24. Usitishaji wa Ajira kwa Mgomo usio Halali

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Leo tunaendelea kuangalia juu ya usitishaji wa Ajira kwa kushiriki mgomo usio halali. Karibu tujifunze.

Maana ya Mgomo

Mgomo ni usimamishaji wa kazi unaofanywa na wafanyakazi kwa lengo la kumlazimisha au kumshurutisha mwajiri wao kukubali madai ya wafanyakazi au mwajiri kubadili au kuacha madai yake dhidi ya wafanyakazi.

Katika makala zilizotangulia tulijifunza juu ya mgomo na hatua zinazopaswa kuchukuliwa na wafanyakazi kuhakikisha wanafanya mgomo halali. Soma uchambuzi wa sheria.13. Migomo

Hatahivyo, yapo mazingira yanayoweza kusababisha mgomo ambapo mgomo husika ukakosa vigezo vya kuwa halali na hivyo kumpelelea mwajiri kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wafanyakazi waliojihusisha katika mgomo haramu.

Katika makala hii ya leo tunakwenda kuangalia usitishaji wa ajira unaotokana na mfanyakazi au wafanyakazi kushiriki mgomo usio halali.

Utaratibu nidhamu katika Mgomo usio Halali

Kwa kawaida mfanyakazi au wafanyakazi hawapaswi kuchukuliwa hatua za kinidhamu na mwajiri wao iwapo watashiriki katika mgomo ambao ni halali uliofuata taratibu za kisheria. Hivyo mwajiri hana haki ya kumfukuza mfanyakazi au wafanyakazi walioshiriki mgomo halali.

Hatahivyo, endapo itabainika kuwa mgomo wa wafanyakazi haukuwa halali basi mwajiri anayo haki ya kuchukua hatua za nidhamu dhidi ya wafanyakazi au mfanyakazi na adhabu mojawapo inayoweza kutolewa ni kusitisha ajira ya mfanyakazi husika.

Kabla ya mwajiri hajachukua hatua ya kusitisha ajira ya mfanyakazi au wafanyakazi kutokana na mgomo usio halali anapaswa kuzingatia yafuatayo;-

  • Kuangalia ni kwa kiwango gani mfanyakazi au wafanyakazi wamekiuka sheria na utaratibu wa mgomo
  • Endapo kitendo cha mgomo usio halali ni matokeo ya kitendo cha mwajiri
  • Endapo pande zote wamefanya jitihada zozote za kutatua mgogoro na kufikia mwafaka.
  • Endapo mfanyakazi au wafanyakazi walipewa onyo la mwisho na mwajiri kusitisha mgomo
  • Namna ambayo mfanyakazi au wafanyakazi walionyesha tabia gani wakati wa mgomo ikiwa
  • Endapo zoezi la mgomo usio halali lilihatarisha biashara au huduma za mwajiri na mahali pa kazi au la.

Endapo mwajiri anataka kuchukua hatua za kusitisha ajira kama adhabu kwa mfanyakazi au wafanyakazi walioshiriki mgomo ni lazima kuchukua hatua zifuatazo;

  1. Mapema iwezekanavyo kabla ya kusitisha ajira, mwajiri anapaswa kuwasiliana na viongozi wa chama cha wafanyakazi nia yake ya kutaka kusitisha ajira kwa wafanyakazi watakaoshiriki mgomo usio halali.

 

  1. Kwamba, mwajiri anapaswa kutoa tamko la ilani kuwataka wafanyakazi kufuata masharti ya kuacha mgomo halali na endapo watakiuka ni hatua gani mwajiri anategemea kuzichukua dhidi yao.

 

 

  1. Baada ya kutoa ilani, wafanyakazi wanapaswa kupewa muda wa kuweza kutekeleza masharti husika au kukataa. Kipindi hicho kisipungue walau siku 1.

 

  1. Mwajiri hapaswi kubagua wafanyakazi katika kutoa adhabu endapo wafanyakazi wote walihusika katika mgomo usio halali. Yaani ikiwa wafanyakazi waliogoma isivyo halali wamedhibitika, adhabu inapaswa kuchukuliwa kwa wote na si kuwasitishia ajira na kuajiri wengine ambao waliadhibiwa pamoja.

Hitimisho

Ndugu mdau ni vyema kufahamu kuwa mgomo ni haki ya wafanyakazi. Hatahivyo kuna utaratibu wa kufanya mgomo ili uwe halali na kwa mujibu wa sheria. Endapo mgomo utafanyika kinyume na sheria mojawapo ya athari kwa wafanyakazi ni kusitishiwa ajira yao kwa utovu wa nidhamu. Muhumu kufuata utaratibu katika kufanikisha mgomo mahali pa kazi.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili.