria, ili mahali unapoona au unapotakiwa kufuata sheria ujue ni kwa sababu gani ya msingi.

Lengo la sheria

Kama tulivyoainisha awali katika makala ya kwanza ya utangulizi ya Nini Maana ya Sheria? tuliweza kuchambua kwa kina maana ya sheria na vipengele muhimu vya kuzingatia katika kujenga tafsiri ya neno sheria.

Lengo kuu la sheria ni kuhakikisha inaleta usawa katika mgongano wa maslahi ya watu ili kila mmoja anapata haki yake kwenye jamii ambayo inaongozwa na sheria. Kama tunavyofahamu sheria imekuja katika jamii kuhakikisha maslahi ya jamii nzima yanazingatiwa hivyo wanajamii kuisha kwa amani, utulivu na kujiletea maendeleo yao.

Tabia za Sheria

Kama vilivyo vitu vingi vilivyoundwa na jamii ya watu, sheria nayo ina tabia zake za msingi. Katika utendaji kazi wa sheria tunaweza kuona tabia hizi zikidhiirika mara kwa mara. Zifuatazo ni kati ya tabia za sheria zinazodhihirika pale inapofanya kazi;

  • Sheria ni ya jumuiya: tabia hii inadhiirishwa kuwa namna ambavyo sheria inatungwa na kutumika inawahusu jumuiya na si mtu mmoja pekee. Sheria inatungwa kuhakikisha wahusika wote wanatii sheria inayowahusu. Mfano sheria za wanafunzi, wafanyakazi au wafanyabiashara au wanajamii zitawalenga watu wote wanaohusika katika makundi hayo.
  • Sheria ina nguvu ya kulazimisha uifuate: hii inaonesha kuwa yeyote ambayo sheria hiyo inamhusu lazima ahakikishe anaitii na kuifuata. Hakutakuwa na mtu ambaye atasema yeye hayuko chini ya sheria hiyo endapo imetungwa kuongoza matendo ya kundi husika.
  • Sheria ina adhabu: tabia hii inaonekana kwa aina ya sheria ambazo kutokutii kwake au kuifuata kunapelekea kupata adhabu. Adhabu inawekwa kwa lengo la kuhakisha sheria inafuatwa. Mfano wa adhabu ni kama faini, fidia au kifungo n.k

 

Hitimisho

Ndugu msomaji naamini leo tena umeongeza ufahamu wako juu ya Lengo na Tabia za sheria ambazo tumejifunza.

Kumbuka lengo la sheria ni kuhakikisha inaondoa mgongano wa maslahi ya kila mmoja kwenye jamii ili maslahi mapana ya wanajamii yaweze kufanikiwa na watu wapate kuishi kwa amani, utulivu na maendeleo.

Sheria ina tabia ya kuhushisha jamii/jumuiya, ina nguvu ya kulazimisha uifuate na inaambatana na adhabu endapo itavunjwa.

Hivyo ndugu msomaji usiwe mjinga wa kutokujua sheria maana hata usipoijua inaweza ikawa inakuhusu kama mwanajamii, inakulazimu uifuate na endapo utaivunja adhabu itakufuata.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

Wako

Isaack Zake, Wakili