Happy Birthday Uliza Sheria

Utangulizi 

Habari za leo ndugu yangu msomaji na mfuatiliaji wa mtandao wa Ulizasheria. Awali ya yote napenda kumshukuru Mungu kwa nafasi hii tuliyopewa leo kuadhimisha mwaka mmoja katika kazi ya kutoa elimu na ushauri kwa masuala ya kisheria.

Utakumbuka ndugu yangu msomaji mnamo tarehe 20th August 2017 tuliwakaribisha wote kufuatilia blog yetu hii ya uliza sheria.

Mtandao wa ulizasheria ulijiwekea malengo ya kutimiza ambayo yamekuwa dira ya kazi yetu kila mara.

Lengo kuu la mtandao huu.

 • Kutoa elimu ya msingi ya sheria kwa mwananchi wa kawaida kabisa ili apate kufahamu namna ya kuishi kwa mujibu wa sheria
 • Kutatua matatizo na kutoa majibu ya maswali ya jamii katika changamoto za kisheria wanazokumbana nazo kila siku.
 • Kusaidia lengo la Tanzania 2025 kuwa nchi yenye kuzingatia sheria na utawala bora.

Hakika kwa sehemu yetu tunasema tumefanya wajibu wetu kwa kadri tulivyoweza kwa kipindi cha mwaka 1.

Katika kipindi cha mwaka 1 tumeweza kuandika makala 205 za maeneo mbalimbali ya kisheria ikiwa ni pamoja na;

 • Makala za jumla
 • Katiba
 • Sheria za ardhi
 • Sheria za mikataba
 • Sheria za madhara
 • Sheria za ndoa
 • Sheria za mirathi
 • Sheria za makosa ya Jinai
 • Sheria za usalama barabarani
 • Sheria za Mtoto
 • Sheria za haki miliki
 • Sheria za Kazi

Kwa kipindi cha mwaka uliza sheria imeweza kufikia mikoa yote ya Tanzania ambayo tumepata wasomaji na wafuatiliaji wa mtandao wa ulizasheria. Tumepokea maswali kutoka kila upande wa Tanzania na hata nchi za nje wakitaka kujua ufafanuzi wa mambo mbalimbali ya kisheria.

Pia tumepokea simu kutoka vituo kadhaa vya redio vikitaka kujua ufafanuzi wa masuala ya kisheria na hata magazeti mbalimbali.

Haya yote ni mafanikio yetu sisi na wewe ndugu msomaji kwa kazi kubwa hii ambayo mpaka sasa tunaendelea kuifanya kwa pamoja.

Matarajio Yetu

Katika kuanza mwaka wa 2 wa huduma zetu kama ulizasheria tunatarajia kuweka nguvu na maarifa zaidi katika kushughulikia masuala mbalimbali ya kisheria yanayowatatiza wananchi na wadau wetu.

Aidha katika mwaka wa 1 tumetumia muda mwingi kuandika juu ya makala mbalimbali zinazotoka kwetu. Ni mipango yetu kwa mwaka huu wa 2 tuanze kuandaa makala zinazotokana na maswali ya wasomaji wetu kwa kadri inavyowezekana. Hii itasaidia zaidi kutatua changamoto ambazo zinawakumba wasomaji wa mtandao huu na hivyo kupelekea kutimizwa kwa lengo la kutatua matatizo ya kisheria wao wenyewe.

Tunatarajia kuboresha zaidi mfumo wa kupokea maswali hasa kwa njia ya sms, watsup au e-mail. Ni wazi kwamba tumekuwa na changamoto kubwa ya watendaji wa uliza sheria hivyo bado hatuwezi kujibu simu ya kila mmoja. Hivyo tutaandaa utaratibu mzuri wa kuweza kujibu maswali yako pasipo kuwa na ulazima wa kupiga simu. Endapo hitaji la simu au kuongea moja kwa moja na mwanasheria litahitajika basi utajulishwa utaratibu husika.

Tunatarajia kuanzisha siku ya ulizasheria ambayo tutakuwa tunaiadhimisha kila siku ya tarehe 20 mwezi wa Agosti ya kila mwaka, ambapo tutakutana na wadau wetu wa mtandao wa uliza sheria kwa lengo la kuwahudumia ana kwa ana.

Ni ahadi yetu kwako msomaji kukuletea suluhu ya kisheria katika maeneo mbalimbali ambayo blog yetu itaendelea kutoa huduma zake.

Nikutakie heri na fanaka ya kuadhimisha mwaka 1 wa mtandao wa uliza sheria.

Tunakukaribisha kwa maoni, mapendekezo, ushauri wa namna bora ya kuboresha huduma zetu kwa siku zijazo. Tafadhali wasiliana nasi kwa maelekezo yaliyoandikwa hapa chini.

Shukrani za kipekee

kwa namna ya kipekee ninapenda kukushukuru sana rafiki yetu, ndugu yetu na Kocha Dr. Amani Makirita kwa sehemu kubwa uliyofanya kufanikisha uwepo wa blog hii hata sasa. Kazi yako hii inawafikia watanzania na kuwagusa hata wengine walio nje ya nchi. Shukrani hizi ziwaendee pia wanamafanikio wa Kisima cha Maarifa haya ni mafanikio yetu sote. Tuendelee kuweka kazi na maarifa kila siku.

Mungu awabariki sana.

Wako

Isaack Zake

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 au 0787 466 687 na email zakejr@gmail.com

DARASA LA ULIZA SHERIA 2018

Maono

Kuwa kituo cha kwanza cha kutoa maarifa mbalimbali ya kitaaluma ili kuleta ufanisi, tija, manufaa kwa jamii.

Dhima

Kwa nidhamu, uadilifu na weledi tunaweza kufikia maono ya kutoa maarifa kwa jamii.

Misingi ya Darasa

 • Uadilifu
 • Kujifunza
 • Huduma bora kwa wateja

Malengo

 • Kutoa elimu ya sheria kwa jamii ili kuisaidia kutatua changamoto za kila siku za kisheria.
 • Kutoa ushauri kwa wanajamii ambao utawasaidia kufanya maamuzi sahihi ya kisheria kila wakati.
 • Kusadia Taifa letu kupunguza migogoro ya mara kwa mara kwa wanajamii kupitia elimu ya sheria na ushauri wa kisheria.

 1.0. Utangulizi

Mtandao wa Uliza Sheria ulianza rasmi mnamo mwezi Augusti 2017. Hata hivyo shughuli za Uliza Sheria za utoaji wa elimu ya kisheria na ushauri wa masuala ya kisheria zilianza tangu mwaka 2010 katika ngazi mbalimbali. Mnamo mwaka 2009/2010 waanzilishi wa Uliza Sheria walianzisha Taasisi isiyo ya kiserikali ya msaada wa kisheria iliyoitwa Community Legal Service Centre iliyofanya kazi kati ya mwaka 2009 – 2012. Taasisi hii ilitoa ushauri na msaada wa kisheria hasa kwa wakazi wa Dar es Salaam. Pia waanzilishi kwa nafasi mbalimbali wamekuwa wakitoa elimu ya sheria kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria ambao wanachukua masomo ya Shahada ya Sheria kati ya mwaka 2010 – 2015. Pia kazi za waanzilishi wa Uliza Sheria zimesambaa katika vyuo mbali mbali kwa ajili ya kutoa maarifa kwa wanafunzi wa sheria wa ngazi tofauti.

Uliza Sheria imekuja kutokana na changamoto pana ya uhitaji wa elimu ya sheria kwa jamii nzima. Hapo awali maarifa ya sheria yalikuwa yanatolewa kwa wanafunzi  wa sheria peke yao. Huduma hii haikuweza kukidhi haja kubwa iliyopo kwa jamii ndipo taasisi ikaja na mfumo wa kutoa maarifa kwa jamii pana zaidi ili kusaidia wananchi kuishi kwa mujibu wa sheria.

Kwa takribani kipindi cha miezi 4 tangu Uliza Sheria ianze kutoa mafunzo kwa jamii pana kupitia blog ya www.ulizasheria.co.tz tumeona mafanikio makubwa na kiu ya wananchi kutaka kujifunza zaidi juu ya masuala mbalimbali ya kisheria ambayo wanakutana nayo kila siku. Changamoto kubwa tuliyokutana nayo ni kupata maswali mengi na simu nyingi zikitaka ufafanuzi wa masuala ambayo tunaandika mara kwa mara.

Hivyobasi, uliza sheria imeandaa mpango wa kutoa mafunzo kupitia Darasa la Sheria ambalo litaendeshwa kupitia group ya watsapp kwa watu wote wanaopenda kujifunza zaidi kuhusiana na sheria ili kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi wakati wote.

1.1. Kwa nini Darasa Uliza Sheria

Zipo sababu kadhaa ambazo ni muhimu kwako ndugu msomaji za kukuwezesha kujiunga na Darasa la Uliza Sheria. Katika maisha kabla ya kuchukua uamuzi wowote ni muhimu sana kufanya tathmini ya kina ili kuona manufaa ya uamuzi wako kwa sasa na baadae. Hapa nitakutajia baadhi ya faida za wewe kujiunga na Darasa la Uliza Sheria

 • Kupata maarifa ya kisheria kila siku. Hii ina maana utakuwa na fursa ya kujifunza juu ya sheria kila siku katika mwaka yaani siku 365.
 • Kupata fursa ya kuuliza maswali ya kisheria kutokana na masomo husika na kujibiwa na wanasheria katika Darasa
 • Kupata nafasi ya mjadala juu ya mada mbalimbali za kisheria siku moja katika wiki.
 • Kupata fursa ya ushauri wa kisheria katika mambo mbalimbali unayokabiliana nayo.
 • Kupata kipaombele katika kutatua changamoto za kisheria ambazo zinahitaji huduma ya wanasheria.
 • Kupata fursa ya kujifunza kutokana na uzoefu wa watu wengine kwenye Darasa la sheria.

Hizi ni baadhi tu ya faida au huduma utakazopata ndani ya Darasa la Uliza Sheria kwa kipindi cha mwaka mzima.

1.2. Vigezo vya kujiunga na Darasa la Uliza Sheria

Je, ni vigezo gani vya kukufanya wewe kuwa msomi wa Darasa la Uliza Sheria?

Uliza sheria imeandaa utaratibu wa vigezo na masharti ambayo mtu anapaswa kuzingatia ili kujiunga na Darasa la Uliza Sheria.

 • Msomi wa uliza sheria angalau awe ana umri kuanzia miaka 18 na kuendelea
 • Msomi awe na uwezo wa kusoma na kuandika kwa lugha ya Kiswahili
 • Msomi kuzingatia kanuni na masharti ya Darasa la Sheria wakati wote
 • Msomi kulipia ada/gharama za mafunzo kabla ya kuunganishwa kwenye Darasa la Sheria
 • Msomi kuzingatia matumizi bora ya lugha na matumizi ya tija katika mtandao. Hii ni kuepuka lugha za matusi, kejeli au ubaguzi wa aina yoyote ile au uvunjifu wa amani na Sheria za Nchi.

Haya ni baadhi ya masharti muhimu ya kuzingatia ili msomi akidhi vigezo vya kujiunga na Darasa la Sheria.

1.3. Gharama za Kujiunga na Darasa la Uliza Sheria

Je, ni kiasi gani msomi wa sheria anapaswa kulipia kama ada ya mafunzo?

Katika mfumo wowote wa kutoa elimu duniani zipo gharama. Gharama hizi unaweza usizione kwa kuwa zinaweza kubebwa na Serikali au Taasisi nyingine lakini haiondoi ukweli kuwa zipo gharama. Gharama za elimu zinatofautiana kutokana na kiwango cha elimu husika na thamani ya elimu kwa wale wanaoipokea.

Uliza Sheria kwa kuzingatia umuhimu wa huduma hii ya elimu na mengineyo yanayoambatana nayo imefanya tathmini na kuweka kiwango cha ada ambacho kila mmoja mwenye kutaka kujifunza anaweza kumudu kulipia gharama hizo.

Uliza sheria imeweka kiwango cha ada/gharama ya mafunzo ya sheria kiasi cha Tsh.60,000/- kwa mwaka kwa kila msomi mwenye nia ya kujiunga na Darasa la Sheria.

Lengo la kuweka gharama ni kuhakikisha kazi hii inapatiwa thamani kwa wale wanayoipokea na kufidia kwa kiasi kigodo gharama za maandalizi ya masomo na kazi nyingine za mtandao wa uliza sheria.

Ada hii italipwa mara moja yaani kwa mkupuo mmoja wakati wa kujiunga na Darasa la Uliza Sheria.

1.4. Ratiba ya Siku katika Darasa la Uliza Sheria

Kama tulivyoeleza awali nia ni kutoa maarifa ya kisheria kila siku kwa wasomi wa sheria. Hivyo uliza sheria imeandaa utaratibu wa kila siku wa namna maarifa na shughuli za darasa zitakavyoongozwa.

 • Kila asubuhi kutumwa somo/makala ya siku kwenye group ya Darasa la Uliza Sheria
 • Wasomi kujisomea makala na kuuliza maswali na kutaka ufafanuzi juu ya somo la siku husika
 • Waalimu kujibu maswali na kutoa ufafanuzi wa somo husika kwa siku
 • Wasomi wanaweza kuuliza maswali kutokana na makala za uliza sheria zilizowahi kuchapishwa.
 • Kutakuwa na saa 1 kwa siku kwa ajili ya kujibu maswali na kutoa ufafanuzi juu ya hoja mbalimbali kutokana na maswali ya wasomi.
 • Katika siku 1 kwa juma kutakuwa na mada maalum ambayo waalimu watajadili na wasomi katika kipindi cha masaa 2.

1.5. Je, unaweza kunufaika na uliza sheria pasipo kujiunga na Darasa la Uliza Sheria

Jibu lake ni NDIO bado ndugu msomaji unaweza kunufaika na huduma za uliza sheria hata kama hujajiunga na Darasa la Uliza Sheria. Ikiwa hapo awali ulikuwa ukipata makala kwenye blog ya www.ulizasheria.co.tz basi makala hizo zitaendelea kuwepo. Pia kama ulikuwa ukipata kwa njia ya e-mail au watsapp basi utaendelea kuzipata kila siku.

Hatahivyo, nafasi ya kuendelea kupata huduma za kujibiwa maswali au ushauri zitaratibiwa sawa na maelekezo yaliyopo kwenye blog ya www.ulizasheria.co.tz juu ya kuandika maswali yako kwa njia ya e-mail.

Hivyo wewe uliyekuwa unapata makala na elimu kama hapo awali usihofu kwani utaendelea kupata. Mpaka sasa zipo zaidi ya makala 130 tayari zimechapishwa tangu mwezi Augusti 2017, unaweza kuzipitia zinazohusu masuala ya sheria za kazi, Katiba, Ardhi, Mirathi n.k. utaweza kusoma makala hizo kupitia ukurasa wa;

 • Sheria Leo
 • Elimu ya Sheria

1.6. Masomo katika Darasa la Uliza Sheria

Sheria ni msitu mnene sana hata kwa wanasheria wenyewe. Yapo mambo mengi na karibu mambo yote kwenye maisha yana sheria zake. Hatahivyo kutokana na uzoefu, utafiti tuliofanya katika kipindi cha zadi ya miaka 10 katika taaluma hii ya sheria tumeona maeneo ya msingi ambayo jamii inakabiliana nayo siku kwa siku.

Maeneo haya ya kisheria ambayo tumeyaainisha kushirikiana kwa mwaka 2018 ndiyo maeneo ambayo yana migogoro mingi sana mahakamani. Mojawapo ya sababu kubwa ya migogoro hii kuwepo mahakamani ni ukosefu wa elimu sahihi kwa wananchi.

Hivyo masomo yatakayoendeshwa katika Darasa la Sheria yatahusisha sheria zifuatazo;

 • Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
 • Sheria za Ardhi
 • Sheria za Mirathi
 • Sheria za Mikataba
 • Sheria za Kazi
 • Sheria za Jinai
 • Sheria za Biashara/Makampuni
 • Sheria za Familia (Sheria ya Ndoa na Mtoto)

Haya ni maeneo muhimu ya kisheria ambayo yatahusishwa kujadiliwa siku kwa siku na katika mada za wiki katika mwaka wa 2018.

1.7. Namna ya Kujiunga na Darasa la Uliza Sheria

Kama tulivyoeleza awali juu ya vigezo na masharti ya mtu kujiunga na Darasa, kimojawapo ni kulipia ada ya mwaka kiasi cha Tsh.60,000/- . Ada hii italipwa mara moja tu yaani kwa mkupuo mmoja.

Darasa la Uliza Sheria limekusudia kuanza rasmi tarehe 1/1/2018. Hivyo ni muhimu kuanza kulipa mapema ili kuunganishwa kwenye group ya watsapp.

 • Endapo msomi atalipia ada kabla ya tarehe 1/1/2018 atapata punguzo la kiasi cha Tsh.10,000/- hivyo atalipia ada ya mwaka kwa 50,000/-
 • Ada itaanza kuhesabika tangu tarehe 1/1/2018.
 • Endapo msomi atajiunga ndani ya mwezi Januari 2018 ada yake itaanza kuhesabika tangu 1/1/2018. Kama akijiunga tarehe yoyote Februari 2018 basi ada yake itaanza kuhesabika tangu tarehe 1/02/2018. Hivyo mwaka wa msomi utaanza kuhesabiwa ndani ya mwezi husika uliolipia ada.

Utaratibu wa kulipa ada

Kwa sasa ada zote zitalipiwa kupitia mawasiliano ya simu kwa tigopesa0713 888 040 yenye majina ya ISAACK DAWSON ZAKE. Mara baada ya kulipia ada husika. Tuma majina yako, kwenye namba hiyo ya 0713 888 040 kwa ujumbe wa watsapp nawe utaunganishwa kwenye Darasa la Uliza Sheria.

Karibu sana kwenye Darasa la Uliza Sheria tujifunze kwa pamoja kwani kujua sheria ni haki yako na kujifunza sheria ni wajibu wako.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Karibu sana.

Isaack Zake, Wakili

Zake Advocates.

www.ulizasheria.co.tz

 

 

 

Sheria Leo.3: Je, Sheria ni Muhimu?

Karibu sana ndugu msomaji wa ukurasa wa Sheria Leo, ambapo tunajifunza mambo mbalimbali ya kisheria ambayo yatatusaidia kila siku kufanya maamuzi sahihi na kuishi kwa mujibu wa sheria. Leo tunakwenda kujibu swali linalosema ‘Je, Sheria ni Muhimu?’ Karibu sana.

Ndugu msomaji ni wazi kabisa mtu hawezi kuhangaika kutafuta kitu au maarifa ya jambo fulani kama halina umuhimu katika maisha yake. Kila siku tunaamka na kwenda kwenye shughuli zetu kutafuta mambo ambayo tunaona ni muhimu kwetu, mfano chakula, mavazi na hata malazi. Tunafahamu umuhimu wa vitu hivi na maana yake katika maisha yetu ndio maana kila kukicha tunatafuta.

Wengi wetu tunadhani kuwa sheria si muhimu kwetu au inawahusu watu fulani au tabaka fulani jambo hili si kweli, sheria inawahusu watu wote. Hivyo ni muhimu kwa kila mtu kuzifahamu sheria. Huwezi kuingia gharama ya kutafuta jambo kama hufahamu maana ya jambo hilo  katika maisha yako.

Kabla hatujajibu swali letu la Je, Sheria ni Muhumu? karibu tuone kwa ufupi nini maana ya Sheria.

Sheria ni mfumo kanuni na taratibu zilizowekwa kwenye jamii na mamlaka kwa ajili ya kuwaongoza matendo yao na mahusiano yao. Sheria ni utaratibu unaotengeneza mfumo na mwelekeo wa maisha chini ya mamlaka husika. Mfano kanuni katika nchi, familia, ukoo, shule na ofisi nk.

Kwa ufafanuzi wa ziada ya maana ya sheria bonyeza hapa Nini Maana ya Sheria?

Kwa maana hii tunaweza kuona umuhimu wa sheria kwani pasipo sheria jamii haiwezi kukaa kwa pamoja na kuweza kustawi na kuwa na maendeleo. Sheria ni muhimu sana kwani ndizo zinaongoza matendo yako na tabia yako kila siku unavyopaswa kuishi katikati ya jamii. Uhuru ambao tunaona tunao ni kwa mujibu wa sheria. Sheria inaongoza kitu cha kuongea, kitu cha kufanya na kitu gani haupaswi kufanya. Ni sawa kusema sheria ni mfumo unaoongoza maisha yetu ya kila siku.

Ndugu msomaji ni muhimu ufahamu kuwa kila unalofanya au usilofanya au unalotamka lina sheria yake au mwongozo wake ambao wewe unapaswa kujuua. Sheria ni mfumo wa ajabu sana ambao unaratibu maisha yako tangu ukiwa tumboni kwa mama yako na hata ukiwa kaburini. Zipo sheria zinazuia utoaji wa mimba (Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura 16 ya Sheria – The Penal Code) na hata sheria ya makaburi (Sheria ya Kuhamisha Makaburi Sura 72 – The Grave (Removal) Act).

Ndugu msomaji kama kuna sheria inayoratibu maisha yako ukiwa bado hujazaliwa na kuna sheria inayoratibu hata masalia ya mwili wako ukiwa umezikwa, je, si zaidi sana kuna sheria za kuratibu maisha yako kila siku.

Unachotakiwa kufanya ndugu yangu kila siku kabla ya kutekeleza maamuzi yoyote iwe kwa maneno au vitendo angalia kama upo kwa mujibu wa sheria.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kwa kutembelea mtandao wako wa  www.ulizasheria.co.tz

Wako

Isaack Zake, Wakili