Sheria Leo. Ufanye nini unapozungushwa kupewa hukumu ya kesi yako?

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Leo kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku.

Kwa muda mrefu nimekuwa nikipokea maswali ya wasomaji na wadau wengi kuhusiana na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika mahakama. Changamoto hizi zimekuwa nyingi sana kiasi kwamba zinaibua hisia za watu kutokutendewa haki. Leo tunaenda kuangalia changamoto mojawapo ambayo nimekuwa nikiwajibu wasomaji wetu. Karibu tujifunze.

Je, ufanye nini unapozungushwa kupewa hukumu ya kesi yako?

Nimepokea jumbe kadhaa na simu za wadau wakiwa wanalalamika sana kuhusiana na kutokupatiwa hukumu au nakala ya hukumu kutokutolewa kwa wakati. Nimeona nitoe ufafanuzi katika makala hii ili iweze kukusaidia na wewe mdau katika kufuatilia haki yako ukiwa mahakamani.

Kama ilivyo kawaida tunatarajia kesi yoyote au mashitaka yoyote iwe ya madai au jinai huwa na kikomo. Hii ina maana kesi inapaswa kufunguliwa kisha kusikilizwa na hatimaye hukumu kutolewa mbele ya wadaawa. Hatahivyo, kumeibuka mtindo wa baadhi ya wahusika kuchelewesha hukumu au kutokutoa nakala za hukumu kama inavyopaswa. Kuna wakati kesi imemalizwa kusikilizwa muda mrefu lakini hukumu haisomwi kwa wakati.

Nimepata malalamiko kwa baadhi ya watu wanapewa tarehe za mbali ikiwezekana hadi Jumamosi na kutokupata majibu yanayojitosheleza kuhusiana na maamuzi ya kesi zao.

Kitu muhimu unachopaswa kufahamu ni kuwa uamuzi wa shauri au kesi yako ni haki yako na unapaswa kutolewa mapema kadri iwezekanavyo. Kuna baadhi ya watendaji wanatoa uamuzi kwa kificho kutokana na sababu zao ili mdaawa aliyeathiriwa na maamuzi asiweze kukata rufaa ndani ya wakati. Jambo hili si sawa na halipaswi kufumbiwa macho.

Hatua unazoweza kuchukua endapo uamuzi wa kesi unacheleweshwa au umetolewa lakini hujapata nakala yake;-

  • Andika barua ya kuulizia endapo uamuzi au hukumu ya kesi yako imeshasomwa
  • Endapo umesomwa na ulikuwepo mahakamani, pia andika barua kuomba kupatiwa nakala yako na nakala ya mwenendo wa shauri lako.
  • Endapo uamuzi utaendelea kuchelewa au kutokupewa nakala ya uamuzi basi andika barua kukumbushia na ambatanisha nakala ya barua kwa mahakama ya juu inayosimamia mahakama ambayo inapaswa kukupa uamuzi wako.

Watu wengi huishia kulalamika au kudai uamuzi kwa maneno kiasi kwamba siku wanaupata mkononi wanaonekana wamechelewa kuchukua hatua kama za kukata rufaa au kuomba marejeo katika ngazi ya juu. Lakini ukichukua hatua ya kuandika barua inakusaidia kuwa sababu ya msingi ya kukata rufaa katika ngazi inafuata.

Usiogope kufuatilia haki yako ya uamuzi au hukumu ya kesi inayokuhusu, hofu yako inaweza kupelekea kupoteza haki yako na uhuru wako.

 ‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040  na email zakejr@gmail.com