11.B. Haki za Chama cha Wafanyakazi
Utangulizi
Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiishambua Sheria ya Kazi, tumeendelea kuwa pamoja kwa kipindi chote hiki. Makala iliyopita ilitupa utangulizi juu ya Uhuru wa Kujumuika katika Vyama vya Wafanyakazi, Jumuiya za Waajiri na Mashirikisho. Tuliweza kuchambua juu ya utaratibu wa kuunda chama cha wafanyakazi, utaratibu wa usajili na wajibu wa chama. Katika makala ya leo tunakwenda kuona Haki za Chama cha Wafanyakazi. Karibu tujifunze.
Haki za Chama cha Wafanyakazi
Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini inabainisha juu ya uwepo wa haki za chama cha wafanyakazi. Haki hizi zipo kisheria na zinasimamiwa na sheria husika. Waajiri au mashirikisho ya waajiri wanapaswa kuzitambua haki hizi na kuziheshimu kwani ukiukwaji wake unaweza kupelekea mgogoro mahala pa kazi.
Ufuatao ni ufafanuzi juu ya haki za msingi za Chama cha wafanyakazi.
1. Haki ya kuingia eneo la Mwajiri
Sheria za Kazi zinatambua haki ya chama kuweza kupata ruhusa ya kuingia eneo la mwajiri kwa nia ya kuendesha shughuli zake. Mwakilishi wa chama cha wafanyakazi kilichosajiliwa anayo haki ya kuingia eneo la mwajiri kwa nia ya kufanya yafuatayo;
• Kusajili wanachama
• Kuwasiliana na wanachama
• Kukutana na wanachama katika kushughulika na mwajiri
• Kufanya mikutano ya wafanyakazi kwenye eneo la mwajiri
• Kusimamia upigaji kura chini ya Katiba ya chama.
Katika haki ya kuingia eneo la mwajiri chama kinapewa pia haki ya kuanzisha tawi la chama endapo kina usajili wa wanachama kuanzia 10 mahali pa kazi. Kadhalika mwajiri atawajibika kukipatia chama vifaa muhimu vya kufanikisha shughuli zake mahala pa kazi.
Hata hivyo haki hii itategemea masharti yoyote ya muda na mahali ambapo yanafaa na muhimu kulinda maisha au mali au kuzuia ukatizaji wa kazi usiohitajika.
2. Haki ya Makato ya Ada
Chama cha wafanyakazi kina haki ya kupatiwa ada ya wanachama wake na mwajiri baada ya kuidhinishwa makato hayo na mfanyakazi. Mwajiri ana wajibu wa kukata makato ya ada ya wanachama kwa wafanyakazi na kuwasilisha kwa chama ndani ya siku 7 baada ya mshahara. Endapo mwajiri atashindwa kuwasilisha makato ndani ya muda husika atapaswa kulipa faini ya kiasi cha asilimia 5 kwa kila siku aliyochelewesha.
Aidha mfanyakazi ana uwezo wa kutengua idhini yake ya kukatwa ada kwa kutoa taarifa ya maandishi katika kipindi cha mwezi mmoja kwa mwajiri na chama. Sheria inamtaka mwajiri anapowasilisha makato ya ada kuambatanisha na orodha ya wanachama waliokatwa ada na nakala ya waliotengua idhini kama wapo.
3. Haki ya Chama kuwa na Wawakilishi mahali pa kazi
Chama kina haki ya kuwa na wawakilishi wake katika eneo la kazi, ambapo upatikanaji wao utaongozwa na Katiba ya chama. Uwakilishi wa chama mahali pa kazi utategemea idadi ya wanachama katika eneo hilo. Mfano
• Ikiwa mwanachama 1 – 9 basi kutakuwa na mwakilishi 1 wa chama
• Ikiwa ni wanachama 10 -20 basi watakuwa wawakilishi 3 wa chama
• Ikiwa ni wanachama 21-100 basi watakuwa wawakilishi 10 wa chama
• Ikiwa ni wanachama 101 na kuzidi basi watakuwa wawakilishi 15 wa chama
Sheria inafafanua juu ya ushiriki wa wawakilishi wanawake katika maeneo ya kazi iwapo kutakuwa na wanachama zaidi ya 100 basi ni lazima wawakilishi wanawake wasipungue 5 kama eneo la kazi linawahusu wanawake pia.
Majukumu ya Wawakilishi wa Chama
• Kuwakilisha wanachama kwenye vikao vya kushughulikia malalamiko na nidhamu
• Kufanya uwakilishi kwa niaba ya wanachama kuhusiana na kanuni, afya na usalama na ustawi
• Kushauri kuhusu tija katika kazi
• Kuwakilisha chama cha wafanyakazi katika upelelezi na uchunguzi unaofanywa na wakaguzi kulingana na sheria za kazi
• Kufuatilia mwajiri kama anafuata sheria za kazi
• Kufanya shughuli za chama cha wafanyakazi chini ya katiba ya chama
• Kuendeleza mahusiano mema
• Kufanya kazi au shughuli yoyote inayokubaliwa na mwajiri.
Katika kutekeleza majukumu yao wawakilishi wa chama watastahili malipo yao ya mishahara kama kawaida hata kama kutekeleza majukumu hayo kutawafanya wasiwepo kazini. Pia mwajiri anawajibika kutoa taarifa zozote zitakazoweza kusaidia utendaji wa wawakilishi wa wafanyakazi.
Hata hivyo haki hii itategemea masharti yoyote yanayofaa kuhakikisha matumizi sahihi ya haki hii bila kuvuruga utaratibu wa kazi.
4. Haki ya Likizo kwa Viongozi wa Chama
Sheria inawapa wawakilishi wa chama mahali pa kazi wanayo haki ya kupewa likizo ya malipo na mwajiri kwa ajili ya kuudhuria mafunzo kuendana na majukumu yao. Aidha sheria inawapa viongozi wa chama cha wafanyakazi na viongozi wa shirikisho kupewa likizo ya malipo kwa ajili ya kuudhuria mafunzo yanayohusiana na majukumu ya chama au shirikisho.
Utaratibu wa Kupata Haki za Chama
Haki za chama katika mahali pa kazi zimewekewa utaratibu wa kisheria ili ziweze kupatikana. Sheria inakitaka chama cha wafanyakazi kilichosajiliwa kinachotaka kutekeleza haki za chama kufanya yafuatayo;
• Chama kinatakiwa kutoa taarifa kwa mwajiri kupitia fomu maalum kikiainisha haki kinataka kuzitekeleza mahali pa kazi
• Mwajiri baada ya kupokea fomu anapaswa kukutana na chama ndani ya siku 30 ili kufikia makubaliano na utaratibu wa kutekeleza haki hizo
• Endapo hakutakuwa na makubaliano, chama kinaweza kuwasilisha mgogoro huo Tume ya USuluhishi na Uamuzi
• Endapo usuluhishi utashindikana chama kinaweza kupeleka mgogoro huo Mahakama ya Kazi.
Utaratibu wa usitishaji wa Haki za Chama
Haki za chama zinaweza kusitishwa endapo chama kitakiuka makubaliano ya msingi ya utoaji wa haki au amri ya mahakama inayotoa haki hizo.
Ikitokea hali hiyo ya ukiukwaji wa makubaliano, mwajiri anaweza kupeleka mgogoro huu mbele ya Tume kwa ajili ya usuluhishi. Usuluhishi ukishindikana, mwajiri anaweza kupeleka mgogoro huo Mahakama ya Kazi akiomba mahakama isitishe makubaliano ya kutoa haki hizo au kuondoa amri yake ya kutoa haki hizo.
Hitimisho
Haki za chama mahali pa kazi ni muhumu sana katika kuwezesha kutimiza majukumu yake ipasavyo. Dhumuni la sheria kuhakikisha upatikanaji wa haki hizi ni kuboresha mahusiano baina ya wafanyakazi na waajiri na hasa kuhakikisha maslahi ya wafanyakazi yanazingatiwa wakati wote wa ufanyaji kazi. Hata hivyo ni muhimu kwa vyama vya wafanyakazi kuzingatia utaratibu wa kupatikana haki hizi ili tija, ufanisi na manufaa vionekane mahala pa kazi na isiwe sababu ya migororo isiyoisha.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com
Wako
Isaack Zake, Wakili