Sheria Leo. Kuepuka Mchakato wa sheria kama sababu ya watu Kujichukulia Sheria Mkononi

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Leo kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku.tumekuwa na mfululizo wa makala zinazohusu tabia ya watu kujichukulia sheria mkononi. Leo tunakwenda kuangalia sababu mojawapo ya watu kujichukulia sheria mkononi ikiwa ni Kuepuka mchakato mrefu wa kisheria. Karibu tujifunze.

Mchakato wa Kisheria kama sababu ya watu kuchukua sheria mkononi

Katika makala iliyopita tumeweza kuzianisha na kueleza kwa kifupi sababu mbalimbali zinazoweza kuchangia watu kujichukulia sheria mkononi. Mojawapo ya sababu hiyo ni Nafasi ya kulipa kisasi. Leo tunaangalia sababu ya mchakato wa kisheria katika kushughulikia uhalifu au kupatikana kwa haki.

Ni wazi kuwa mchakato wa kisheria katika kushughulikia uhalifu au upatikanaji wa haki huchukua muda mrefu. Hii imekuwa ni sababu mojawapo ya watu kukata tamaa na mchakato huu na kuamua kuchukua maamuzi ya kuchukua sheria mkononi

Mchakato wa kisheria katika kushughulikia suala lolote hasa linalohitaji maamuzi linahusisha vyombo mbalimbali na hatua mbalimbali. Endapo linajitokeza suala lolote ambalo mchakato wa kisheria unahitajika kuchukua mkondo wake kuna hatua zinazotakiwa kuchukuliwa;

  • Taarifa ya tukio au tatizo katika vyombo vinavyohusika. Hii ina maana kama tatizo linahusiana na jinai basi chombo mahsusi ni Jeshi la Polisi kupata taarifa ya tukio husika. Endapo tatizo ni la madai ni vyema kupata ushauri wa wanasheria kujua namna bora ya kuanzisha mchakato wa kisheria kushughulikia tatizo husika
  • Uchunguzi wa tukio au taarifa; mara nyingi matukio au taarifa za kijinai zinaingia katika mchakato wa uchunguzi yaani upelelezi. Hapa vyombo vinavyohusika vitakusanya ushahidi kutoka kwa mashahidi na kuweka kumbu kumbu zinazotakiwa kwa ajili ya kushughulikia tatizo husika
  • Mashitaka; edapo taarifa za uchunguzi zitajitosheleza basi mashitaka yataandaliwa na taasisi ya mashitaka na kupelekwa kwenye chombo cha uamuzi.
  • Kusikilizwa kwa mashitaka na maamuzi; mchakato wa kisheria unatoa nafasi kwa mtu anayetuhumu na anayetuhumiwa mbele ya mahakama kutoa hoja na ushahidi wa kila upande. Hapa ushahidi na vielelezo vinawasilishwa
  • Nafasi ya kukata rufaa; mchakato wa kisheria pia unahusisha nafasi ya kukata rufaa kwa yule asiyeridhika na maamuzi ya mahakama kwenda ngazi ya juu ambapo rufaa inaweza kukubaliwa au kukataliwa. Ngazi za rufaa zipo zaidi ya moja kutegemea na ngazi ya mahakama iliyosikiliza mashitaka ya awali.

Ndugu msomaji kama tulivyoona kuwa suala la mchakato wa kisheria katika kutoa haki au kutatua changamoto ya kisheria inachukua muda mrefu na unahusisha vyombo vingi. Kwa hali ya mfumo huu katika nchi zetu za kiafrika kuna changamoto kubwa ya rasilimali watu wa kuwezesha mchakato na pia rasilimali fedha. Jeshi la Polisi halijitoshelezi kwa rasilimali watu na fedha kukidhi haja ya kushughulikia matatizo yote haya, hali kadhalika ofisi ya mwendesha mashitaka na mahakama zetu si za kutosha kukabiliana na changamoto hizi.

Katika hali kama hii je, ni sahihi kwetu kuchukua hatua za mkato kwa sababu tu mchakato wa kisheria unachukua muda mrefu?

Hatua za kuchukua

  • Elimu kwa jamii inahitajika hasa katika kuishi kwa kuzingatia sheria kwani kitendo cha kuvunja sheria kitasababisha usumbufu si tu kwa mtuhumiwa bali kwa jamii nzima kupoteza muda mwingi kufuatilia haki
  • Wananchi wajihamasishe kama walivyohamasika katika kushiriki shughuli nyingine katika jamii za michango ya sherehe, basi wachange hata katika kuboresha ulinzi na usalama kwa ujenzi wa vituo vya Polisi katika makazi yao. Kama tunavyohamasishana kwenye maeneo mengine ikiwa kujenga shule au nyumba za ibada basi iwe kawaida na kutazama juu ya ulinzi wetu
  • Kuwa jamii ya maridhiano katika masuala ambayo yanaweza kuridhiana. Hii haimaanishi watu kuacha kushughulikia uhalifu bali yapo masuala ambayo kwa mazungumzo yanaweza kumalizwa mfano migogoro mingi ya ardhi iliyo mahakamani kama pande zinazohusika zingekaa na kuridhiana basi wasingekuwa mahakamani. Suala la kwenda mahakamani liwe ni suluhu ya mwisho kabisa endapo njia zote za kumaliza tatizo zimeshindikana.

Bila ubishi mchakato wa kisheria katika kushughulikia matatizo ya kisheria ndani ya jamii ni mrefu na unachukua muda mwingi. Si vyema kuwa na jamii ambayo inapoteza muda katika malumbano bali tutumie muda vizuri kwa kuzalisha. Maeneo mengi yamesimama kimaendeleo kutokana na migogoro iliyopo mahakamani. Hali hii inakatisha tamaa wadaawa na wanaamua kuchukua sheria mikononi mwao.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili