Kisa Mkasa 5: Mkulima (Said Mwamwindi) kufanya mauaji ya Mkuu wa Mkoa (Dr.Kleruu) – 1

Utangulizi

Karibu tena ndugu msomaji kwenye makala zetu za Kisa na Mkasa Mahakamani, leo hii tukianza simulizi ya kesi ambayo ilisisimua sana miaka ya 1970 kwa tukio kubwa lililojitokeza na habari zake kusambaa kwa kasi kubwa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Ilikuwa ni nyakati za kuenea kwa siasa ya ujamaa miaka 10 baada ya Tanganyika huru. Nchi nzima ilikuwa ikihimizwa katika kufanya mambo ya ujamaa na maeneo ya wengi yalitaifishwa ili kufanya shughuli za pamoja. Katikati ya harakati hizo za kisera katika nchi yetu lilijitokeza tukio kubwa sana ambalo katika medani za kisiasa, kijamii na kimahakama haliwezi kusahaulika. Tukio hili lilihusisha mauaji ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dr.Wibert Kleruu yaliyofanywa na Said Abdallah Siulanga Mwamwindi mnamo tarehe 25/12/1971.

Wasifu wa Dr. Kleruu

Dr. Kleruu alikuwa ni mmoja kati ya wasomi wachache sana waliofikia ngazi ya shahada ya Uzamivu (Phd) katika masuala ya uchumi wa kijamaa. Alifanya kazi na kuaminiwa katika nafasi ya Mkuu wa Mkoa huko Mtwara na baadae kupata uamisho kwenda kueneza shughuli za ujamaa katika Mkoa wa Iringa. Hulka yake na namna ya uongozi wake alikuwa ni mtu wa amri na kupendelea kufanya kazi wakati wote kueneza kwa vitendo siasa ya ujamaa. Walioshuhudia nyakati zake walieleza juu ya utendaji wake na ushiriki wake wa shughuli mashambani pamoja na wananchi. Alisifika kwa bidii, uchapa kazi na hata ukali wake.

Wasifu wa Said Mwamwindi

Historia yake inaonesha alikuwa na shughuli za udereva kabla ya mwaka 1954 na ilipofika 1954 aliachana na shughuli za udereva na kuhamia eneo la Mkunguu, Isimani na kuanza shughuli za kilimo. Kwamba alikuwa na maeneo madogo lakini kwa bidii yake aliweza kusafisha pori na kuwa na shamba la ukubwa wa takribani ekari 160. Alikuwa akilima kisasa na kuwa na wafanyakazi wa shambani.

Tangazo la Sera ya Ujamaa

Dr, Kleruu alipofika Iringa kama mkuu wa mkoa alitangaza mpango wa serikali juu ya kuyafanya mashamba yote kuwa ya ujamaa. Kwamba alitoa muda kuwa kufikia Novemba 1971 basi mashamba yote binafsi yanapaswa kuwa ya ujamaa. Hili ni tangazo ambalo pia lilitishia maslahi ya Said Mwamwindi ambaye alianza kidogo na kwa juhudi zake aliweze kufikia kuwa mmoja wa wamiliki wa mashamba makubwa katika eneo la Mkungugu.

Ndugu msomaji leo tumeweza kuona tu utangulizi wa simulizi hii ya kesi hii iliyovuta hisia za watu wengi sana nchini Tanzania. Tumeona historia za wahusika kila mmoja na historia yake kwa usimamizi wa kile alichoamini. Je, ni nini kitatokea baina ya watu hawa wawili? Usikose kufuatilia kisa hiki uendelee kujifunza zaidi.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya barua pepe info@ulizasheria.co.tz

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako              

Isaack Zake, Wakili wa dunia (Global Advocate)