Ijue dhana ya Urithi katika Mirathi.

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunaendelea kujifunza na mfululizo wa makala zinazohusu masuala ya mirathi. Karibu tujifunze kwa pamoja.

Maana ya Urithi

Urithi ni kitu chochote ambacho anapatiwa mtu kutoka kwa yule mtu anayemuhusu ambaye amefariki. Kama tunavyofahamu dhana ya urithi ni dhana kongwe kabisa duniani kwani imekuwepo vizazi hata vizazi.

Sheria zinazozungumzia masuala ya urithi ndizo zinaitwa sheria za Mirathi. Tumeweza kuangalia maana ya mirathi kuwa ni mchakato unahusisha kurithishwa kwa warithi halali wa marehemu mali na madeni yanayomhusu marehemu.

Katika makala ya leo tunakwenda kuangalia hasa kwa undani suala la urithi linalohusianishwa na mchakato mzima wa mirathi. Katika makala hii tunakwenda kujibu swali muhimu ambalo linasema

Qn. Je, ni vitu gani au mambo gani yanaweza kurithishwa katika suala la mirathi?

Majibu ya swali hili yanaweza kutusaidia kujua vitu muhimu vya kuzingatia katika mchakato wa mirathi. Hii itasaidia jamii kufahamu mambo gani yanapaswa kuingizwa kwenye mirathi na mambo gani hayapaswi kuingizwa kwenye mirathi.

  1. Mali zisizohamishika za marehemu

Mchakato wa usimamizi wa mirathi unahusisha juu ya uwepo wa mali za marehemu. Katika makundi ya mali za marehemu zipo zile zisizohamishika hii ni kama ardhi au majengo yanayomilikiwa na marehemu. Mali za marehemu zisizohamishika zinapaswa kuinga katika usimamizi wa mirathi. Marehemu anaweza kuwa anamiliki ardhi au majengo akiwa binafsi au kwa ubia na mtu au taasisi nyingine, hivyo kiwango cha umiliki wake ikiwa ni ubia basi kitahusika katika usimamizi wa mirathi au mgao kulingana na wosia kama marehemu atakuwa ameacha wosia.

  1. Mali zinazohamishika za marehemu

Mali nyingine ambazo zinaweza kuingia kwenye usimamizi wa mirathi ni zile ambazo zinahamishika. Watu wanakuwa na vitu mbalimbali katika maisha yao wanaweza kuwa na vyombo vya usafiri au vyombo vya nyumba au vifaa vya kufanyia kazi, mitambo au mashine. Vitu vyote hivi vinahamishika. Katika usimamizi wa mirathi ni muhimu kubaini juu ya mali za marehemu zinazohamishika ili ziingizwe kwenye utaratibu wa mirathi.

  1. Mali zisizoshikika

Sheria zinatambua kuwa mtu anaweza kuwa na mali zinazoonekana na kushikika na pia zipo kazi ambazo hazishikiki. Kuna sheria inayompa mmiliki juu ya haki miliki ya kazi zake. Sheria hii inalinda kazi za sanaa na ubunifu. Ikiwa marehemu alikuwa mwandishi, au mwanamziki au msanii mwenye kazi za sanaa na ana haki ya umiliki wa kazi zake, basi kazi na haki hizo zinaweza kuingizwa katika utaratibu wa mirathi na familia au warithi wake wakanufaika na mapato yatokanayo na kazi husika.

  1. Madai ya marehemu

Katika maisha ya kawaida watu wanaweza kuwa na madai mbalimbali au pia madeni kadhaa. Iwapo marehemu pindi anapofariki alikuwa na madai yake halali kwa watu au taasisi kadhaa madai hayo hayafi pamoja naye bali utaratibu wa usimamizi wa mirathi unahusisha na madai husika. Zipo sheria ambazo zinaongoza juu ya madai au mafao wanayopaswa kulipwa warithi pindi ndugu yao anapofariki. Ni muhimu kufahamu madai na stahiki mbalimbali ambazo wanapaswa kupata warithi wa marehemu.

  1. Madeni ya marehemu

Hili ni eneo lingine muhimu katika mchakato wa mirathi ya marehemu. Inawezekana kipindi akiwa hai marehemu alikuwa na madeni ambayo hayajalipwa, katika mchakato wa mirathi ni muhimu madeni husika yakaainishwa na ukaandaliwa utaratibu wa kulipa madeni kabla ya kurithisha mali nyingine kwa warithi halali wa marehemu.

Hitimisho

Leo tumejifunza juu ya dhana ya urithi na kuanisha vitu muhimu ambavyo vinarithishwa kwa warithi halali wa marehemu. Msingi wa somo hili ni kuwapa watu nafasi ya kufanya tathmini juu ya mali ambazo wanazo ikiwa zinazohamishika na zile zisizohamishika, madai na hata madeni yao. Ni vyema kuwa na kumbukumbu na pia kuwapa taarifa watu wako wa karibu juu ya mali zako na mahali zilipo. Watu wengi kwa kutokuchukua taadhari na kuishi maisha ya kificho hata wenzi wao kutokujua mali za mume au mke kumesababisha upotevu na dhuluma nyingi za mali kwa warithi halali wa marehemu.

Wewe na mimi ni mashahidi kuna maeneo au viwanja vingi vinaonekana vimetelekezwa na majumba yamebaki kuwa mapagala, inawezekana na ni kwa sehemu kubwa wenye mali hizo wamefariki pasipo ndugu zao kujua kuwa mali hiyo au mali hizo zinawahusu wao.

Chukua hatua madhubuti mtambulishe mali mwenzi wako siku hizi hata ndugu hawaaminiki, tambulisha mali zako kwa watoto wako hata kama ni wadogo wapeleke, tunza nyaraka zako mahali salama, tafuta ushauri wa wanasheria. Kuwa na mwanasheria wa familia ambaye atafahamu masuala ya maisha na mali zenu kuepusha matatizo haya.

‘Andika wosia sasa, maadam unaishi leo’

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili