Sheria Leo. Ijue Sheria ya Madhara

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa makala za Sheria Leo ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Hivi karibuni tumekuwa na mfululizo wa makala za makundi ya sheria. Tumeanza mfululizo wa makala 10 za utabulisho wa baadhi ya sheria ambazo zina matumizi ya kila siku kwa mwananchi. Kundi la kwanza la sheria ni zile zinazoangukia kwenye Madai, tayari tumeangalia aina za sheria 4 za madai. Leo tunamaliza sheria ya 5 kwenye kundi la sheria za madai. Leo tunakuletea utambulisho wa Sheria ya Madhara. Karibu tujifunze.

 Msingi wa Uwepo wa Sheria ya Madhara

Kama tulivyokuwa tunaangalia katika misingi ya sheria nyingine ambazo tumejadili, ni kwamba sheria yoyote msingi wake ni mahusiano. Katika jamii sheria ipo kuongoza maisha ya wanajamii kwa matendo yao ili kuepuka madhara yanayoweza kuwapata watu wengine. Sheria za madhara zipo kulinda na kuhakikisha madhara yanapojitokeza basi mwathiriwa anapata fidia inayostahili. Msingi wa sheria za madhara ni haki na wajibu ambao wanajamii wamepewa na sheria kwamba wajibu wako ni haki ya mwengine, ukishindwa kutimiza wajibu wako unaweza kujikuta umevunja haki ya mwengine. Sheria ya madhara ipo kuhakikisha kila mtu anatimiza wajibu wake kulinda haki za wengine.

Maana ya Madhara

Kwa tafsiri ya kawida mtu anaweza kusema madhara ni matokeo hasi ya kitendo fulani ambacho kimefanywa na mtu dhidi ya mtu mwengine.

Madhara ni matokeo ya kosa ambalo limefanywa na mtu ambaye ameshindwa kutekeleza wajibu wake, na kosa hilo likasababisha mtu mwengine kuathiriwa kwa kupata maumivu kimwili, kisaikolojia au kibiashara n.k (kuvunjiwa haki yake).

Tofauti kati ya Sheria ya Madhara na Sheria ya Jinai

Sheria ya madhara ina utofauti na sheria za jinai kwa maana kitendo kinaweza kuwa cha kijinai ambapo Serikali itachukua hatua ya kumshitaki mkosaji na mahakama ikatoa adhabu ya faini au kifungo wakati kosa hilo hilo linaweza kuwa la madai kutokana na madhara aliyopata mwathiriwa naye akafungua shauri la madai dhidi ya mkosaji na kupata fidia.

  • Jinai ni uvunjifu wa haki na wajibu wa kijamii ambazo zinaathiri jamii nzima wakati madhara ni uvunjifu wa haki za mtu binafsi
  • Katika jinai mkosaji anaadhibiwa na Jamhuri kwa maslahi ya jamii wakati kwa madhara mkosaji anaadhibiwa kwa kumfidia mwathiriwa.
  • Katika jinai mwenendo wa mashitaka unaongozwa na wanasheria wa Serikali na mkosaji anaadhibiwa kwa faini ambayo inalipwa kwa Serikali au kifungo au vyote kwa pamoja wakati kwenye madhara mwathiriwa ndiye anafungua shauri la madai ili kupata fidia.

Mfano

Kwenye ajali ya gari dereva aliyesababisha ajali anaweza kushtakiwa kwa makosa ya uzembe na kusababisha ajali akadaiwa faini au kifungo ambapo Serikali italipwa faini hiyo. Baada ya hapo waathiriwa wa ajali husika wanaweza kumshitaki dereva na kampuni ya Bima ili kupata fidia kutokana na madhara yaliyosababishwa na ajali husika.

Vipengele vya kosa la Madhara

Ili kosa lenye kuleta madhara lionekane kuwa limetendwa ni lazima vitu 3 muhimu vionekane;

  • Lazima kuwe na kitendo kilichofanywa na mkosaji ambacho ni kinyume na sheria
  • Lazima kuwe na madhara yanayotambuliwa na sheria yametokea kwa mwathiriwa
  • Kitendo kilichofanywa na mkosaji kiwe na asili ya kupelekea madai ya kisheria ili kupata fidia.

Mifano ya makosa ya Madhara

Yapo makosa mengi ya madhara, na makosa mengine yanaweza kuwa ya jinai na ya madhara pia. Hapa tutataja baadhi ya makosa yanayoweza kusababisha madhara na mwathiriwa kuwa na haki ya kuchukua hatua za kisheria kudai fidia, achilia mbali mchakato wa kijinai unaopaswa kuendeshwa na Jamhuri.

  • Makosa yatokanayo na uzembe: mkosaji anaweza kufanya jambo linalopelekea madhara kwa mtu mwengine kwa uzembe. Mfano madereva wa vyombo vya moto.
  • Makosa ya kumshambulia mtu. Mkosaji anaweza kumpiga mtu na kumuumiza, kosa hili ni la jinai pia la madai kwa maana ya mwathiriwa anaweza kudai fidia kutokana na maumivu aliyopata.
  • Makosa ya Kukashifu mtu. Mkosaji anaweza kumkashifu mtu kwa kutoa taarifa dhidi ya mwathiriwa ambazo si za kweli. Mwathiriwa anaweza kufunga shauri la madai kutokana na madhara aliyopata.

 

Hitimisho

Sheria za madhara zipo nyingi sana katika mazingira ya jamii yetu. Watu wengi wanatendewa isivyo halali na vyombo au watu mbali mbali wanaishia kulalamika tu au kuacha kuchukua hatua stahiki. Ikiwa kuna jambo unaona umetendewa linavunja haki yako, tafuta ushauri kwa wataalamu wa sheria ili wakuongoze kujua hatua unazostahili kuchukua.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

Wako

Isaack Zake, Wakili