Kisa Mkasa 4: Emmanuel Didas vs MOI

Utangulizi

Karibu tena ndugu msomaji kwenye mfululizo wa 4 wa simulizi ya kesi ya Emmanuel Didas vs MOI. Mpaka sasa tumeona jinsi mahakama kuu ilivyoweza kutoa ufafanuzi wa hoja kuu 2 katika kutatua mgogoro huu wa mdai kupata madhara kutokana na uzembe wa kitaaluma.

Leo tunakwenda kuangalia hoja ya 3 kuhusu nafuu (reliefs) za kifedha ambazo mdai anatakiwa kupata kutokana na madhara aliyopata. Karibu ndugu msomaji tuendelee.

Baada ya Mahakama Kuu kuthibitisha juu ya uwepo wa uzembe na madhara katika maeneo 10 tuliyojadili katika makala iliyopita.

Katika kutoa fidia kutokana na madhara yaliyojitokeza kwa mdai, Mahakama Kuu iliangalia maeneo mbalimbali ambayo mdai anaweza kuwa ameathirika na tukio hilo kama:

  • Gharama za matibabu
  • Kukosa kipato baada ya tukio na baada ya kesi
  • Gharama za matibabu kwa siku za baadae
  • Gharama za matunzo nyumbani kutokana na hali ya ugonjwa endelevu
  • Kupoteza fursa ya kufanya shughuli mdai anazopendelea
  • Gharama za kujikimu kimaisha nk

Mahakama Kuu kwa kufanya tathmini ya kipidi cha madhara tangu kufanyiwa upasuaji mpaka kukamilika matibabu ni kipindi cha miezi 21 na kulingana na kipato cha mdai kwa wakati huo Mahakama Kuu iliamuru mdai kulipwa kiasi cha Tsh.1,076,620/-

Mahakama Kuu halikadhalika ilifanya tathmini ya gharama za matunzo ya nyumbani atakayohitaji mdai kwa kipindi chote ambacho angekuwa anafanya kazi. Mdai alipata madhara akiwa na umri wa miaka 20 na alitegemewa kufanya kazi mpaka umri wa kustaafu wa miaka 60, hivyo Mahakama Kuu ilifanya hesabu ya miaka 40 ya kazi. Gharama za matunzo ambazo Mahakama ilitamka kufidia ni kiasi cha Tsh.10,600,000/-

Mahakama Kuu pia ilifanya tathmini ya fidia kutokana na maumivu ambayo mdai amepata na ataendelea kupata kuokana na makosa ya uzembe yaliyofanywa na mdaiwa na kuamua kutoa kiasi cha Tsh.88,323,380/-

Fidia zote ambazo Mahakama Kuu iliamuru mdaiwa kumlipa mdai kutokana na madhara yaliyosababishwa na mdaiwa ni Tsh.100,000,000/-

Ndugu msomaji leo tumeweza kuona fidia ambayo Mahakama Kuu iliamuru mdai kulipwa kutokana na madhara ambayo mdaiwa aliyafanya dhidi yake. Tukio hili ambalo lilitokea miaka kadhaa iliyopita kwa sehemu kubwa sana limesaida taasisi zetu za matibabu kuboresha mifumo ya huduma ili kuepuka makosa kama haya ambayo yanaweza kuleta madhara makubwa kwa wanaopokea huduma katika maeneo hayo. Inawezekana pia yapo mengine ambayo yanaendelea kujitokeza katika taasisi kama hizo, muhimu ni wewe kuchukua hatua stahiki endapo suala kama hili litajitokeza kwa lengo la kuzuia madhara kama haya kwa siku za baadae.

Nahitimisha mfululizo wa Kisa Mkasa Mahakamani kwa kesi ya Emmanuel Didas kwa kutoa pole kwake pamoja na na familia ya Emmanuel Mgaya. Usiache kufuatilia makala hizi za Kisa Mkasa Mahakamani ambapo tutaanza simulizi ya kesi nyingine tutakayopata mafunzo zaidi.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya barua pepe info@ulizasheria.co.tz

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako              

Isaack Zake, Wakili wa dunia (Global Advocate)