Haki ya Kuishi na Adhabu ya Kifo

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa www.ulizasheria.co.tz . Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunakwenda kujifunza zaidi juu ya Haki ya Kuishi na Adhabu ya Kifo. Kama ni mfuatiliaji wa makala hizi niliwahi kuandika juu ya Maisha ni Haki yako. Leo tunaingia ndani kidogo kuona Haki ya Kuishi na Adhabu ya Kifo. Karibu tujifunze.

Maana ya Haki ya Kuishi

Katiba ya JMT inaeleza wazi wazi kuwa kila mwananchi anayo haki ya kuishi. Ibara ya 14 ya Katiba ya JMT inasema

kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha yake kwa jamii kwa mujibu wa sheria’.

Maisha ni zawadi ambayo kila mwanadamu amepewa na Mungu, hivyo mifumo ya tawala za duniani kwa mujibu wa Katiba na sheria inawajibika kulinda na kutunza maisha ya kila mmoja wetu.

Hatahivyo katika utekelezaji wa haki hii ya kuishi, baadhi ya mifumo ya Katiba duniani inaeleza kuwa yapo mazingira ambayo haki hii inaondolewa na Serikali endapo kuna makosa ambayo mtu atakuwa amefanya. Makosa hayo endapo yatadhibitika mbele ya Mahakama basi inaweza kutolewa adhabu ya kifo ambayo inaondoa ile haki ya kuishi.

Maana ya Adhabu ya Kifo

Hii ni mojawapo ya adhabu katika makosa ya kijinai ambayo inatekelezwa kwa mtu au watu waliotiwa hatiani na Mahakama yenye mamlaka kwa makosa ambayo yanahushisha adhabu hiyo.

Katika nchi ya Tanzania adhabu ya kifo bado inatumika endapo makosa ambayo yameainishwa katika sheria yatatendwa na mtu au watu. Makosa ambayo yanaambatana na adhabu ya kifo;

  • Kuua kwa kukusudia
  • Uhaini

Pamekuwa na mjadala kuhusiana na matumizi ya adhabu ya kifo dhidi ya haki ya kuishi. Wapo wanaounga mkono matumizi ya adhabu hii na wapo wanaopinga kwa msingi kwamba mwanadamu au Serikali haipasi kutoa uhai ambao hauwezi kuumba. Kwa upande mwengine wapo wanaosema kuwa adhabu hii itekelezwa kwa kuwa wanaotiwa hatiani nao kwa njia moja au nyingine wamesababisha kifo cha mtu au watu wengine hivyo wanastahili kifo pia.

Mjadala huu umeendelezwa mahali pengi ulimwenguni tumeona yapo makosa katika nchi nyingine kama uhujumu uchumi au biashara ya madawa ya kulevya yameingizwa katika adhabu ya kifo endapo mtu au watu wahusika watatiwa hatiani.

Tumeona katika nchi yetu, watu ambao wametiwa hatiani kwa makosa ambayo yanahitaji utekelezaji wa adhabu ya kifo wakikaa muda mrefu gerezani kwa kusubiri idhinisho la Rais aliyepo madarakani kwa kipindi hicho.

Hitimisho

Nadhani sasa ni wakati wa kulitazama jambo hili la haki ya kuishi dhidi ya adhabu ya kifo katika mazingira yetu ya Tanzania. Ni muhimu kama jamii kuwa na mjadala mpana wa namna ya kuona jinsi ya kusitisha au kutekeleza adhabu hii. Ni maoni yangu kuwa adhabu hii ya kifo iondolewe kwani haijaleta matunda katika kupunguza makosa yanayofanyika kila siku.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili