Kisa Mkasa 8: Mkulima (Said Mwamwindi) kufanya mauaji ya Mkuu wa Mkoa (Dr.Kleruu) – 4

Utangulizi

Karibu tena ndugu msomaji kwenye makala iliyopita tuliweza kuona juu ya utetezi wa kurukwa na akili ulivyojadiliwa na mahakama wakati wa shauri la Saidi Mwamwindi. Tuliona vigezo ambavyo vilitumiwa kuamua endapo wakati akitenda kosa alikuwa na akili timamu au la. Leo tunakwenda kuona utetezi wa Kukasirishwa (Provocation)

Utetezi wa Kukasirishwa (Defense of Provocation)

Hoja nyingine ambayo upande wa utetezi wa kesi ya Saidi Mwamwindi uliwasilisha kama utetezi ni kitendo cha kukasirishwa kwa Said kilichofanywa na marehemu Dr. Kleruu. Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 inaeleza kuwa mtu anaweze kutumia utetezi wa kukasirishwa kwa matendo ya mtu mwengine ambayo yalichangia mtu huyo kutenda kosa kutokana na hasira hiyo ambapo hakupata muda wa kupoa hasira yake.

Tunaweza kuangalia sheria inavyoeleza kwa kina suala zima la utetezi wa kukasirishwa. Kifungu cha 201 cha Kanuni ya Adhabu kinaeleza zaidi:

‘When a person who unlawfully kills another under circumstances which, but for provisions of this section would constitute murder, does the act which causes death in the heat of passion caused by sudden provocation as defined in section 202, and before there is time for his passion to cool, he is guilty of manslaughter only’ Section 201 Penal Code [CAP 16. R.E.2022]

Kwa tafsiri ya kifungu hiki kwa lugha ya kiswahili

Pale ambapo mtu ambaye isivyokuwa halali anamuua mwengine katika mazingira ambayo kwa masharti ya kifungu hiki ingefanya kosa la kuua kwa kusudia, anatenda kitendo ambacho kinasababisha kifo akiwa katika hali ya joto la hasira iliyosababishwa na kukasirishwa kwa ghafla kama ilivyofafanuliwa katika kifungu cha 202, na kabla ya kuwepo muda wa hasira kupoa, ana hatia ya kuua bila kukusudia’ Kifungu 201 Kanuni ya Adhabu Sura ya 16.

Kanuni ya Adhabu inafafanua zaidi kuhusiana na neno kukasirishwa lina tafsiri gani kwa mujibu wa sheria. Kifungu cha 202 cha Kanuni ya Adhabu kinaeleza:

The term provocation means, except as hereinafter stated, any wrongful act or insult of such a nature as to be likely, when done to an ordinary person, or in the presence of an ordinary person to another person who is undet his immediate care, or to whom he stands in conjugal, parental, filian, or fraternal relation, or in the relation of master or servant, to deprive him of the power of self-control and to induce him to commit an assault of the kind which the person charged committed upon the person by whom the act or insult is done or offered’ Section 202 of the Penal Code [CAP 16 R.E.2022]

Tafsiri yake kwa Kiswahili inaweza kusomwa ifuatavyo:

‘Neno ‘kukasirishwa’ maana yake ni, isipokuwa kama itakavyoelezwa hapa chini, kitendo chochote cha maudhi au tusi la namna yoyote, ambayo akitendewa mtu wa kawaida au akitendewa mbele ya mtu wa kawaida kwa mtu mwengine aliyemo katika uangalizi wake halisi, au kwa mke, mume, mzazi, mwana, ndugu, mwajiri au mtumishi kwa kumsababishia asimudu kujizuia nafsi yake na kumshawishi kufanya shambulio kama alichofanya huyo mshtakiwa kwa mtu aliyetendewa kitendo hicho au aliyetukanwa’ Kifungu cha 202 Kanuni ya Adhabu.

Ufafanuzi

Kwa ufupi sheria ya Kanuni ya Adhabu inaeleza kuwa mtu anaweza kutumia utetezi wa kukasirishwa ‘provocation’ pale ambapo atatenda kosa ambalo linaweza kusababisha mauaji kwa mtu mwengine endapo aliyeuawa alimfanyia mshtakiwa kitendo au jambo lililoamsha hasira ya mshatakiwa kiasi kwamba alipoteza udhibiti wa matendo yake kutokana na kutukanwa huko au kufanyiwa kitendo kibaya yeye binafsi au mtu wa karibu yake ikiwa ni mwenzi, mzazi, mtoto, ndugu wa karibu au mwajiri wake au mtumishi wake.

Kutokana na simulizi yetu ya Saidi Mwamwindi, mshtakiwa aliwasilisha pia ushahidi wake na mashahidi wake kuwa vitendo vya marehemu Dr.Kleruu viliamsha hasira kali kwa Saidi Mwamwindi kiasi cha kufikia hatua ya kufanya mauaji yale. Swali ni je yale yaliyosadikiwa kufanywa na Dr. Kleruu yalijitosheleza kusababisha ‘hasira’ kwa Said Mwamwindi kiasi cha kufanya mauaji?

Endelea kufuatilia mfululizo wa makala hizi kuhusiana na Kisa Mkasa Mahakamani kuona Mahakama jinsi ilivyoweza kujibu hoja hii.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya barua pepe info@ulizasheria.co.tz

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako              

Isaack Zake, Wakili wa dunia (Global Advocate)