Kisa Mkasa 2: Emmanuel Didas vs MOI

Utangulizi

Katika makala iliyopita tumeweza kuona sehemu ya kwanza ya Kisa cha Emmanuel Didas dhidi ya MOI (Hospitali ya Muhimbili kitengo cha mifupa) ambapo habari za wangonjwa kufanyiwa upasuaji tofauti na mazingira ya ugonjwa wao zilishtua hadhira kubwa ya Tanzania mwishoni mwa mwaka 2007. Makala iliyopita ilieleza juu ya Emmanuel Didas kufungua shauri Mahakama Kuu Kanda ya Dar Es Salaam kudai fidia kutokana na uzembe uliojitokeza. Karibu ndugu msomaji tuendelee.

Madai

Katika kuwasilisha madai yake kwenye hati ya madai mdai Emmanuel Didas aliiomba mahakama iamuru wadaiwa kulipa madai yafuatayo:

  1. Kiasi cha 9,125,000/- kama pato lililopotea kwa mwaka kuanzia Novemba 2009 na kiasi cha Tsh.25,000/- kwa kila siku baada ya hukumu
  2. Kiasi cha 150,000/- kwa mwezi tangu Oktoba 2010 mpaka siku ya hukumu
  3. Riba ya kimahakama kiasi cha 7% tangu siku ya hukumu mpaka kutekelezwa kwake; na
  4. Gharama za kesi

Mahakamani

Katika kutatua mgogoro ulio mbele yake Mahakama ilijielekeza katika kubaini mambo makuu 3

  • Endapo kulikuwa na uzembe wa kitaaluma uliofanywa na MOI  dhidi ya mdai Emmanuel Didas
  • Kama ni kweli kulikuwa na uzembe, je, mdai alipata madhara na uzembe huo
  • Ni nini haki wanazostahili kila upande

Mahakama katika kujibu hoja ya kwanza endapo kulikuwa na uzembe wa kitaaluma, ilijiridhisha kuhusiana na hilo kutokana na ushahidi uliotolewa na pande zote kwamba uzembe ulijitokeza pale makabrasha (files) ya wagonjwa hao yalipochanganywa. Kwamba kilichowachanganya wauguzi ni majina ya kwanza ya wagonjwa wote kuanza kwa Emmanuel hivyo nyaraka zao zikachanganywa. Hoja hii pia ilithibitishwa kutokana na taarifa ya kimatibabu ya Emmanuel Didas ambayo iliwasilishwa kama kielelezo. Halikadhalika kitendo cha Hospitali kuchukua hatua ya kumpeleka India kwa matibabu zaidi kilidhihirisha kuwa uzembe ulifanyika ndio maana walichukua jitihada zaidi kuhusiana na suala hilo.

Ndugu msomaji leo tumeona juu ya madai yaliyowasilishwa na Emmanuel Didas dhidi ya MOI na hoja kuu 3 ambazo Mahakama Kuu ilijikita katika kutatua mgogoro huu. Endelea kufuatilia makala ijayo ya Kisa na Mkasa Mahakamani kujifunza zaidi.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya barua pepe info@ulizasheria.co.tz

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako              

Isaack Zake, Wakili wa dunia (Global Advocate)