Haki za Mtoto

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa makala hizi ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Katika makala ya Sheria Leo.31. Ijue Sheria ya Mtoto tulizungumza kwa kifupi juu ya sheria ya Watoto iliyotungwa 2009. Leo tunakwenda kuangalia Haki za Watoto ambazo wananchi tunapaswa kuzizingatia na kuhakikisha zinalindwa.

Msingi wa Haki za Mtoto

Kama tulivyoeleza katika makala ya Ijue Sheria ya Mtoto, kwamba kundi hili ni moja wapo ya makundi ya kijamii ambayo yamekosa kipaombele. Watoto wamekuwa wakinyanyaswa kwa kila namna. Unyanyasaji huu unaanzia ngazi ya familia kwa maana ya wazazi, ndugu wa karibu na hata jamii kwa ujumla. Kundi hili limepata madhila makubwa sana katika kutendewa vitendo vya ukatili kama kipigwa pasipo sababu, kuingiliwa na watu wakubwa, kunyanyaswa utu wao.

Sheria ya Mtoto imekuja kwa lengo ya kuanisha haki za mtoto na kuhakikisha zinalindwa na makundi yote hasa wazazi na jamii kwa ujumla. Haki hizi hazimaanishi kuwa mtoto asifunzwe wala kuadhibiwa kwa makosa lakini kila kitu kifanyike kwa kiasi ambacho anaweza kustahimili.

Mtoto ni mtu yeyote aliye na umri wa chini ya miaka 18. Hili ni kundi kubwa sana katika jamii yetu ya Tanzania, hivyobasi tunapaswa kufahamu namna ya kulihudumia ipasavyo ikiwepo ulinzi wa haki zao.

Haki za Mtoto

Sheria ya Mtoto inaaninisha haki kadhaa za mtoto ambazo Serikali, jamii na wazazi wanapaswa kuzizingatia na kuhakikisha mtoto analindwa kwa haki zake. Katika makala hii tutakwenda kuzichambua.

  1. Haki ya kutokubaguliwa

Hii ni haki ya msingi sana kwa mtoto kama kwa raia mwengine. Mtoto ana haki ya kujumuika na watoto wengine pasipo kujali rangi yake, hali yake ya kiafya au kiakili. Katika jamii yetu hivi karibuni imekumbwa na wimbi kubwa la ubaguzi wa watoto ambao unafanywa na wazazi. Tumeshuhudia watoto wakifungiwa ndani kutokana na hali zao za ulemavu wa aina mbali mbali. Wazazi na ndugu wa karibu tunao wajibu wa kuhakikisha haki za watoto zinalindwa kila mahali.

 

  1. Haki ya kuwa na jina na uraia

Haki ya jina na uraia ni haki muhimu sana kwa mtoto. Haki hii inaenda mbali kwa mtoto kupata kujua ni nani wazazi wake halisi waliomzaa na ndugu zake wa karibu. Kumekuwa na hali ya jamii kwa wazazi kutowaambia watoto juu ya mzazi mwenzake. Mfano mtoto anaweza kulelewa na mama lakini mama hampatii mtoto taarifa zozote kuhusu baba yake. Mtoto ana haki hiyo na ikibidi hata vipimo vya nasaba vifanyike kutambua wazazi wake halisi.

Haki hii inamtaka mzazi au mlezi wa mtoto kuhakikisha mara mtoto anapozaliwa kuandikishwa kwa Msajili wa Vizazi na Vifo  yaani wakala wa usajili (RITA) ambaye ofisi zake zipo katika kila wilaya nchini Tanzania. Hii itampa mtoto hadhi na utambulisho wake kama raia wa Tanzania ili aweze kupata stahiki zake zote na kusaidia mipango endelevu kwa Serikali kujua idadi ya watoto.

 

  1. Haki ya kutunzwa na kukua akiwa na wazazi wake au walezi wake

Hii ni haki muhimu katika ustawi wa maisha ya mtoto. Sheria inabainisha kuwa juu ya mtoto kuwa na haki ya kutunzwa na wazazi au walezi. Kipaombele anachopewa mtoto ni kuwa na wazazi wake. Changamoto kubwa inatokea pale mtoto anapozaliwa na wazazi wake hawajakubaliana kukaa pamoja kumlea mtoto ndipo mvutano mkubwa unaingia baina ya pande mbili na kuhusisha hata ndugu. Katika mvutano huu wengi wao hawazingatii maslahi ya mtoto husika. Mahakama itakuwa na uamuzi wa mwisho kuzingatia upande upi unapaswa kukaa na mtoto endapo mvutano utatokea. Jambo muhimu kwa wazazi kuzingatia hasa maslahi ya mtoto.

 

  1. Haki ya kutumia na kufurahia mali ya mzazi

Mtoto ana haki ya kutumia mali ya mzazi wake. Kama tulivyoeleza kwenye haki ya kutokubaguliwa. Vivyo hivyo mtoto anayo haki ya kufurahia na kutumia mali za mzazi mfano kupata malazi kwenye nyumba, kutumia vifaa mbali mbali kwenye nyumba vinavyoruhusiwa kwa umri wake.

  1. Haki ya maoni

Sheria hii inatumbua uwezo wa mtoto kuwa na maoni. Watu wengi hasa wazazi au walezi wanafanya maamuzi juu ya hatma ya watoto pasipo kuwashirikisha hii sio sahihi. Jamii inawachukulia watoto kama ‘mali’ yao wakati watoto ni watu wenye utashi wao na uwezo wa kutoa maoni yao. Ni muhimu kuwahusisha kwenye maamuzi hasa yanayohusu ustawi wao, kukosa kwao nguvu za kiuchumi hakumaanishi wanakosa mawazo mazuri ya kuchangia katika ustawi wa familia.

  1. Haki ya kulindwa kutokana na kazi hatarishi

Sheria inawataka wazazi na walezi na jamii kwa ujumla kuhakikisha mtoto analindwa kutokana na kazi hatarishi katika maisha yake, ustawi wa kielimu na kiafya. Tunashuhudia jamii yetu ikiwaingiza watoto wadogo hasa chini ya miaka 10 kweye kazi hatarishi za kupita barabarani kuomba omba, kufanya kazi kwenye migodi mbali mbali na kazi nyingine ambazo zisingewezwa kufanywa kwa umri wao. Wapo watu wanaajiri watoto wadogo kwa sababu mahitaji yao ya kifedha si makubwa kama mtu mzima. Haya ni makosa makubwa, ni muhimu kwetu sote yaani wazazi, walezi na jamii kuwalinda watoto na hasa tukiona wanajihusisha au kuhusishwa kwenye kazi hatarishi kukemea tabia hiyo na kuchukua hatua.

  1. Haki ya kulindwa kutokana na mateso au adhabu zilizopitiliza.

Watoto wanatakiwa kulindwa kutokana na adhabu kali zilizopitiliza uwezo wao hasa za kuwazalilisha wao mbele ya jamii. Walezi na wazazi katika nyakati hizi wamekuwa wepesi wa kutoa adhabu kali zinazopitiliza juu ya watoto. Tunashuhudia matukio ya watoto kufungiwa ndani au kwenye eneo hata kupoteza maisha, kuunguzwa moto, kupigwa hata kuzirai au kupoteza maisha. Haya matukio yameshamiri sana nyakati hizi. Ni vyema adhabu zinazotolewa ziwe kwa makosa yaliyodhibitishwa na iwe ya kiasi ya kumfanya mtoto alewe. Nyakati nyingine mzazi au mlezi unapaswa kumhoji mtoto juu ya makosa na kumpa ushauri unaostahili. Kupiga au kutoa adhabu kubwa kunaweza kusiwe suluhu ya mtoto husika kama tabia zimekithiri tafuta washauri wa masuala ya watoto wanaweza kukusaidi njia mbadala ya kushughulika na tabia zake.

 

  1. Wajibu wa kutunzwa na wazazi au walezi

Sheria inahakikisha juu ya wazazi au walezi kuwatunza watoto katika ustawi wa maisha yao. Kazi ya wazazi au walezi ni kuhakikisha watoto au mtoto anapata chakula, malazi, mavazi, huduma za afya ikiwemo chanjo, elimu, uhuru na haki ya kucheza. Kwa namna yoyote ile mzazi au mlezi hawezi kutumia sababu ya kumwadhibu mtoto kwa kumnyima mambo yaliyoanishwa katika wajibu wao.

Ukiukwaji  wa Haki zilizoanishwa katika Sheria ya Mtoto unaweza kupelekea adhabu ya faini isiyozidi Tsh.5,000,000/- au kifungo kisichozidi miezi 6 au vyote kwa pamoja. Hata hivyo yapo makosa mengine ambayo wanatendewa watoto kama kuumizwa mwili, au ubakaji n.k makosa haya yatakapodhibitika adhabu itatolewa kutokana na sheria husika ampapo mwenye hatia anaweza kupata kifungo kuanzia miaka 30 hadi kifungo cha maisha kutokana na kosa.

Hitimisho

Ndugu msomaji nisisitize mwishoni mwa makala hii kuwa watoto ni kundi muhimu sana katika ustawi wa Taifa letu na kujenga haiba ya watu wanaojiamini, wenye maadili, nidhamu na elimu katika maeneo mbali mbali. Sisi sote tulikuwa watoto siku moja tumelelewa ni zamu yetu kuwalea katika njia njema na kuhakikisha wanapata haki zao.

Mlee mtoto vizuri leo atakulea na wewe katika uzee wako, mpe haki zake leo atakupatia haki zako kesho katika uzee wako’.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

Wako

Isaack Zake, Wakili