Kisa Mkasa 6: Mkulima (Said Mwamwindi) kufanya mauaji ya Mkuu wa Mkoa (Dr.Kleruu) – 2
Utangulizi
Karibu tena ndugu msomaji kwenye makala iliyopita ilituonesha utangulizi wa kisa hiki cha mauaji kilichojitokeza mwanzoni mwa 1970. Pia tumeweza kufahamu wasifu wa wahusika wakuu kwenye kisa hiki. Leo tunaendelea na mwendelezo wetu wa simulizi hii.
Siku ya tarehe 24/12/1971 aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dr.Kleruu alifanya ziara ya kutembelea mashamba mbalimbali maeneo ya Tarafani, Igulu na Ndolela katika harakati za kuhamasisha kilimo cha pamoja kwenye mashamba. Siku ya tukio hili ilikuwa 25/12/1971 sikukuu ya Krismas ambapo Dr.Kleruu majira ya saa 11 jioni alitembelea kwenye shamba la Said Mwamwindi aliyekuwa akiendelea na shughuli zake za shamba. Dr.Kleruu alifika eneo hilo akiwa peke yake bila viongozi wengine au askari wa kuambatana naye kwenye ziara. Shambani alikuweko Said Mwamwindi, mtoto wa Said (Mohamed) na wafanyakazi wawili (Yadi Chaula na Charles Mwamalata), mkwe wa Said (Joseph Kusava) na wake zake Said Mwamwindi.
Kwa ushahidi uliowasilishwa mahakamani Dr. Kleruu alipofika eneo la shamba la Said alimfuata moja kwa moja kwenye trekta alilokuwa anatumia kulima pale shambani. Mazungumzo yao yalikuwa kama ifuatavyo:
Dr.Kleruu – shuka. Uwongo shenzi
Mwamwindi – kwa nini bwana unanitukana, nimefanya nini?
Dr. Kleruu – funga mdomo wako. Ng’e – ng’e nini? Tazama nawaambia lakini hamsikii.
Mwamwindi – umeniambia nini?
Dr. Kleruu – Bloody fool
Wakati wa mazungumzo haya Dr.Kleruu alikuwa ana fimbo anayotembea nayo na akawa anamchomachoma nayo Mwamwindi wakati wanazungumza. Ilipofikia hatua hii Said aligeuka na kuanza kuondoka kuelekea kuelekea kwenye nyumba yake ili kuepusha makabiliano na Mkuu wa Mkoa. Hatahivyo, Mkuu wa Mkoa akawa anamfuata kwa nyuma.
Dr. Kleruu – tazama unaendelea kujenga nyumba za kudumu
Mwamwindi – hii sio nyumba ni mahali ninapozika ndugu zangu
Dr.Kleruu – ni mahali unapozika mirija(wanyonyaji) wenzio mbwa wee’
Ni baada ya maneno haya Said Mwamwindi analeza katika ushahidi wake kuwa alipoteza mwelekeo na hasira yake kupanda kiasi cha kuchukua hatua kuingia ndani kufuata silaha.
Ndugu msomaji leo tumeweza kuona hasa kile kilichotokea baina ya Said Mwamwindi na Dr.Kleruu kulingana na ushahidi uliowasilishwa mahakamani. Mazungumzo yao ambayo yalipelekea kisa hiki kutokea. Endelea kufuatilia mfululizo huu kujua zaidi.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.
Muhimu
Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya barua pepe info@ulizasheria.co.tz
‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’
Nakutakia siku njema.
Wako
Isaack Zake, Wakili wa dunia (Global Advocate)