44. Dhana ya Kukazia Uamuzi wa Tume

Utangulizi

Karibu tena ndugu msomaji wa makala za uchambuzi wa sheria ya Kazi. Tunaendelea kuchambua sheria hii yenye mahusiano ya mfanyakazi na mwajiri katika mfululizo wa makala. Katika makala iliyopita tuliangalia juu ya Haki ya Marejeo au Mapitio juu ya Uamuzi wa Tume. Leo tunakwenda kuangalia juu Dhana ya Kukazia Tuzo au Uamuzi wa Tume.

Nini maana ya Kukazia Hukumu?

Kukazia hukumu au maamuzi ya chombo cha kimahakama ni mchakato wa utekelezaji wa amri ya mahakama.

Haitoshi tu maamuzi ya mahakama au Tume kukupa haki fulani, muhimu zaidi ni kutekelezwa kwa maamuzi hayo na wewe kuipata haki husika.

Katika mchakato wa mashauri ya madai ambapo pia migogoro ya kazi inaangukia katika kundi hilo, mchakato wa kukazia uamuzi au hukumu unajitokeza mara kwa mara endapo amri ya Tume au Mahakama ya Kazi haijatekelezwa ndani ya muda uliotolewa.

Mfano

Amri ya Tume katika Tuzo imeamuru mfanyakazi arudishwe kazini na kulipwa mishahara yake yote katika kipindi alichokuwa nje ya kazi na amri hiyo inapaswa kutekelezwa ndani ya siku 21.

  • Je, ni kitu gani kinatokea endapo mwajiri akikaidi kutekeleza amri hiyo ndani ya muda huo husika?
  • Je, mfanyakazi anaweza kuchukua hatua gani kisheria ili amri ya Tume itekelezwe?

Majibu ya maswali haya ndiyo yanayoelezea dhana nzima ya Kukazia hukumu ya Mahakama au Tuzo ya Tume.

Jinsi ya Kukazia Hukumu ya Tume

Mara baada ya uamuzi wa Tume yaani Tuzo, mwamuzi anatoa muda wa utekelezaji wa maamuzi au amri zilizotolewa ndani ya Tuzo inaweza kuwa ndani ya siku 14 mpaka 21 kulingana na mwamuzi atakavyoona.

Endapo upande unaopaswa kutekeleza amri zilizopo ndani ya Tuzo umeacha kutekeleza katika kipindi kilichotolewa na pia muda wa kuomba marejeo au mapitio yaani majuma 6 umepita, ndipo upande ulioshinda Tuzo unaweza kuchukua hatua za kukazia maamuzi au amri ya Tuzo.

Sheria ya Ajira inaelekeza juu ya mamlaka ya Mahakama ya Kazi kusimamia utekelezaji wa maamuzi ya Tume au Tuzo zilizotolewa na Tume.

Hivyo upande ulioshinda mbele ya Tume utafanya maombi maalum ya kukazia maamuzi ya Tuzo mbele ya Mahakama ya Kazi ili mahakama itumie mamlaka yake kumlazimisha aliyeshindwa kutekeleza matakwa ya amri ya Tume.

Utekelezaji huo wa amri ya Tume utasikilizwa na Msajili wa Mahakama ya Kazi na kutolewa maamuzi juu ya utekelezaji.

Zipo njia kadhaa ambazo Mahakama itatoa maamuzi ya namna ya utekelezaji au ukaziaji hukumu ya Tuzo. Mfamo

  • Kuweza kumtaka mdaiwa alipe au aweke kiasi anachopaswa kulipa katika akaunti maalum, au
  • Kukamata mali za mdaiwa kupitia madalali wa mahakama au
  • Kumfunga mdaiwa mpaka deni husika lilipwe.

Hitimisho

Ni muhimu sana kwa wadaawa wa mashauri ya kazi kufahamu haitoshi tu kuwa na Tuzo mkononi inayoelezea kushinda kwako kesi bali msingi wa kesi nzima ni kupata haki yako mkononi ikiwa ni kiasi cha fedha kama fidia au mishahara au amri ya kurejeshwa kazini. Hivyo ni lazima kuwa na ufahamu na kufanya maandalizi yanayopasa ya kisheria ili kupata haki hiyo. Mchakato wa kisheria wa kukazia hukumu nao una changamoto zake ni muhimu kuzifahamu na kukabiliana nazo.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili.