Sheria Leo.132. Ufanye nini unapozungushwa kupewa hukumu ya kesi yako?

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Leo kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku.

Kwa muda mrefu nimekuwa nikipokea maswali ya wasomaji na wadau wengi kuhusiana na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika mahakama. Changamoto hizi zimekuwa nyingi sana kiasi kwamba zinaibua hisia za watu kutokutendewa haki. Leo tunaenda kuangalia changamoto mojawapo ambayo nimekuwa nikiwajibu wasomaji wetu. Karibu tujifunze.

Je, ufanye nini unapozungushwa kupewa hukumu ya kesi yako?

Nimepokea jumbe kadhaa na simu za wadau wakiwa wanalalamika sana kuhusiana na kutokupatiwa hukumu au nakala ya hukumu kutokutolewa kwa wakati. Nimeona nitoe ufafanuzi katika makala hii ili iweze kukusaidia na wewe mdau katika kufuatilia haki yako ukiwa mahakamani.

Kama ilivyo kawaida tunatarajia kesi yoyote au mashitaka yoyote iwe ya madai au jinai huwa na kikomo. Hii ina maana kesi inapaswa kufunguliwa kisha kusikilizwa na hatimaye hukumu kutolewa mbele ya wadaawa. Hatahivyo, kumeibuka mtindo wa baadhi ya wahusika kuchelewesha hukumu au kutokutoa nakala za hukumu kama inavyopaswa. Kuna wakati kesi imemalizwa kusikilizwa muda mrefu lakini hukumu haisomwi kwa wakati.

Nimepata malalamiko kwa baadhi ya watu wanapewa tarehe za mbali ikiwezekana hadi Jumamosi na kutokupata majibu yanayojitosheleza kuhusiana na maamuzi ya kesi zao.

Kitu muhimu unachopaswa kufahamu ni kuwa uamuzi wa shauri au kesi yako ni haki yako na unapaswa kutolewa mapema kadri iwezekanavyo. Kuna baadhi ya watendaji wanatoa uamuzi kwa kificho kutokana na sababu zao ili mdaawa aliyeathiriwa na maamuzi asiweze kukata rufaa ndani ya wakati. Jambo hili si sawa na halipaswi kufumbiwa macho.

Hatua unazoweza kuchukua endapo uamuzi wa kesi unacheleweshwa au umetolewa lakini hujapata nakala yake;-

 • Andika barua ya kuulizia endapo uamuzi au hukumu ya kesi yako imeshasomwa
 • Endapo umesomwa na ulikuwepo mahakamani, pia andika barua kuomba kupatiwa nakala yako na nakala ya mwenendo wa shauri lako.
 • Endapo uamuzi utaendelea kuchelewa au kutokupewa nakala ya uamuzi basi andika barua kukumbushia na ambatanisha nakala ya barua kwa mahakama ya juu inayosimamia mahakama ambayo inapaswa kukupa uamuzi wako.

Watu wengi huishia kulalamika au kudai uamuzi kwa maneno kiasi kwamba siku wanaupata mkononi wanaonekana wamechelewa kuchukua hatua kama za kukata rufaa au kuomba marejeo katika ngazi ya juu. Lakini ukichukua hatua ya kuandika barua inakusaidia kuwa sababu ya msingi ya kukata rufaa katika ngazi inafuata.

Usiogope kufuatilia haki yako ya uamuzi au hukumu ya kesi inayokuhusu, hofu yako inaweza kupelekea kupoteza haki yako na uhuru wako.

 ‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040  na email zakejr@gmail.com

Sheria Leo.130. Je, Unamshtaki Nani?

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Leo kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunajiuliza swali muhimu sana katika masuala ya mashauri ya mahakamani Je, unamshtaki nani?. Karibu tujifunze.

Mfumo wa Mashauri

Katika suala la kudai haki mahali au kwa mtu fulani, mara nyingi mchakato unaohusisha kwenda katika vyombo vya maamuzi haukwepeki yaani mahakama. Mfumo wetu wa kudai na kutoa haki unasimamiwa na Mhimili wa Dola unaoitwa Mahakama. Kazi kubwa ya mahakama ni kusikiliza mashauri mbali mbali na kutoa tafsiri sahihi ya sheria kama zilivyotungwa na Bunge.

Pande mbili zinazotafuta au kudai haki mbele ya mahakama zinatarajiwa kuleta hoja na ushahidi wa kusaidia ushindi au kupata haki wanayostahili. Ni wajibu wa kila upande kujiandaa na kujipanga endapo unashitaki au kushtakiwa, mahakama haina upande wowote bali kazi yake ni kuangalia ni upande gani una haki kisheria.

Je, unamshtaki nani?

Nieleze kisa kimoja ambapo mwananchi mmoja alifanya kesi kwa takribani miaka 3 na kushinda kesi husika dhidi ya mdaiwa wake. Hata hivyo mara baada ya kupata ushindi wa kesi hiyo, utekelezaji wa amri ya mahakama ulishindikana kwa sababu majina halisi ya mdaiwa na yale yaliyowasilishwa kwenye hati ya madai yalitofautiana.

Hiki ni kisa kimoja tu, miongoni mwa visa hivi vinavyotokea mahakamani kila siku.

Mojawapo ya vigezo vikubwa sana katika uendeshaji wa mashauri mahakamani ni kuhakikisha unamshitaki mtu sahihi na si vinginevyo. Watu wengi, hata wajuzi wa sheria huwa wanapata changamoto hii ya kushindwa kumshitaki mtu au taasisi sahihi. Umakini mkubwa unahitajika pale ambapo umefikia hatua ya kufungua shauri mahakamani kwa lengo la kudai haki yako.

Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai inamtaka mlalamikaji anayefungua shauri kuhakikisha anafungua shauri dhidi ya mdaiwa kwa majina yake halali ya kisheria.

Kesi nyingi na madai mengi ya wadai yameshindwa mahakamani kwa sababu mdai hakufanya kazi yake ya msingi kujua majina halisi ya mdaiwa. Ni muhimu sana ukiwa mdai kuhakikisha ya kwamba unamdai au kumshtaki mtu sahihi au taasisi sahihi kwa majina sahihi ili uweze kupata haki yako.

Msisitizo huu tunaweza kuuona katika shauri la rufaa lililofanyika mahakama ya rufaa baina ya CHRISTINA MRIMI na COCA COLA KWANZA BOTTLES LTD, rufaa  Na.112 of 2008, ambapo Mahakama ya Rufaa ilieleza yafuatayo, ninukuu kwa lugha ya kiingereza

 

‘Companies, like human beings, have to have names. They are known and differentiated by their registered names. In the instant case, it is apparent that the names ‘Coca Cola Kwanza Bottles’ Coca Cola Kwanza Ltd’ or ‘Coca Cola Bottlers Ltd’ have been used inter changeably. Although the Appellant wants this Court to hold that they mean one and the same Company, strictly, this view cannot be accepted without same risk of inexactitude.’

 

Tafsiri isiyo rasmi inasema

 

Kampuni ni kama wanadamu, zina majina na zinajulikana na kutofautishwa kwa majina katika kesi ya sasa majina kama Coca Cola Kwanza Bottles’ Coca Cola Kwanza Ltd’ au ‘Coca Cola Bottlers Ltd’ yamekuwa yakitumiwa mara kwa mara. Ingawa mrufani anataka mahakama hii iseme kuwa majina haya yote yanamaanisha ni kampuni moja, mtazamo huu hauwezi kukubalika bila kuleta athari kubwa’

Kisheria kumshitaki mtu anayeitwa JOHN JOSEPH JOHN na JOSEPH JOHN JOSEPH ni watu wawili tofauti.

Hitimisho

Ni muhimu sana kwako mdai mara zote kuhakikisha kuwa unamshitaki mdaiwa kwa majina yake sahihi. Tumeona mifano ya watu wengi wakikosa haki au haki yao ikichelewa kutokana na kukosea au kutokufanya utafiti wa kutosha juu ya yule anayetakiwa kushtakiwa.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 au 0787 466 687 na email zakejr@gmail.com

 

 

Sheria Leo.129. Upi ni ukomo wa mashauri ya Ardhi?

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Leo kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunajibu swali la msomaji wetu kuhusiana na suala la umiliki na ukomo wa mashauri ya ardhi. Karibu tujifunze.

Swali la msomaji wetu

Tunapokea maswali mengi sana kutoka kwa wasomaji wetu na tunapasa muda wa kuwashauri na kuchukua hatua zinazostahili. Leo tunakushirikisha swali mojawapo la msomaji wetu linalosema

‘Familia yetu ilisafisha eneo la ekari 10 na kuanza kilimo mnamo mwaka 1994. Tumeendelea kulitunza shamba hilo na kupanda mazao ya muda na miti ya kudumu kwa kipindi chote. Utaratibu wa kumilikishwa ardhi na Kijiji ulituwezesha kupata hati ya kijiji mwaka 2017 baada ya kukidhi masharti yote. Hivyo tumekuwa na umiliki wa eneo hili kwa muda wa miaka 24 sasa. Wamejitokeza watu wakidai kuwa eneo hilo ni lao, na kwamba mara ya mwisho waliacha kulima mwaka 1995. Je, sheria inasemaje katika suala kama hili? Hamis – Dodoma

Njia za Umiliki wa Ardhi

Swali hili la msomaji wetu limejikita katika maeneo mawili ya kuonesha juu ya umiliki wa ardhi. Maeneo haya tuliyajadili katika Sheria Leo.81. Utaratibu wa Umiliki wa Ardhi kwa njia ya Kusafisha Eneo na Sheria Leo.82. Utaratibu wa Umiliki wa Ardhi kwa njia ya Uvamizi kwa ufafanuzi zaidi unaweza kurejea kuzisoma makala hizo.

Sheria ya Ardhi inatambua umiliki kwa njia ya

 • Kusafisha eneo au pori
 • Kumiliki ardhi kwa njia ya uvamizi

Umiliki wa ndugu yetu muuliza swali unaweza kuangukia katika maeneo haya mawili yaani kusafisha eneo au uvamizi. Mtu anaweza kumiliki ardhi akisafisha eneo na kuendelea kulitumia kwa muda mrefu kiasi kwamba jamii na majirani anaopakana nao wakatambua kuwa yeye ni mmiliki halali.

Hali kadhalika mtu anaweza kumiliki kwa njia ya uvamizi ‘adverse possession’ wa eneo kwa muda mrefu pasipo kuingiliwa na mmiliki wa awali katika kipindi kisichopungua miaka 12 mfululizo.

Ni wazi kuwa familia husika imekuwa ikimiliki eneo husika kwa kipindi kisichopungua miaka 20 mfululizo na kuthibitisha kutokana na shughuli za maendeleo zilizofanyika katika eneo hilo. Hoja inayotoka kwa upande unaodai eneo ni lao tangu mwaka 1995 inapaswa iambatane na ushahidi wa juu ya matumizi au maendeleo yaliyofanyika katika eneo husika.

Sheria inaeleza wazi kuwa kama mtu amemiliki au amekuwa akiitumia ardhi kwa shughuli mbalimbali mfululizo kwa miaka isiyopungua 12 pasipo kuingiliwa na aliyekuwa mmiliki basi eneo hilo linakuwa ni halali kwa yule anayemiliki kwa sasa.

Pia ifahamike kuwa masuala ya ardhi yana ukomo wa muda wa kuwasilisha mashauri mahakamani. Endapo eneo lako limevamiwa au kuchukuliwa na mtu unapaswa kuchukua hatua za kisheria ndani ya miaka 12. Kushindwa kwako kuchukua hatua za kisheria katika kipindi hicho, ni dhahiri kuwa unazuiwa kisheria kudai haki katika eneo hilo kutokana na kuwa nje ya muda wa kisheria.

Hivyo, hoja ya msingi ambayo wadai wanapaswa kuiwasilisha ni kujieleza walikuwa wapi miaka yote 24 wasichukue hatua siku zote hizo?

 

Hitimisho

Ni rai yangu kwa wananchi wote hasa wa maeneo ya mijini au vijijini kupata uhalali wa umiliki wa maeneo yao. Lipo wimbi kubwa la watu wasio waaminifu na kwa kutumia watendaji wasio waadilifu wanaweza kupotosha haki ya mtu. Ni vyema kuzifahamu sheria na kuzifuata. Pia wananchi wasitelekeze maeneo na mara baada ya kuona hali ya kimaendeleo imebadilika wanarudi kutaka kudhulumu walioyafanyia kazi kwa muda mrefu.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 au 0787 466 687 na email zakejr@gmail.com

 

Sheria Leo.128. Mauzo ya Mali za Mirathi

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Leo kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunajifunza juu ya mauzo ya mali za mirathi. Karibu tujifunze kwa pamoja.

Mali za Mirathi

Katika masuala ya usimamizi wa mirathi, eneo la mali ndilo linaibua changamoto kubwa sana ndani ya familia na jamii kwa ujumla. Iwapo marehemu aliacha mali basi wanaohusika na wasiohusika watajitahidi kuweka mazingira ya kunufaika na mali za marehemu huku wakiacha majonzi na kilio kwa warithi halali.

Katika makala ya leo tungependa kuangazia mojawapo ya swali ambalo tumelipokea kutoka kwa wasomaji wetu linalosema

Nini kinaweza kufanyika kisheria, endapo mmojawapo wa warithi au ndugu wa marehemu anauza mali za marehemu pasipo kuteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi?

Hali hii imekuwa ikijitokeza mara kwa mara kwenye familia zetu za kiafrika ambazo nyingi hazina utaratibu wa kuandika wosia au kuweka mambo ya mali kisheria ili warithi wasije kubugudhiwa na ndugu au jamaa au marafiki.

Ipo mifano mingi kwenye jamii zetu mara baada ya mtu kufariki, ghafla mali zake zinaanza kuuzwa na wengine wanaanza kujichukulia kwa kadri wanavyoweza.

Ni muhimu kufahamu msimamo wa kisheria juu ya mali zilizoachwa na marehemu kuwa haziwezi kugawiwa au kuuzwa au kukodishwa  isipokuwa msimamizi wa mirathi amependekezwa na familia na kudhibitishwa na mahakama.

Hivyobasi, mauzo au namna yoyote ambayo mtu au mrithi anayofanya na mali ya marehemu bila kuteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi ni BATILI.

Maana ya ubatili wa mauzo haya ni kama vile hayajawahi kufanyika kabisa.

Hatua za kuchukua

Endapo wewe ni mrithi au mwathiriwa wa vitendo vya ndugu au mrithi mwenzako kuuza mali za marehemu pasipo kuwa na usimamizi wa mirathi basi chukua hatua zifuatazo;

 1. Itisha kikao cha familia au ukoo mara moja

Hii ni hatua ya kwanza ambayo unaweza kufanya endapo marehemu aliacha mali pasipo wosia. Itisha kikao cha wanandungu na kupendekeza majina ya wasimamizi wa mali ya marehemu. Katika kikao hicho kitaonesha wajumbe na hata mali za marehemu na uandaliwe muhtasari wa kikao husika.

 1. Fungua shauri la mirathi

Mara baada ya kuitishwa kikao cha wanandugu, fungua shauri la kuteuliwa msimamizi wa mirathi katika mahakama ya mwanzo mahali alipokuwa akiishi marehemu. Sheria za Mirathi zinataka utaratibu wa mtu kuteuliwa usimamizi wa mirathi udhibitishwe na mahakama kisheria. Wengi wanaishia kuteuliwa na kikao cha kifamilia na kuanza majukumu ya usimamizi wa mirathi, hii ni kinyume cha sheria na yote anayofanya msimamizi pasipo kuidhinishwa na mahakama ni batili kisheria.

Unapofungua shauri la mirathi utaorodhesha mali zote za marehemu ikiwa ni pamoja na zile ambazo zimeuzwa au zimekodishwa mara baada ya marehemu kufariki na kabla ya uteuzi wa usimamizi wa mirathi.

 1. Fungua shauri dhidi ya muuzaji na wanunuzi wa mali ya mirathi kwenye mahakama husika

Mara baada ya kuteuliwa usimamizi wa mirathi, na kuidhinishwa na mahakama, msimamizi anakuwa na uhalali wa kisheria kuhusiana na mali zote za marehemu. Msimamizi anaweza kufungua mashauri ya madai dhidi ya mtu aliyeuza mali za marehemu pamoja na walionunua. Lazima ifahamike kuwa wajibu mkubwa alionao msimamizi wa mirathi ni kukusanya mali za marehemu, kulipa madeni na kugawa kwa warithi halali. Katika kukusanya mali za marehemu, msimamizi anao wajibu wa kufuatilia kila mali ya marehemu ikiwezekana kufungua mashauri ya kisheria dhidi ya mtu yeyote au taasisi yoyote iliyouza mali au kununua mali ya marehemu.

 1. Fungua shitaka la jinai dhidi ya muuzaji

Msimamizi anayo haki na wajibu wa kufungua hata mashitaka ya kijinai dhidi ya muuzaji au mtu aliyejipatia mali za marehemu kwa njia za udanganyifu. Kisheria msimamizi wa mirathi anasimama katika miguu ya marehemu hivyo matendo yake yanahesabika kama ni matendo ya marehemu yaani anafanya kwa niaba yake. Hivyo anatarajiwa kuilinda mali ya marehemu kama vile marehemu angefanya mwenyewe.

Hitimisho

Ni muhimu sana kwa watu wote na jamii kuzingatia na kujiepusha kujinufaisha na mali za marehemu pasipo kuzingatia utaratibu wa kisheria. Ni rai yangu kwa wanunuzi wa viwanja, mashamba, au magari au mashine mbalimbali zinazohusishwa na mirathi kuwa makini. Ni lazima ujiridhishe uhalali wa muuzaji endapo ni msimamizi halali na anacho kibali cha kisheria kufanya mauzo au kuingia makubaliano ambayo mnataka kuingia, kinyume na hapo ni hasara mbele endapo sheria itachukua mkondo wake.

Nitoe rai kwa wale waathiriwa wa matendo ya watu wasio waaminifu katika mali za marehemu, kuchukua hatua kama nilivyopendekeza katika makala hii. Hatahivyo, ni vyema kwetu wote kwa kuwa ni ‘marehemu watarajiwa’ kuchukua hatua ya kuandika wosia ili warithi wetu wasikumbwe na changamoto husika.

‘Andika wosia sasa, maadam unaishi leo’

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

 ‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na uwakilishi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 au 0787 466 687 na email zakejr@gmail.com

 

 

Sheria Leo.127. Hatua za Kuchukua dhidi ya Ukatili kwenye Mahusiano

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa makala za Sheria Leo ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Tumejifunza kwa muda mrefu juu ya makosa mbali mbali na namna ya kisheria kosa linavyotokea kwa kitendo na dhamira. Katika makala iliyopita tuliangalia ‘Kwa nini watu husita kuchukua hatua dhidi ya ukatili kwenye mahusiano?. Leo tutaangalia ‘Hatua za Kuchukua dhidi ya Ukatili kwenye Mahusiano’

Karibu tujifunze.

 Ukatili/Vipigo kwenye Mahusiano ni Kosa Kisheria

Ni muhimu kufahamu kuwa vitendo vyovyote vya kuonesha ukatili au kumpiga mwenzi katika mahusiano ni kosa la kijinai. Tumeeleza wazi mwanzo kuwa jinai ni makosa yanayoshtakiwa na Jamhuri dhidi ya mtuhumiwa na ukipatikana na hatia basi unaweza kufungwa jela. Hivyo ni vyema pande zote zikatambua kuwa vitendo vya kupiga mwengine au ukatili katika mahusiano ni makosa ambayo pande zote yaani mwathiriwa na mtendaji ukatili wanapaswa kufahamu.

‘Kifungu cha 66 cha Sheria ya Ndoa ya 1971 kinaeleza wazi kuwa hakuna mwenye haki ya kumwadhibu mwenzi wake kwa vipigo au adhabu ya viboko bila kujali tamaduni au mila za eneo husika au asili ya wanandoa hao’

Kuna wengine wanachukulia suala la kumwadhibu mume au mke ni jambo la kimila au kitamaduni, Sheria hii imeweka wazi kuwa kitendo hicho hakiruhusiwi na ni kosa kisheria.

Katika makala hii ya leo tunaenda kuangalia baadhi ya hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa na mwathiriwa au jamii kwa lengo la kupunguza au kukomesha vitendo hivi vya ukatili au vipigo kwenye mahusiano.

Kumekuwa na changamoto kubwa kwa waathiriwa wa vitendo vya unyanyasaji kutokujua hatua za kuchukua au wapi pa kupeleka malalamiko yao. Wengi huishia kuumia au kuwaambia ndugu, jamaa na marafiki ambao hawatoi msaada wowote zaidi ya kuwaambia ‘wavumilie’. Katika makala ya leo tutakuonesha baadhi ya maeneo yanayoweza kushughulikia masuala haya na kupata suluhu ya kudumu.

 1. Kutoa taarifa katika baraza la usuluhishi la ndoa la Kata

Sheria ya Ndoa ya 1971 inaeleza juu ya uundwaji wa mabaraza ya usuluhishi ya masuala ya ndoa katika kila Kata. Wanandoa wengi hawafahamu uwepo wa mabaraza haya. Ni muhimu linapojitokeza tatizo lolote kuchukua hatua na kutoa taarifa kwenye baraza la usuluhishi wa ndoa nao watachukua hatua za kumwita mwenzi huyo kuweza kupata suluhu. Hii itasaidia hata kwa baadae na kukulinda dhidi ya mashambulizi mengine.

 1. Kutoa taarifa kwa Taasisi ya Kidini

Hili ni eneo lingine ambalo kutokana na changamoto hizi unaweza kutumia kwa ajili ya kutafuta suluhu. Tunafahamu ndoa nyingi zinafungwa na viongozi wa kidini. Ni dhahiri wana mchango mkubwa wa kuweza kuleta amani na ustawi wa ndoa au mahusiano husika endapo kutajitokeza tofauti baina ya pande mbili. Tumia fursa hii vizuri ya kuweza kutafuta suluhu baina yako na mwenzi wako endapo kutaanza kujionesha matukio ya ukatili au vipigo.

 1. Ofisi ya Ustawi wa Jamii

Ofisi za ustawi wa jamii zipo katika kila Kata, hivyo ni nafasi nzuri ya kuweza kuwasilisha malalamiko yoyote yanayohusiana na manyanyaso kwenye uhusiano wako na mwenzi wako. Ofisa wa ustawi atachukua hatua za kumwita mwenzi wako ili kuweza kuzungumza tofauti zilizopo na kufikia mwafaka wa tatizo lenu.

 1. Dawati la Jinsia katika Vituo vya Polisi

Kutokana na wingi wa matukio ya unyanyasaji unaoendelea katika familia, Serikali kupitia Jeshi la Polisi lilianzisha dawati maalum la jinsia. Dawati hili lnajishughulisha na maswala yanayojitokeza katika familia kama ya unyanyasaji, vipigo n.k. kama hali katika mahusiano yenu imezidi kuwa mbaya na mwenzi wako haonekani kubadili mwenendo wake basi chukua hatua ya kutoa taarifa katika kituo cha Polisi nao watakuelekeza kufuata utaratibu wa kushughulikia malalamiko hayo kupitia dawati la jinsia.

Linapokuja suala la mtu kumshtaki mwenzi wake kituo cha Polisi linahamsha ukakasi sana kwenye jamii na kuona kama vile anayeshtaki hamtakii mema mwenzi wake, hatahivyo jamii yetu imekuwa nzito sana kuchukua hatua kumsaidia mwathiriwa kabla hali yake kuwa mbaya. Hivyo kama tungependa hali hii isiendelee basi ni muhimu kuwasaidia mapema.

Hitimisho

Hofu kubwa inatawala jamii yetu kwa kufumbia macho vitendo hivi hasa wale wanaoathiriwa na ukatili huu na unyanyasaji katika mahusiano. Wengine wanahofu kuwa wakieleza yanayowasibu basi mateso yataongezeka. Hatuna sababu ya kuwa na hofu kwani hata watesi hao wana hofu kubwa kuliko wewe mwathiriwa kwamba ikitokea amejulikana na jamii kile anachokitenda hatokuwa na ujasiri wa kufanya hivyo mbele ya jamii. Tuchukue hatua kuepusha majanga na mauaji ya kutisha yanayotokea kila leo, kukaa kwetu kimywa kunaweza hali hii kututokea na sisi pia. Hakuna aliye salama kwa kukaa kimya.

Usikubali kuwa sehemu ya jamii inayonyamazia vitendo vya ukatili katika mahusiano bali chukua hatua sahihi ndani ya wakati

Kumbuka kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail ulizasheria@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms 0787 466 687.

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili

 

Sheria Leo.126. Kwa Nini watu hawachukui hatua dhidi ya Ukatili kwenye Mahusiano?

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa makala za Sheria Leo ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Tumejifunza kwa muda mrefu juu ya makosa mbali mbali na namna ya kisheria kosa linavyotokea kwa kitendo na dhamira. Katika makala iliyopita tuliangalia juu ya Ulinzi wa Kisheria dhidi ya Ukatili kwenye Mahusiano. Leo tutajifunza ‘Kwa nini watu husita kuchukua hatua dhidi ya ukatili kwenye mahusiano’.

Karibu tujifunze.

Kusita Kuchukua Hatua

Kumekuwa na dhana ya muda mrefu ndani ya jamii kutokuwa wazi kuhusuana na ukatili unaoendelea katika mahusiano. Wengi wao wanaona si jambo la kiungwana kueleza juu ya hali wanazopitia ndani ya mahusiano hasa masuala ya manyanyaso na vipigo vya mara kwa mara. Wengine wameenda mbali kuona ni suala la kitamaduni na linalohitaji uvumilivu. Zimekuwepo sababu nyingi za kuwafanya waathiriwa kutochukua hatua kukomesha au kuondoa tatizo hili. Sababu hizo ni pamoja na;

 1. Aibu au fedheha kwa jamii

Wanamahusiano wengi wanaogopa kuchukua hatua dhidi ya ukatili au vipigo ndani ya mahusiano kwa hofu ya fedheha kwa jamii. Wanajiuliza kuwa wataonekana vipi mbele ya jamii. Je, jamii itawachukulia vipi juu ya uhusiano wao. Hii si sababu ya msingi kwani ulinzi wa maisha yako ni jukumu lako la kwanza. Aibu hii na hofu hii imewaponza wengi na kusababishiwa ulemavu na hata kupelekea kifo. Kama wangepata ujasiri wa kusema basi madhara zaidi yangeepukwa.

 1. Kutoonekana mvumilivu wa maisha ya mahusiano au ndoa

Kuna msemo usemao kuwa ndoa ni uvumilivu au mahusiano ni uvumilivu. Ni kweli yapo mazingira katika mahusiano yanahitaji kuvumilia. Ni lazima tujue kilichowaunganisha watu wawili mwanzo ni upendo. Upendo ukiondoka na uvumilivu hupungua au kutoweka kabisa. Ielewe yapo yanayovumilika ila si vipigo na kuharibu maisha ya wengine kwa kigezo cha kuvumiliwa.

 1. Sababu za kiuchumi

Hii pia imekuwa sababu ya watu kutochukua hatua au kusita kuchukua hatua dhidi ya unyanyasaji au ukatili katika mahusiano. Inawezekana mmoja katika mahusiano ana uwezo wa kiuchumi na ndiye anahusika na mahitaji yote na kwa kigezo hiki anakitumia dhidi ya mwengine. Lazima turudie kuwa uhai au afya ya mtu ni muhimu na inapaswa kupewa kipaombele kabla ya vingine. Hili ni suala la kifikra tu na kujiuliza je mahitaji ya kiuchumi yana nafasi kubwa kuliko afya na uhai wako au la?

 1. Sababu za watoto

Watoto wamekuwa wakitumiwa kama sababu ya kuficha unyanyasaji na ukatili kwenye mahusiano. Wengi wanahofu kuchukua hatua ya kuzuia au kuondoa hali hii kwa sababu ya watoto. Anajiuliza itakuwaje juu ya malezi ya watoto endapo uhusiano huu utaisha? Ni muhimu kufahamu kuwa afya, uzima wako ni muhimu sana kwa watoto hao ili uweze kuwahudumia vizuri. Usiache kuchukua hatua kwa kigezo cha kutokujua hatma ya watoto. Vipo vyombo vya kisheria vinavyoweza kusaidia kupata haki ya malezi na matunzo kwa watoto endapo uhusiano baina ya wazazi utakuwa umeharibika.

 1. Hofu ya kuogopa hali kuwa mbaya zaidi

Katika kuendeleza unyanyasaji wa maneno na vitendo, baadhi ya watu wamekuwa watisha wenzi wao kuwa endapo ataeleza kwa watu au vyombo vingine basi ataendeleza mateso au manyanyaso zaidi. Ieleweke kuwa mtu anayetoa vitisho hivyo tayari yeye ni mwoga, ana hofu ya kuchukuliwa hatua na vyombo husika. Usikubali kuendelea kunyanyasika kila leo kwa hofu ya mateso kuendelea. Ni heri kutoa taarifa ili kupata msaada wa mapema kabla mambo hayajaharibika zaidi.

 1. Mfungamano wa Kifamilia

Kama tunavyofahamu kuwa mahusiano ya kindoa au uzazi yanahusisha familia pana zaidi yaani ndugu wa pande zote. Ndugu pia wamekuwa chanzo cha kuendeleza manyanyaso na vipigo dhidi ya wanandoa kwa kuingilia au kupendelea pande za ndugu zao. Wengi wanahofu ya kuchukua hatua kutokana na mitazamo ya ndugu watasemaje. Pia upo wakati wa ndugu kulaumu endapo ndugu yao atachukuliwa hatua dhidi ya unyanyasaji.

Kwa kuangalia sababu zote hizi haziwezi kuwa mbadala wa uhai wa mwathiriwa au ustawi wa afya yake kwa ujumla. Hakuna sababu ya msingi inayoweza kumzui mtu kuchukua hatua. Kama upo kwenye kundi la watu ambao wananyanyasika kwenye uhusiano na una mojawapo ya sababu hizi ni vyema kufahamu kuwa hiyo si sababu ya msingi. Uhai wako na ustawi wa afya yako kama mwanadamu ndio sababu ya msingi na kitu cha kwanza kulindwa na wewe.

Ni vyema kama jamii tukachukua mtazamo mmoja wa kutoruhusu jamii yetu iishi katika hali hii ya vipigo na manyanyaso. Kama kuna tatizo baina ya watu walio kwenye mahusiano basi jamii tuwasidie kufikia mwafaka pasipo kupigana. Tusikubali kuchukua upande wa wanyanyasaji hata kama ni ndugu zetu, tuwasaidie kumaliza tofauti zao kwa amani na ikishindikana hivyo basi wafuate utaratibu wa kisheria inavyopaswa pasipo madhara ya kupigana.

Kumbuka kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail ulizasheria@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms 0787 466 687.

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili

Sheria Leo.125. Ulinzi wa Kisheria dhidi ya Ukatili kwenye Mahusiano

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa makala za Sheria Leo ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Tumejifunza kwa muda mrefu juu ya makosa mbali mbali na namna ya kisheria kosa linavyotokea kwa kitendo na dhamira. Katika makala iliyopita tulianza kuangalia juu ya Jinai ya Kipigo kwenye mahusiano. Leo tunaendelea na sehemu nyingine juu ya Ulinzi wa Kisheria dhidi ya Ukatili kwenye Mahusiano.

Ulinzi wa Kisheria dhidi ya Ukatili kwenye Mahusiano

Ni jambo la kufahamu wa watu wote walio kwenye mahusiano iwe ya kindoa au mahusiano mengine, kwamba hakuna mtu anayemmiliki mwenzi wake. Kila mmoja ana haki ya kulindwa na Katiba na Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katiba ya JMT inaeleza wazi wazi kuwa kila mwananchi anayo haki ya kuishi. Ibara ya 14 ya Katiba ya JMT inasema

kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha yake kwa jamii kwa mujibu wa sheria’.

Maisha ni zawadi ambayo kila mwanadamu amepewa na Mungu, hivyo mifumo ya tawala za duniani kwa mujibu wa Katiba na sheria inawajibika kulinda na kutunza maisha ya kila mmoja wetu.

Kumekuwa na dhana ya kijamii kuwa mume anammiliki mwanamke kwa sababu tu ya utamaduni kuwa waume ndio wanaoa na kulipa mahari. Dhana hii imeleta madhara makubwa hasa kwa makundi ya wanawake katika kujikuta wananyanyasika na kudhalilika katika mahusiano. Maneno makali, vipigo na matishio ya mara kwa mara vimehusishwa sana na wanaume dhidi ya wanawake.

Mahusiano ya mume na mke au mapenzi kati ya mtu mume na mke, hayawezi kumpa mmoja wapo au wote haki ya kummiliki mwengine. Kila mmoja analindwa na sheria.

 

Mambo ya Msingi kuzingatia kwenye mahusiano ili kuepusha jinai ya kipigo;

 • Kufahamu msingi wa ulinzi wa Kikatiba na Kisheria kwa watu wote ikiwa ni pamoja na wanandoa au walio kwenye mahusiano
 • Walio kwenye mahusiano kutoona aibu au fedheha kutoa taarifa kwa watu au serikali au ustawi wa jamii juu ya vitendo vinavyoashiria ukatili dhidi ya utu wao

 

 • Jamii kutokunyamaza au kutokupuuzia matendo au viashiria vya unyanyasaji na ukatili katika mahusiano.

Endelea kufuatilia makala zinazokuja ili kujifunza hatua zinazopaswa kuchukua ili kupunguza tatizo hili la vipigo katika mahusiano.

 

Kumbuka kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail ulizasheria@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms 0787 466 687.

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili

 

Sheria Leo.124:A. Jinai ya Kipigo kwenye Mahusiano

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa makala za Sheria Leo ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Tumejifunza kwa muda mrefu juu ya makosa mbali mbali na namna ya kisheria kosa linavyotokea kwa kitendo na dhamira. Leo tunaenda kuangalia juu ya Jinai ya Kipigo kwenye mahusiano.

Makosa ya Kijinai

Katika makala za mwanzo kabisa tulijifunza juu ya makundi ya sheria na mojawapo ni kundi la Sheria za Jinai. Makosa ya kijinai ni aina ya makosa ambayo mtu akifanya anashtakiwa na Jamhuri/Serikali na matokeo yake endapo atapatikana na hatia basi anaweza kupata adhabu ya kifungo au faini au adhabu nyingine yoyote kwa mujibu wa sheria.

Kwa siku za karibu kumeongezeka makosa mengi au kumekuwa na wimbi kubwa la utendaji wa makosa ya kijinai hasa yanayohusiana na mahusiano baina ya mume na mke au wapenzi yaani watu walio kwenye uhusiano.

Tumesikia utendaji wa makosa haya kwenye vyombo vingi vya habari juu ya mume kumpiga mke hata kusababisha ulemavu au kupelekea mauti. Tumesikia mauaji ya kutisha ya kifamilia kwa sababu zinazoelezwa kuwa ni ‘wivu wa mapenzi’ n.k

Kama jamii na wadau tunaoishi ndani ya jamii hii tunapaswa kujiuliza tumefikaje hapa na katika hali hii na ipi njia nzuri ya kuweza kupunguza au kuepusha madhila haya ndani ya jamii zetu ambayo yameacha simanzi kubwa sana.

Msingi wa Mahusiano

Sheria ya Ndoa ya 1971 inatambua kuwa watu wanaweza kuwa kwenye mahusiano ya kindoa. Kwamba uhusiano huu ni wa hiyari baina ya mwanamke na mwanaume ambao wamefikia umri mwafaka wa kuamua kuishi pamoja.

Sheria ya ndoa inatambua kutokana na jamii yetu zipo ndoa ambazo zinafungwa kiserikali yaani bomani, zipo zinazofungwa kwenye nyumba za ibada yaani makanisani na misikitini na zile ambazo zinafungwa kimila. Zote hizi ni ndoa na halali kwa jamii kuzitambua.

Hatahivyo, ipo dhana ya ndoa ambayo inatambuliwa na sheria endapo mtu mume ataishi na mtu mke kwa kipindi kisichopungua maika 2 na kuonekana mbele ya jamii kama mke na mume watachukuliwa katika hali hiyo mpaka pale itakapodhibitika vinginevyo.

Msingi huu wote unaooneshwa kwenye sheria yetu ya ndoa ya 1971 inadhihirisha kuwa jamii yetu kwa ustaarabu wake na kuheshimu utashi wa watu wawili kuwa pamoja umeweka mazingira yote yanayowezekana ili watu hawa waishi kwa amani kwa hiyari yao wenyewe.

Katazo la ukatili katika mahusiano

Sheria ya ndoa ya 1971 inatoa onyo kwa pande zote kuwa ukatili katika ndoa unaweza kusababisha ndoa kuvunjika. Vipigo, manyanyaso na mambo mengine ya kikatili yanaweza kusababisha ndoa kuvunjwa na mahakama.

Hatahivyo, kama jamii tumekuwa tukishuhudia ukatili mkubwa ndani ya mahusiano ya kindoa na hata sasa ukatili au vipigo hivyo vimepitiliza hata kwenye mahusiano ya ‘boy friend’ na ‘girl friend’ kitu ambacho si sawa. Tunachokuja kushuhudia mwisho wa siku ni watu kuumizwa, kupata ulemavu na hata kupoteza maisha.

Kama jamii tunao wajibu mkubwa wa kuona tatizo hili na kuchukua hatua madhubuti ya namna bora ya kisheria kukabiliana nalo.

Endelea kufuatilia makala zinazokuja ili kujifunza hatua zinazopaswa kuchukua ili kupunguza tatizo hili la vipigo katika mahusiano.

 

Kumbuka kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms 0787 466 687.

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili

 

 

 

Sheria Leo.123: Aina ya Dhamira za Kijinai ‘Kinds of Mens rea’

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa makala za Sheria Leo ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Katika makala iliyopita kwenye tuliangalia juu ya Mambo ya Msingi ya Kitendo cha Kijinai. Leo tunakwenda kuangalia tena kwa undani juu ya Aina ya Dhamira za Kijinai ‘Kinds of Mens rea’

Dhamira ya Kijinai

Tumeona katika makala zilizotangulia juu ya umuhimu wa kiashiria cha kosa ni muhimu kwa dhamira ya kijinai kudhibitika mbali na kitendo cha kijinai peke yake. Dhamira ya kijinai inazungumzia hali ya kifikra ya mtuhumiwa wakati anatenda kosa husika.

Tuliona msisitizo huu katika maneno haya ya Kiingereza

‘the act itself does not constitute guilt unless done with a guilty intent’

Maneno haya yakimaanisha kuwa kitendo pekee cha kijinai hakiwezi kuonesha hatia mpaka kiwe kimeambatana na dhamira ya kijinai.

Aina ya Dhamira za Kijinai

Katika somo la leo tunaendelea kujifunza zaidi juu ya msingi wa mahakama kuchunguza kuhusu aina za dhamira za kijinai katika kufikia maamuzi juu ya kesi mbele yake. Katika mfumo wa kuchambua makosa na namna dhamiri ya kijinai ilivyohusika na kiwango cha adhabu atakachopata mtuhumiwa dhamira hizi zimegawanywa katika makundi yafuatayo;

 1. Dhamira ya Makusudi ya Kijinai ‘Intentional mens rea’

Aina ya dhamira hii ya makusudi ni ile ambayo inaonesha kuwa mtuhumiwa alikusudia kutenda kosa alilotenda kwa utashi wake huku akijua kitendo anachofanya ni cha kihalifu na kina madhara kwa mwathiriwa. Katika kupima endapo dhamira ilikuwa kusudi ni lazima kuona kuwa

 • Mtuhumiwa anajua matokeo ya kitendo anachofanya; hii ina maana mtuhumiwa anajua madhara ya kile kitendo anachokusudia kufanya. Mfano mtu anaiba fedha anajua matokeo yake ni hasara kwa mwathiriwa wa kuibiwa.

 

 • Mtuhumiwa anakusudia matokeo hayo ya kitendo chake yatokee; hapa ina maana mtuhumiwa kwa kujua kwake matokeo ya kitendo chake anakusudia kuyaona au kuyafikia matokeo hayo. Mfano mtuhumiwa anaiba kwa kusudi la kumnyang’ang’anya mwathiriwa haki ya mali yake. Katika kuainisha makosa ya makusudi ni muhimu sheria inayotamka kosa husika ioneshe dhamira ya kosa la makusudi. Mfano ‘kwa kukusudia’ ‘kwa utashi’ n.k

 

Katika shauri la Brazila vs Jamhuri la 1968, mtuhumiwa alikuwa karani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba na alikuwa mwangalizi wa wafungwa waliokuwa katika Mahakama ya Mwanzo kwa mashauri yao. Aliwatoa wafungwa wawili kwenye chumba cha mahabusu na kuwaamuru kufua nguo zao naye akaenda kutembea wafungwa wakatoroka. Mtuhumiwa alishitakiwa kwa kosa la kusaidia wafungwa kutoroka kinyume cha Kifungu 117 (1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu akahukumiwa kifungo. Wakati wa rufaa Jaji wa Mahakama kuu Mustafa aliangalia sheria na kifungu alichoshitakiwa nacho na kuona kuwa kilihitaji dhamira ya makusudi kudhibitishwa hivyo akabatilisha hukumu na kuhukumu kuwa mtuhumiwa alikuwa mzembe wa hali ya juu.

 

 1. Dhamira ya Uzembe uliokithiri ya Kijinai ‘ Recklessness mens rea’

Hapa dhamira ya uzembe uliokithiri hutokea katika mazingira ambayo mtuhumiwa anajua kuwa kutokana na kitendo chake kuna uwezekano mkubwa wa madhara kutokea lakini hayuko tayari kuyataka matokeo ya kitendo chake anachofanya. Kiwango cha uzembe huu uliokithiri katika kudhibitisha shitaka adhabu yake inakuwa tofauti na ile ya dhamira ya makusudi.

Mfano.

Dereva wa gari anaendesha gari pasipo kufuata sheria za barabarani haendi kwa mwendo unaopaswa kisheria na anadharau taa za barabarani matokeo yake kamgonga mtembea kwa miguu na kufa papo hapo. Dereva huyu pamoja na kwamba ameua lakini hatoshitakiwa kwa kosa la kuua kwa makusudi bali uendeshaji wa uzembe uliokirithi na kusababisha kifo cha mtembea kwa miguu.

 1. Dhamira ya Uzembe ya Kijinai ‘Negligence mens rea’

Hii ni aina nyingine ya dhamira ya kijinai ya uzembe ambapo mtuhumiwa haoni athari ya moja kwa moja ya matokeo ya kitendo anachofanya au anachoacha kufanya lakini kwa mtu wa kawaida alipaswa kufahamu kuwa kitendo chake kina madhara.

Katika shauri la Jamhuri vs Chape Kalangari la 1973 mtuhumiwa alishindwa kumuhudumia mtoto ambaye alikuwa anamtunza ambaye alikuwa anasumbuliwa na mafua makali. Kutokana na kutopata matunzo na usaidizi wa matibabu mtoto akafariki. Mahakama ilimpata mtuhumiwa na kosa la kuua kwa kutokukusudia sawa na Kifungu cha 203 cha Kanuni ya Adhabu. Mahakama ilisema kuwa ili mtu akutwe na hatia ya mauaji pasipo kukusudia kwenye mazingira haya ni lazima awe na wajibu wa kisheria wa kutimiza.

 

Hitimisho

Leo tumejifunza juu ya aina za dhamira ya kijinai ambazo ni makusudi, uzembe uliokithiri na uzembe. Mahakama ni lazima ijiridhishe juu ya aina ya dhamira inayohitajika katika kila kosa kabla ya kumhukumu mtu kuwa na hatia. Hivyo unapokuwa umetenda kosa au kuna mtu ametenda kosa ni muhimu kupata ushauri wa wanasheria kujua ni kwa mazingira gani kosa hilo limetendeka na endapo adhabu yake itakuwa ya namna gani kuweza kuandaa utetezi wako vizuri au utetezi wa mtuhumiwa vizuri.

Endelea kufuatilia makala ijayo ili kujifunza zaidi juu ya kiashiria kingine cha kosa la kijinai.

Kumbuka kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms 0787 466 687.

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili

 

 

Sheria Leo.122: Fahamu Mambo ya Msingi kuhusu Kitendo cha Kijinai ‘Actus reus’

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa makala za Sheria Leo ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Katika makala iliyopita kwenye tuliangalia juu ya kitendo cha kijinai na dhamira ya kijinai. Leo tunakwenda kuangalia tena kwa undani juu ya mambo ya msingi ya kuzingatia kuhusu Kitendo cha Kijinai.

Kitendo cha Kijinai

Kwa kuangalia makala zilizopita tulizungumzia juu ya viashiria vya kosa la jinai kuhusisha ‘kitendo cha kijinai’ na ‘dhamira ya kijinai’ yaani ‘actus reus’ na ‘mens rea’. Tumeona kwa mifano juu ya kitendo cha kijinai na namna ambayo kinafanya kazi.

Kitendo cha kijinai au ‘actus reus’ kinaweza kutafsiriwa kama tendo au kitendo ambacho sheria imekataza mtu kufanya. Tendo kinyume cha sheria.

Kwa mujibu wa sheria suala la kitendo cha kijinai linahusisha dhana kuu mbili yaani ‘kutenda kitendo kilichokatazwa na sheria’ au ‘kuacha kutenda kile ambacho unawajibika kutenda’. Kwa tafsiri ya kiingereza ina maana      ‘actus reus means an act or omission punishable by law’

Dhana hii tunaiona pia katika sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, Kifungu cha 5 kinachosema

Kosa ni kitendo, jaribio au kuacha kutenda kunakoadhibiwa na sheria

‘Offence is an act, attempt or omission punishable by law’

Mambo ya Msingi kuhusu Kitendo cha Kijinai

Katika kutafsiri kitendo cha kijinai vyombo vinavyohusika ikiwepo Polisi, Ofisi ya Mashitaka na Mahakama ni lazima kuzingatia mambo haya ya msingi kabla ya mtuhumiwa kutiwa hatiani kutokana na kitendo alichokifanya endapo kimekidhi vigezo vya kuhesabika kama kitendo cha kijinai au la.

 1. Kitendo cha Kijinai kwa maana ya Kitendo kinyume cha sheria ‘an act as actus reus

Katika kupata tafsiri halisi ya kisheria na kudhibitisha juu ya kosa la kijinai ni muhimu mahakama kujiridhisha kuwa mtuhumiwa alitenda kitendo cha kijinai. Kitendo hiki ni lazima kiwe kimekatazwa na sheria au kinyume cha sheria. Lazima uwepo ushahidi wa kutosha kuwa ni mtuhumiwa na si mtu mwengine alitenda tendo hilo.

Mfano;

Kifungu cha 130 cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 kinatoa marufuku ya Kitendo cha Kubaka. Hivyo ili kosa hili lidhibitike ni lazima mtuhumiwa awe ametenda kitendo hicho kinyume na sheria. Kwa tafsiri ya sheria ni lazima mbakaji awe mwanaume.

 1. Kitendo cha Kijinai kwa maana ya Kuacha kutenda kwa mujibu wa sheria ‘ommission as actus reus’

Hapa mahakama inajikita katika kuangalia ni wajibu gani ambao mtuhumiwa alipewa kisheria kisha ni kwa jinsi gani hakutekeleza wajibu huo. Tunafahamu kuwa haki huambatana na wajibu na ili kupata haki lazima uhakikishe umetimiza wajibu.

Mfano;

Kifungu 167 cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 kinaeleza juu ya ‘mtu mwenye wajibu wa kutoa matunzo kwa watoto ikiwa ni chakula, malazi, mavazi na huduma za kiafya, akiacha kutenda au kutekeleza wajibu huo anakuwa ametenda kosa la kijinai.

 1. Kitendo cha Kijinai na Hali ‘actus reus with circumstances’

Yapo makosa ya kijinai ambayo sheria inachukulia yamefanyika kutokana na hali ya mazingira. Mtuhumiwa anaweza asionekane amefanya kitendo fulani au ameacha kutenda kitendo bali mazingira aliyokutwa nayo yanaweza kuashiria kosa la kijinai.

Mfano

Katika sheria zinazohusiana na Usalama Barabarani, sheria inamtaka dereva awe katika hali nzuri ya uendeshaji wa chombo yaani asiwe katika hali ya kilevi, endapo itabainika kuwa anaendesha huku akiwa na kilevi basi atakuwa ametenda kosa la jinai. Hapa hatuoni dereva akitenda kosa la kunywa kilevi lakini anakutwa kuwa hawezi kuendesha au kukidhibiti chombo kutokana na matumizi ya kilevi aliyoyafanya hapo awali.

 1. Kitendo cha Kijinai na Kusababisha madhara ‘actus reus with causation’

Ni muhimu sana mahakama ikapata uchunguzi wa kutosha kuhusiana na kosa na endapo ni kitendo cha mtuhumiwa husika ndicho kilicholeta madhara kwa mwathiriwa. Kuna wakati unaweza kujitokeza kwa mtuhumiwa kutenda kitendo kinyume cha sheria lakini kisilete madhara kwa mwathiriwa na hivyo kukosekana kwa hatia. Hivyo ni lazima idhibitike kuwa ni kitendo cha mtuhumiwa ndicho kilicholeta madhara kwa mwathiriwa.

Mfano

A anakusudia kumuua B na anamwekea sumu kwenye chakula. B kabla ya kula chakula alichowekewa anapata mshtuko wa moyo na kufariki. A pamoja na kwamba alikusudia kumuua B kitendo alichofanya hakikusababisha kifo cha B hivyo hawezi kuhesabiwa hatia ya kumuua B.

Ndio maana ni muhimu sana linapotokea tukio la kifo lazima wachunguzi wafahamu sababu husika ya kifo.

Hitimisho

Leo tumejifunza mambo ya msingi kuhusu kitendo cha kijinai yaani ‘actus reus’ ambao vyombo vya uchunguzi, mashitaka na mahakama lazima vijiridhishe kuwa mtuhumiwa ndiye muhusika wa kufanya kitendo cha kijinai pasipo shaka. Wapo watu wengi wameingia katika hatia pasipo kujua au kukosa namna ya kujitetea au utetezi unaopaswa na kujikuta wanahukumiwa. Pia ni muhimu kwa jamii kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kuadhibu watu pasipo kuwa na utaalam wa kujua endapo kitendo wanachodhani ni cha kijinai ikiwa kwa hakika kimetendwa na mtuhumiwa husika au la.

Endelea kufuatilia makala ijayo ili kujifunza zaidi juu ya kiashiria kingine cha kosa la kijinai.

Kumbuka kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms 0787 466 687.

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili