Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya Hali ya Hatari. Leo tunaangalia juu ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kama ilivyo kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Karibu tujifunze.

Maana ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora

Katika kusimamia shughuli za kuhakikisha haki za binadamu zinazingatiwa na utawala bora yaani utawala wa sheria, Katiba ya JMT imeunda chombo maalum yaani Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora. Ibara ya 129(1) ya Katiba inasema;

‘Kutakuwa na Tume itakayoitwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, ambayo majukumu yake yatakuwa kama ilivyoelezwa katika ibara ya 130 ya Katiba hii’

Tume hii ni chombo maalum cha kikatiba chenye mamlaka ya kufuatilia utendaji mpana wa haki za kibinadamu katika taifa letu.

Muundo wa Tume

Tume itaundwa na makamishna ambao wataongozwa na Mwenyekiti ambaye ni mtu mwenye sifa ya kuweza kuteuliwa kuwa Jaji na makamu mwenyekiti. Uteuzi wa mwenyekiti na makamu utahusisha pande zote za muungano, yaani iwapo mwenyekiti anatoka upande mmoja wa muungano basi makamu mwenyekiti atatoka upande mwengine.

Pia Tume itakuwa na makamishna wengine wasiozidi 5 ambao wana uzoefu mkubwa katika masuala ya haki za binadamu, sheria, utawala, siasa au mambo ya jamii. Makamishna hawa watasaidiwa na makamishna wasaidizi. Hii ni kwa mujibu wa Ibara ya 129(2) (3) ya Katiba.

Majukumu ya Tume

Majukumu ya Tume yameainishwa katika Katiba sawa na Ibara ya 130 (1) kuhusisha;

  • Kuhamasisha nchini hifadhi ya haki za binadamu na wajibu kwa jamii kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi;
  • Kufanya shughuli za kupokea malalamiko ya uvunjaji wa haki za binadamu kwa jumla;
  • Kufanya uchunguzi juu ya mambo yanayohusu uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora;
  • Kufanya utafiti, kutoa na kueneza nchini elimu kwa umma kuhusu haki za binadamu na utawala bora;
  • Kama ikibidi, kufungua mashauri mahakamani ili kuzuia vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu au kurekebisha haki inayotokana na uvunjwaji huo wa haki za binadamu, au ukiukwaji wa misingi ya utawala bora;
  • Kuchunguza mwenendo wa mtu yeyot anayehusika au taasisi yoyote inayohusika na masharti ya ibara hii katika utekelezaji wa kawaida wa madaraka ya kazi au majukumu yake au utekelezaji unaokiuka madaraka hayo;
  • Kutoa ushauri kwa Serikali na vyombo vingine vya umma na vya sekta binafsi kuhusu haki za binadamu na utawala bora
  • Kuchukua hatua zipasazo kwa ajili ya kukuza na kuendeleza usuluhishi na suluhu miungoni mwa watu na taasisi mbalimbali wanaofika au kifikishwa mbele ya Tume

 

Hitimisho

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ni chombo muhumu sana katika katiba kwani ndicho kinahakikisha uzingatiaji wa haki kwa wananchi na watu wote. Majukumu ya Tume yanavyoanishwa katika Katiba yanaonesha wigo mpana wa utendaji wa Tume kuhusisha wananchi, viongozi au taasisi za kibinafsi au za umma kuweza kuhojiwa na kuchunguzwa na Tume. Ni muhimu wananchi kuifahamu Tume hii na namna inavyofanya shughuli zake ili kunufaika na huduma zake. Tuendelee kufuatilia makala nyingine ambazo zitaendelea kufafanua juu ya Tume hii.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili