Sheria Leo. Sheria za Umma
Karibu sana kwa siku ya leo ndugu yangu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa wa Sheria Leo. Tunaendelea kukuletea maarifa ya kisheria kwa uchambuzi wa masuala kadhaa ya kisheria. Tumekuwa na mfululizo wa kuchambua makundi ya sheria ambayo tuliyaaninisha kwenye makala Yatambue Makundi ya Sheria. Leo tunakuletea ufafanuzi juu ya uchambuzi wa Sheria za Umma. Karibu tujifunze
Maana ya Sheria za Umma
Ni aina ya kundi la sheria zinazotungwa kwa lengo la kuratibu mahusiano baina ya Serikali na wananchi, na mahusiano baina ya wanajamii ambayo jamii ina maslahi nayo. Hizi ni sheria zinazotungwa ili kueleza inapaswa kufanya nini juu ya wananchi na wananchi wanapaswa kufanya nini juu ya Serikali.
Sheria hizi zinaratibu haki na wajibu wa Serikali pamoja na haki na wajibu wa wananchi. Kama tunavyofahamu Serikali inaundwa kwa sheria kama chombo cha kusimamia na kutekeleza sheria. Hivyo sheria hizi za umma zinaundwa kuongoza mienendo ya Serikali katika kutimiza wajibu wake kwa wana jamii.
Sheria za Umma zinalenga katika kuainisha mihimili ya dola yaani Bunge, Serikali na Mahakama, majukumu yake. Pia zinaainisha wajibu wa nafasi za kisiasa, mamlaka,haki, wajibu wa viongozi mbali mbali wa Umma. Hivyo ni kusema sheria za Umma zinaongoza tabia na mienendo ya watumishi wa umma vile ambavyo wanatakiwa kuwatendea wanajamii na pia namna wanajamii wanatakiwa kuenenda kwa kufuata sheria zinazosimamiwa na watumishi wa Umma.
Maeneo ya Sheria za Umma
Wigo wa sheria za umma ni mpana sana lakini kwa uchache sheria hizi zinazungumzia maeneo makuu manne yaani;
- Sheria ya Katiba
- Sheria za Uongozi
- Sheria za Kodi
- Sheria za Jinai
Mara zote Sheria za Umma zinahusisha angalau makundi haya ya sheria ambayo tutayafafanua katika makala zinazofuata.
Hitimisho
Kundi hili la sheria za Umma ni muhimu sana kwa wananchi kuzifahamu kwani zitasaidi wao kujua namna ya kuwajibika kwa mujibu wa sheria na namna ya kudai haki zao ikiwa zimezuiwa kutokana na watumishi husika kutokutimiza wajibu wao.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kwa kutembelea mtandao wako wa www.ulizasheria.co.tz
Wako
Isaack Zake, Wakili