89. Nani mwenye mamlaka ya kusitisha ajira ya mwajiriwa?

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Tumeendelea kujifunza changamoto mbalimbali zinazotokea katika mahusiano ya kiajira na kuzitafutia ufumbuzi kwa lengo la kuboresha mahusiano ya kiajira. Leo tunakwenda kuangalia changamoto ya mamlaka ya kusitisha ajira ya mwajiriwa. Karibu tujifunze.

Swali ya Msomaji wa Uliza Sheria

Makala hii ni matokeo ya swali ambalo niliulizwa na msomaji wa blog hii ya uliza sheria akiuliza

‘Mimi ni mwajiriwa katika kampuni ambapo mkurugenzi mmojawapo alifariki na kubaki mwengine. Familia ya mkurugenzi  ilifanya taratibu za mirathi  na mke wake kuteuliwa kusimamia mirathi, cha kushangaza ameanza kuandika barua za kutufukuza kazi. Sheria inasemaje? Msomaji kutoka Arusha

Inawezekana wewe msomaji umewahi kukutana na changamoto kama hii au inayofanana na hii, pale mwajiri wako anapofariki na mtu mwengine kuingia kuchukua wajibu wake na kukuachisha kazi, je utaratibu wa Kisheria unasemaje. Tumeshuhudia hali hii ikijitokeza ndani ya jamii na waajiriwa wengi wanakosa mwelekeo na kutokujua hatua za kuchukua.

Mambo ya Msingi

Yapo mambo ya msingi kujua ili kuchukua hatua sahihi katika mazingira ambayo mtu aliyekuajiri amefariki na wewe bado upo au mkataba wako wa ajiri unaendelea.

  1. Lazima ujue endapo uliajiriwa na mtu binafsi au taasisi. yaani Kampuni au taasisi yoyote inayoundwa kwa mujibu wa sheria
  2. Nani mwenye mamlaka ya kukuajiri na kukuachisha kazi katika ofisi yako

Umuhimu wa kufahamu mambo haya mawili ya msingi, utakusaidia mwajiri au mfanyakazi kujua hatua sahihi za kuchukua endapo changamoto itajitokeza.

Leo tutaichambua hoja ya kwanza ya endapo umeajiriwa na mtu binafsi au taasisi.

Nani Mwajiri wako?

Hili ni swali muhimu sana kwa watu wote kulifahamu hasa katika masuala ya ajira. Watu wengi huwatazama mabosi wao kufikiri ndio waajiri wakati inawezekana kabisa kwenye mkataba wa ajira mwajiri ni taasisi au kampuni. Hili ni eneo muhimu sana kwa waajiriwa kujua kwa hakika endapo wanafanya kazi kwa mtu binafsi au taasisi au kampuni.

Sheria za mikataba zinatambua aina mbili za watu yaani

  • Mtu kwa maana ya mwanadamu
  • Mtu kwa maana ya sheria – huyu ni taasisi au kampuni au shirika linaloundwa kwa mujibu wa sheria

Hivyo mwajiriwa anapaswa kufahamu katika mkataba wake wa kazi endapo aliajiriwa na mtu binafsi au taasisi.

Kwa mujibu wa tafsiri ya neno mwajiri sawa na Kifungu cha 4 cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, 2004 ina maana ya

‘mtu yeyote, ikiwa ni pamoja na Serikali na wakala mtendaji, anayemwajiri mwajiriwa’

Kwa tafsiri ya kiingereza inaonekana vizuri zaidi neno mwajiri likimaanisha

“employer” means any person, including the Government and an executive agency, who employs an employee;

Tunaona katika tafsiri hii ikionesha neno ‘any person’ hii ina maana anaweza kuwa mtu wa asili yaani mwanadamu au mtu wa kisheria kama Taasisi, Kampuni au shirika kama ilivyooneshwa Serikali au Wakala.

Kwa upande mwengine mwajiriwa ina maana ni lazima awe mtu wa asili yaani mwanadamu na si mtu wa kisheria. Hii ni kwa mujibu wa tafsiri ya Kifungu cha 4 cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini.

Mwajiriwa ina maana ya mtu ambaye

  • Ameingia kwenye mkataba wa ajira; au
  • Ameingia kwenye mkataba mwengine wowote ambao
  • Mtu anafanya kazi mwenyewe kwa niaba ya upande mwengine wenye mkataba; na
  • Upande mwengine sio mteja au mtaalamu yeyote, biashara au shughuli yoyote inayofanywa na mtu huyo; au
  • Anachukuliwa kuwa mwajiriwa na Waziri chini ya Kifungu cha 98(3)

Kwa tafsiri hii tunaona ya kuwa mwajiriwa ni ‘mtu’ yaani mwanadamu ingawa tafsiri iliyotumiwa katika neno mwajiriwa na mwajiri kusema ni mtu lakini tofauti yake unaiona kwenye tafsiri ya kiingereza.

“employee” means an individual who—
has entered into a contract of employment; or
has entered into any other contract under which—
the individual undertakes to work personally for the other party to the contract; and
the other party is not a client or customer of any profession, business, or undertaking carried on by the individual; or
is deemed to be an employee by the Minister under section 98(3);  

Hapa unaona neno ‘mtu’ kwa Kiswahili limetafsiriwa ‘individual’ kwa lugha ya kiingereza kutofautisha na neno ‘person’. Hii ina maana mtu ya ‘individual’ ni mwanadamu na mtu kwa maana ya ‘person’ anaweza kuwa mwanadamu au taasisi.

Hivyo ni muhimu sana kwa waajiri pamoja na wafanyakazi kujua endapo mwajiri anaweza kuwa mtu kwa maana ya mwanadamu na mtu kwa maana ya kisheria yaani Taasisi au kampuni au shirika.

Tofauti hii ya nani ni mwajiri inakuwa msingi wa kukusaidia kujua hatua za kuchukua endapo changamoto ya kifo inapotokea.

Endelea kufuatilia mfululizo huu tunapojibu swali hili la wasomaji wetu katika makala zijazo.

MUHIMU

Ningependa kukukaribisha ndugu msomaji wa Uliza Sheria, ikiwa una maswali yanayohusu suala la KAZI na AJIRA katika sheria, basi karibu kuuliza kwa mawasiliano hapo chini na sisi tutatoa ufafanuzi kunufaisha watu wote. Tuma ujumbe mfupi kwenye namba za simu au barua pepe.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Isaack Zake, Wakili

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com