Utaratibu wa Umiliki wa Ardhi kwa njia ya Zawadi

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika makala iliyopita tuliangalia juu ya njia Familia au Ukoo. Leo tunaendelea na mfululizo wa uchambuzi wa njia ya umiliki kwa Zawadi. Karibu tujifunze.

Umiliki wa Ardhi kwa njia ya Zawadi

Zawadi ni kitu anachopata au anachopewa mtu pasipo kulipa au kutoa gharama yoyote. Katika mfumo wa maisha yapo mazingira watu au ndugu wanapeana zawadi. Msingi wa zawadi kwa kila mmoja unatofautiana.

Vivyo hivyo ardhi kwa kuwa inamilikiwa na mtu au familia inaweza kutolewa sehemu au yote kama zawadi kwa mtu mwengine au kikundi maalum kwa malengo fulani.

Ardhi yoyote alimradi anayeitoa anayo mamlaka basi inaweza kutolewa kama zawadi iwe ardhi ya kimila ua ile iliyosajiliwa kwa hati maalum za serikali.

Utaratibu wa umiliki ardhi kwa njia ya Zawadi

Katika ugawaji wa ardhi kama zawadi upo utaratibu ambao unapaswa kuzingatiwa ili uhalali wa zawadi hiyo ya ardhi ubainike. Ardhi haitolewi tu kiholela bali kuna misingi ya utoaji na taratibu za kuzingati.

Ufuatao ni utaratibu wa kutoa ardhi kama zawadi;-

  1. Umiliki halali wa Mtoa zawadi

Hili ni jambo la msingi na muhimu zaidi kwa kuwepo na umiliki ardhi kabla haijatolewa kama zawadi na mmiliki. Uhalali wa ardhi kutolewa kama zawadi unatokana na mtoa zawadi kuwa mmiliki. Watu wengi wanatoa zawadi ya ardhi huku hawana umiliki wa moja kwa moja na kusababisha matatizo ya baadae kwa aliyepokea ardhi husika. Inawezekana ardhi inamilikiwa pamoja kati ya baba na mama alafu mmoja wapo anaitoa kwa mtoto mmoja pasipo kushauriana na mwenzi wake, hali hii husababisha mgogoro baina ya wenye ardhi na yule anayeipokea.

  1. Sababu za utoaji wa zawadi ya ardhi

Pamoja kwamba jambo hili si lazima sana kuelezwa au kufafanuliwa na mtoa zawadi mara kwa mara, kunakuwepo na sababu ambazo zimepelekea zawadi ya ardhi husika kutolewa. Katika mila za kiafrika wengi hupokea zawadi ya ardhi baada ya kuanzisha familia yaani kuoa au kuolewa ndipo tunaona wazazi wakitoa eneo/ardhi kama sehemu ya kuanzisha familia yao. Zipo sababu nyingine nyingi mfano kuhitimu elimu fulani au kufanikisha kwa jambo fulani kunaweza kuwa sababu ya zawadi husika kutolewa.

Pia ardhi inaweza kutolewa kama zawadi kwa taasisi ya kidini au yenye kufanya shughuli za kijamii mfano makanisa au misikiti au taasisi za kusadia wasiojiweza na wenye changamoto za kimaisha n.k.

  1. Uhusiano wa Mtoaji na Mpokea zawadi

Katika utoaji wa zawadi ya ardhi ni muhimu sana kuhakikiwa uhusiano baina ya mtoa zawadi na mpokeaji wa zawadi. Ni lazima uwepo uhusiano au wa kinasaba au kindoa au ukaribu wowote ambao utahalalisha utoaji wa ardhi kama zawadi. Kwa mfano mke anaweza kumpa ardhi mume au mtoto na kadhalika mume anaweza kufanya hivyo. Pia babu anaweza kumpa ardhi mjukuu au mjomba kumpa ardhi mtoto wa dada yake. Uhusiano wa karibu ni muhimu kuhakikiwa kwani watu wengi wamekuwa wakitumia jambo hili kama nafasi ya kutaka kukwepa kodi ya serikali wakati wa kubadilisha umiliki wa ardhi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwengine.

  1. Uandishi wa nyaraka ya utoaji wa zawadi

Ni muhimu sana pale ardhi inapotolewa kama zawadi pawepo na maandishi. Hii itasaidia pande zote mbili yaani mtoaji na mpokeaji wa zawadi husika. Uwepo wa maandishi unaweza kuepusha mgongano baina ya ndugu au watu wenye nasaba moja kugombana kwa sababu ya ardhi iliyotolewa zawadi. Nyaraka hii inaitwa kisheria ‘hati ya zawadi’ au kwa lugha ya kiingereza ‘Deed of Gift’.

  1. Usajili wa ardhi kwa majina ya aliyepewa zawadi

Hatua muhimu katika kuhitimisha mchakato wa utoaji wa ardhi kama zawadi ni kuisajili katika mamlaka husika ili kuonesha uhamishaji wa umiliki kutoka kwa mmiliki aliyetoa zawadi kwenda kwa mmiliki mpya anayepokea zawadi. Hii inasadia sana hasa kwa yule ambaye amepewa zawadi kuweza kutumia ardhi hiyo kwa uhuru katika kuiendeleza pasipo kuingiliwa na mtu na kutambuliwa na mamlaka husika. Endapo ardhi hii imesajiliwa katika hati ya umiliki basi aliyepokea anapata hati ya umiliki wa eneo.

Hitimisho

Sheria za ardhi zinatambua suala zima la umiliki au uhamishaji wa umiliki wa ardhi kwa njia ya zawadi. Ni muhimu hasa kwa mtoaji na mpokeaji wa zawadi kuhakikisha utaratibu husika unafuatwa na kuzingatiwa kuepusha mgogoro baina ya ndugu au wahusika wengine katika eneo. Endapo eneo linalokusudiwa kutolewa kama zawadi.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040.

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili