Kitendo cha Kijinai ‘Actus reus’
Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji wa makala za Sheria Leo ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Katika makala iliyopita kwenye tuliangalia kwa utangulizi juu ya Viashiria vya Kosa la Jinai, ambapo tulijadili juu ya historia ya adhabu kwa makosa ya jinai na mabadiliko yake. Leo tunakwenda kuangalia tena kwa undani juu ya Viashiria vya Kosa la Jinai.
Dhana Kuu za Viashiria vya Kosa la Jinai
Katika makala iliyopita tumeweza kuona juu ya dhana iliyoanzishwa kama mbadala wa kutoa adhabu kwa kila tendo ambalo ni kinyume cha sheria kwamba mtu hawezi kuadhibiwa kwa kitendo tu mpaka pale itakapodhibitika kuwa wakati anatenda tendo husika alikuwa amedhamiria ndani ya fikra zake kutenda kosa husika.
Dhana hii kama inavyoelezwa katika lugha ya Kiingereza kwa maneno haya
‘the act itself does not constitute guilt unless done with a guilty intent’
Kupitia msemo huu tunapata kuona kuwa Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 Kifungu cha 10 kinaeleza pia sheria hii
‘Kulingana na masharti yaliyotajwa katika Kanuni hii kuhusiana na vitendo vya uzembe na kuacha kufanya, mtu hatawajibika kwa kosa la kijinai kwa kutenda au kuacha kutenda jambo ambalo limetokea bila ya idhini yake, au kwa tukio lililotokea kwa bahati mbaya’.
Ufafanuzi
Kifungu cha 10 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kinaeleza wazi kuwa mtu yeyote hatawajibika kisheria kwa kitendo au kuacha kutenda jambo ambalo limetokea bila ya idhini au kudhamiria kutoka kwenye fikra zake mwenyewe.
Kwa msingi wa dhana hii ndipo tunaona kuwa ili kosa la kijinai au mtu atiwe hatiani kwa kosa la kijinai ni lazima kudhibitishwa viashiria vya kosa ambavyo ni kitendo kinyume cha sheria na dhamira ya kutenda kosa.
Maana ya Kitendo cha kijinai
Katika kudhibitisha juu ya kosa analokabiliwa nalo mtuhumiwa ni lazima mahakama ijiridhishe kuwa mtuhumiwa ndiye aliyetenda kosa husika. Katika lugha ya kilatini kitendo cha kijinai kinajulikana kama ‘Actus reus’.
Katika tafsiri ya sheria kuhusiana na kitendo ina maanisha ‘mtu kutenda jambo kinyume cha sheria au kuacha kutenda kitendo ambacho anawajibika kisheria’. Hivyo suala la kitendo kisheria lina maana pana zaidi ya kutenda tu bali hata kutokutenda kile ambacho unawajibika kutenda.
Mfano.1
Sheria inakataza kuiba hivyo mtu ambaye anatuhumiwa kuiba ni lazima awe amechukua hatua ya kutenda kitendo hicho cha kuiba.
Mfano.2
Sheria inatoa wajibu wa mtu kutunza watoto wenye chini ya miaka 14 ndani ya himaya yake endapo mtu huyo atakiuka wajibu huo na madhara yakajitokeza kwa mtoto chini ya miaka 14 kwa kukosa matunzo aliyostahili basi muhusika atawajibika kijinai kwa makosa husika.
Katika shauri la Queen vs Instan, 1893, mtuhumiwa aliishi na marehemu kwa kipindi Fulani ambapo kabla ya mauti, mareemu aliugua kwa muda kiasi cha kushindwa kujihudumia. Mtuhumiwa alishindwa kumsaidia kwa kumpa chakula wala madawa kiasi kwamba kutotimiza wajibu huo kukapelekea mauti. Mahakama katika uamuzi wake ukasema kuwa mtuhumiwa alikuwa na wajibu wa kisheria katika mazingira yake kumpatia marehemu chakula na uangalizi wa kimatibabu na kwamba kifo chake kimechangiwa na mtuhumiwa kutotimiza wajibu wake. Mtuhumiwa akatiwa hatiani kwa kosa la kuua pasipo kukusudia.
Hitimisho
Leo tumejifunza kiashiria kimojawapo cha kosa la jinai yaani Kitendo kilichozuiwa na sheria. Maana ya kitendo si tu kutenda bali hata kutokutenda kile ambacho unawajibika kutenda. Tumekuwa mashuhuda wa siku hizi za karibuni wazazi au walezi wamekuwa wakifungia watoto au watu wenye ulemavu katika vyumba na nyumba zao kwa kipindi kirefu. Watu hawa wanafanya makosa ya kijinai kwani hawatimizi wajibu wao kama sheria inavyowataka kufanya. Hivyo ni muhimu kufahamu kuwa ili kosa liwe kosa la kijinai lazima kuwe na kitendo au kuacha kutenda kile ambacho unapaswa kutenda kisheria.
Endelea kufuatilia makala ijayo ili kujifunza zaidi juu ya kiashiria kingine cha kosa la kijinai.
‘Anzisha na fuata mchakato wa kisheria katika kushughulikia masuala ya uhalifu katika jamii’
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.
Muhimu
Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .
‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’
Nakutakia siku njema.
Wako
Isaack Zake, Wakili
This is very good and I support this idea to the fullest.
Let’s keep this rolling and help individuals on the key areas on how to understand basic knowledge of law.
Kwakweli nimefarijika sana.
Karibu sana ndugu yangu Makaranga mdau wa sheria za Kazi nashukuru kwa mchango wenu wote kufanikisha ndoto za uliza sheria kuwa chombo cha kufundisha na kutoa ufafanuzi katika maeneo mbalimbali ya kisheria ikiwemo sheria za kazi. Karibu sana
Explain the legal sovereignty immunity basically in Tanzanian countr?
Karibu ndugu Amina, nadhani swali uliloleta ni la darasani halikutokana na makala ambazo tumeendelea kuchapisha, hivyo ni muhimu kuzingatia namna bora ya wengi zaidi kupata maarifa kwa kuuliza au kutaka ufafanuzi kwa yale hasa tunayojifunza. ikiwa kuna changamoto za darasani ambazo ungependa kushirikisha wanasheria basi unaweza kutumia utaratibu mwengine uliotolewa. Nikutakie kila la heri katika masomo yako. Usiache kufuatilia uliza sheria
Nimeelimika katika suala hili
Asante sana ndugu Clemence Mwakasendo kwa kuwa pamoja nasi, tutaendelea kutoa maarifa zaidi ya kisheria
Aiseh! Wakili Isaack, ubarikiwe kwa jambo hili jema sana.
Aksante kwa kutuambukiza ufahamu
Karibu sana ndugu Kaseha Wilson tunashukuru kwa kuwa msomaji wetu.