Kisa Mkasa 3: Emmanuel Didas vs MOI

Utangulizi

Makala iliyopita ilieleza juu ya Emmanuel Didas kufungua shauri Mahakama Kuu Kanda ya Dar Es Salaam kudai fidia kutokana na uzembe uliojitokeza na madai yaliyowasilishwa dhidi ya wadaiwa. Tuliona hoja kuu ambazo Mahakama ilizitumia katika kuamua shauri hili na kisha Mahakama kuthibitisha hoja ya kwanza muhimu kuhusiana na uzembe uliojitokeza mahakamani. Leo tunakwenda kuangalia hoja ya 2 endapo kulikuwa na madhara kwa Mdai kutokana na uzembe uliojitokeza. Karibu ndugu msomaji tuendelee.

Katika kujibu hoja ya kuwa endapo mdai Emmanuel Didas alipata madhara kwa vitendo vya uzembe vilivyosababishwa na watendaji wa wadaiwa mahakama ilithibitisha hoja hiyo kupitia ushahidi uliowasilishwa na mashahidi na vielelezo kadhaa. Vielelezo vilivyowasilishwa vilieleza wazi kuwa tangu tarehe 1/11/2007 mpaka 28/07/2008 Mdai alikuwa kwenye matibabu kwa wakati wote huo. Mahakama ilijiridhisha kuwa madhara yaliyojitokeza kutokana na makosa yaliyofanyika yalipelekea mdai kuathirika kama ifuatavyo:

  1. Kushindwa kuzungumza vizuri
  2. Kushindwa kuunganisha sentensi ndefu wakati wa kuzungumza
  3. Kushindwa kuzungumza mfululizo zaidi ya sekunde 30
  4. Kutoweza kukaa vizuri kwa kunyooka
  5. Anapokaa kuelemea upande mmoja wa kulia ambao ulionesha dalili za kupooza
  6. Kushindwa kufanya kazi
  7. Mguu uliofanyiwa upasuaji kwa kuchelewa bado haukupona vizuri
  8. Hawezi kukaa vizuri (unbalanced)
  9. Anatetemeka mguu wa kushoto pindi anapoongea
  10. Hawezi kujisimamia mwili wake vizuri

Kwamba kwa ushahidi ambao alitoa mdai mwenyewe alieleza kuwa kutoana na upasuaji huo anashindwa kujihudumia masuala ya kawaida ambayo mtu anategemea kujihudumia kama kuoga, kufua, kupika nk.

Hivyo, kwa hoja ya 2 Mahakama ilijiridhisha pasina shaka kuwa uzembe uliofanywa na wadaiwa ulisababisha madhara makubwa sana kwa mdai.

Ndugu msomaji leo tumeona juu ya madai yaliyowasilishwa na Emmanuel Didas dhidi ya MOI na hoja ya 2 kuthibitishwa mbele ya Mahakama. Endelea kufuatilia makala ijayo ya Kisa na Mkasa Mahakamani kuona ni nini Mahakama itaamua kutokana na kuthibitishwa kwa hoja namba 1 na 2.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya barua pepe info@ulizasheria.co.tz

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako              

Isaack Zake, Wakili wa dunia (Global Advocate)