Kisa Mkasa 7: Mkulima (Said Mwamwindi) kufanya mauaji ya Mkuu wa Mkoa (Dr.Kleruu) – 3

Utangulizi

Karibu tena ndugu msomaji kwenye makala iliyopita tuliweza kuona kile kilichotokea pale shambani kwa Said Mwamwindi kuhusiana na majibizano baina yake na Dr.Kleruu. Ni kitu gani kilifuata baada ya majibizano haya. Fuatana nami kwenye simulizi hii.

Mara baada ya majibizano kati ya Dr.Kleruu na Said Mwamwindi, Said aliingia ndani na kutoka na gobole kisha kufyetua risasi 2 ambazo zilikatisha uhai wa Dr.Kleruu kisha akamwita mtoto wake Mohamed kuja kuubeba mwili na kuupakia kwenye gari alilokuja nalo Mkuu wa Mkoa, kisha akaliendesha gari hilo mpaka kituo cha polisi na kujisalimisha mwenyewe.

Utetezi wa Kurukwa Akili (Defense of Insanity)

Moja ya hoja zilizoletwa Mahakama Kuu kuhusiana na utetezi wa Said Mwamwindi ni kuwa katika kipindi anatenda tukio hilo hakuwa katika akili timamu ‘defense of insanity’. Katika mashauri ya kijinai mtu anaweza kuondolewa hatia kama ametenda kosa wakati hakuwa na akili timamu.

Mashahidi wa utetezi waliwasilisha ushahidi kuwa Mtuhumiwa aliwahi kuwa na ugonjwa wa akili ambao uligundulika mwaka 1958 na kwamba alikuwa akipata matibabu. Utetezi huo uliwasilishwa na shahidi – 7 Zula binti Feruzi (mama mzazi wa Said Mwamwindi). Ushahidi huu pia ulielezewa  kwa kirefu na Dr.Pendaeli aliyemchunguza mtuhumiwa katika kituo cha Isanga Mental Institution mnamo Septemba 1972. Kwamba Dr.Pendaeli alithibitisha kuwa mtuhumiwa aliwahi kuwa na ugonjwa wa akili unaoitwa CATATONIC SCHIZOPHRENLA. Ugonjwa huu unaweza kumfanya mtu kuwa mwenye hasira, fujo kwa upande mmoja na anaweza kuwa mpole sana, hajigusi, hali wala haongei kwa muda. Dalili zote hizi ziliwahi kumpata Said Mwamwindi mnamo mwaka 1958. Hatahivyo, katika kufikia hitimisho la ushahidi wake, Dr.Pendaeli alieleza kuwa kipindi Said Mwamwindi anatekeleza tukio la mauaji hakuwa katika athari za ugonjwa huo wa akili.

Mahakama Kuu katika kuamua endapo utetezi kuhusiana na mtuhumiwa kurukwa na akili wakati akitenda kosa inaangalia masuala kadhaa:

  • Historia ya familia ya mtuhumiwa
  • Historia binafsi ya mtuhumiwa
  • Mazingira yanayozunguka tukio lenyewe la jinai
  • Ushauri wa kitaalam kutoka kwa Daktari

Katika kufanya uamuzi endapo mtuhumiwa alikuwa katika hali ya kurukwa na akili wakati wa kutenda kosa la mauaji, mahakama iliangalia vipengele vyote ikiwa ni pamoja na maelezo ya mtuhumiwa aliyoyatoa tarehe 26/12/1971 chini ya mlinzi wa amani kuwa alieleza kwa kina jinsi tukio zima lilivyotokea, tangu kuwasili kwa Dr.Kleruu, majibizano waliyokuwa nayo, matusi aliyotukanwa, jinsi alivyoingia ndani kuchukua bunduki, alivyomwita mtoto wake kumsaidia kuweka mwili kwenye gari, alivyoendesha gari mpaka kituo cha polisi na kujisalimisha nk.

Mahakama Kuu kwa kuzingatia ushahidi wote uliotolewa na upande wa utetezi, ilitupilia mbali hoja ya utetezi kuwa mtuhumiwa wakati anatenda kosa hili kwamba alikuwa amerukwa na akili.

Ndugu msomaji leo tumeona hoja mojawapo ya utetezi ya kuwa mtuhumiwa wakati anatenda kosa alikuwa amerukwa na akili. Mahakama iliitupilia mbali hoja hii. Je, Said Mwamwindi alikuwa na hoja nyingine ya utetezi? Endelea kufuatilia mfululizo huu kujua zaidi.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya barua pepe info@ulizasheria.co.tz

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako              

Isaack Zake, Wakili wa dunia (Global Advocate)