Utaratibu wa Umiliki wa Ardhi kwa njia ya Uvamizi

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika makala iliyopita tuliangalia juu ya njia ya Kusafisha eneo. Leo tunaendelea na mfululizo wa uchambuzi wa njia ya Kuvamia. Karibu tujifunze.

Umiliki wa Ardhi kwa njia ya Uvamizi

Kama tulivyowahi kuzungumza katika makala zilizopita kuwa uvamizi wa maeneo ni kinyume cha sheria na ikibainika mvamizi anaweza kuchukuliwa hatua za kijinai pamoja za kimadai. Hatahivyo, sheria ya ardhi inatambua aina ya umiliki kwa njia ya uvamizi ambapo mvamizi anaweza kutambulika kama mmiliki akikidhi baadhi ya vigezo ambavyo vimewekwa kisheria.

Leo tunakwenda kuangalia namna mvamizi anaweza kubadilika kuwa mmiliki halali katika eneo na mbinu ambazo zitamsaidia mmiliki halali kuhakikisha kuwa eneo lake halivamiwi na kusababisha umiliki wake kuhamishwa kwenda kwa mvamizi.

Tafsiri sahihi ya umiliki kwa njia ya uvamizi ni hali inayojitokeza kwa mvamizi wa eneo kuingia katika eneo na kufanya shughuli zake ikiwa za makazi au uzalishaji katika eneo pasipo ruhusa ya mmiliki halali na kuwepo hapo kwa kipindi kisichopungua miaka 12 pasipo kuingiliwa na mmiliki au wakala wake.

Kwa maneno mengine neno la umiliki kwa njia ya uvamizi linajulikana kama ‘adverse possession’ kwa lugha ya kiingereza.

Utaratibu wa umiliki ardhi kwa njia ya Uvamizi

Katika utaratibu wa umiliki kwa njia ya uvamizi wa eneo yapo mazingira ambayo yanaweza kumsaidia mtu kuhalalisha umiliki wa maeneo husika.

Ufuatao ni utaratibu wa kupata ardhi kwa uvamizi eneo;-

  1. Uwepo wa ardhi ambayo si milki ya mvamizi

Ili umiliki kwa njia ya uvamizi uweze kupata uhalali jambo la msingi ni uwepo wa eneo ambalo halimilikiwi na mvamizi yaani ni milki ya mtu mwengine ambaye hawana uhusiano na mvamizi. Ardhi hii ni lazima iwe inamilikiwa tofauti na ile ambayo tulijadili katika makala iliyopita yaani ardhi ambayo ni pori halipo chini ya umiliki wa mtu au kikundi cha watu. Yapo maeneo kadhaa vijijini au katika miji yana umiliki wa watu lakini kwa taswira ni kama yametelekezwa. Katika mazingira haya mvamizi anaweza kuingia kwenye eneo husika.

  1. Mvamizi kuchukua udhibiti wa eneo

Hatua hii ya pili ni muhimu kwa ajili ya kujenga mazingira ya umiliki kwa njia ya uvamizi yaani mvamizi husika ambaye eneo hili si lake kuchukua hatamu za eneo kwa kuanzisha shughuli za uzalishaji ikiwa ni kilimo au shughuli nyingine au kuweka makazi katika eneo husika. Mvamizi hawezi kupata uhalali mbele ya sheria endapo hajachukua hatua za kudhibiti eneo husika ambalo anataka ahesabiwe ni halali yake.

  1. Mvamizi hapaswi kupata ruhusa au kibali kutoka kwa mmiliki au wakala wake.

Mtu anayetaka kupata umiliki kwa njia ya uvamizi ni lazima asiwe na kibali au ruhusa kutoka kwa mmiliki au wakala wake. Watu wengi wanataka kuhesabiwa ni wamiliki kwa njia hii ya uvamizi lakini unakuta hapo awali walikabidhiwa eneo kama walinzi au kuruhusiwa kufanya shughuli za uzalishaji au kuweka makazi na mmiliki au wakala wake. Sheria inatambua kuwa kitendo cha uvamizi hakihusiani na kupewa ruhusa au kibali na mmiliki.

  1. Kuwepo katika eneo kwa muda usiopungua miaka 12

Mvamizi ni lazima aweze kudhibitisha kuwa yupo katika eneo husika la uvamizi kwa kipindi kisichopungua miaka 12 pasipo kuingiliwa au kuibuliwa mgogoro wa ardhi katika eneo hilo na mmiliki au mwakilishi wake. Mvamizi anapaswa adhibitishe uwepo wake katika eneo husika mfululizo katika kipindi kisichopungua miaka 12. Hii inatoa nafasi hata kwa jamii inayozunguka eneo husika kujua kuwa mvamizi husika ni mmiliki halali wa eneo hilo.

Ufafanuzi

Msingi wa sheria kuruhusu umiliki kupitia njia hii ya uvamizi wa muda mrefu ni kuondoa ile dhana ya watu kumiliki maeneo mengi pasipo kufanya shughuli zozote za maendeleo. Kumekuwa na tabia ya watu kumiliki maeneo mengi kwa lengo la kufanya biashara ya ardhi badala ya kuchukua hatua ya kuyaendeleza. Wengi wanamiliki maeneo na kuyatelekeza pasipo kufanya shughuli za uzalishaji. Kwa kuwa Serikali na jamii kwa ujumla inataka maendeleo ikiwepo na shughuli za uzalishaji uvamizi wa muda mrefu pasipo kuingiliwa na mmiliki au wakala wake unaweza kumpatia mvamizi haki ya umiliki kwani atakuwa na msingi wa kuendeleza eneo.

Hitimisho

Pamoja na kwamba njia hii ya umiliki kwa hali ya kawaida inaonekana kama si halali lakini ni njia muhimu sana kuhakikisha ardhi haikai tupu pasipo kufanyiwa maendeleo ya msingi. Hii itasaidia pia kwa wamiliki kuchukua hatua madhubuti kutimiza masharti ambayo wamepewa ardhi husika ikiwa ni kwa ajili ya ujenzi au kilimo au shughuli za viwanda wanapaswa kutimiza masharti hayo ndani ya muda husika. Ndio maana kwa sasa unasikia zipo hati za umiliki zinafutwa na Rais kutokana na wamiliki kutochukua hatua madhubuti kutekeleza shughuli zile ambazo wamepewa hati husika.

Nitoe rai kwa wamiliki wa maeneo kuhakikisha kila eneo wanalomiliki wanafanya shughuli ambazo zitaweza kuonesha maendeleo katika eneo na si kuyatelekeza kwa nia ya kutaka kuuza baaadae kwani kuna hatari ya kuvamiwa au kufutiwa hati za umiliki na mamlaka husika.

‘Pata ardhi, tumia ardhi kwa shughuli za maendeleo ya nchi’

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili