90. Nani mwenye mamlaka ya kusitisha ajira ya mwajiriwa?

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Tumeendelea kujifunza changamoto mbalimbali zinazotokea katika mahusiano ya kiajira na kuzitafutia ufumbuzi kwa lengo la kuboresha mahusiano ya kiajira. Katika makala iliyopita tumeona utangulizi wa kujua nani mwenye mamlaka ya kusitisha ajira ya mwajiriwa. Tumejifunza juu ya tofauti za mtu wa asili yaani mwanadamu na mtu wa kisheria mfano kampuni, taasisi au shirika. Leo tunakwenda kuangalia kwa mifano juu ya mtu wa asili kama mwajiri. Karibu tujifunze.

Namna ya Kisheria ya kuendesha shughuli au biashara

Kama tulivyoona katika makala iliyopita, ya kuwa mwajiri anaweza kuwa mtu wa asili au mtu wa kisheria. Ili kufahamu tofauti hizi na namna zinavyoweza kufanya kazi ni muhimu kufahamu namna ambazo mtu awe wa asili au kisheria anavyoweza kuendesha shughuli zake kisheria.

Usajili wa Shughuli za kibiashara

Ipo mamlaka maalum inayohusika na usajili wa shughuli zote za kibiashara ambayo imewekwa kwa mujibu wa Sheria. Hapa ni eneo ambalo watu wote iwe binafsi au ubia au kampuni wanasajili shughuli zao na kupata namba ya utambulisho kwa malengo ya kibiashara. Mamlaka ya Usajili ‘BRELA’ inahusika kusajili namna zote za biashara.

Katika usajili huu wa kibiashara mtu anaweza kusajili aina ya shughuli zake katika mifumo 3

  1. Biashara au shughuli ya mtu binafsi – hapa biashara hii inajulikana kama biashara ya mtu mmoja binafsi au kwa lugha ya kiingereza ‘Sole Proprietorship’

Hii ni aina ya biashara binafsi inayoendeshwa na mtu mmoja ambaye anahusika kuzifanya shughuli zake au kwa usaidizi wa watu wengine kama waajiriwa wake.

Mifano ipo mingi ya aina ya shughuli kama hizi za biashara au huduma ya mtu binafsi kama maduka ya jumla na rejareja, wakala wa mitandao kama tigopesa, M-pesa, Airtel money, magenge, maduka ya vifaa mbalimbali, huduma za kitaalam za ushauri n.k.

Hivyo katika biashara ya mtu binafsi inaweza kuwa inaendeshwa kwa majina halisi ya mtu mwenyewe au akawa amesajili majina ya biashara.

Mfano

Mtu binafsi ana duka lake la rejareja amelisajili kwa jina la ‘MWENDOKASI SHOP’ ambapo majina halisi ya muhusika ni ADAM JUMA HASSAN. Katika hali kama hii mwajiri halisi katika biashara hii ya duka endapo kutakuwa na wafanyakazi ni ADAM JUMA HASSAN.

Changamoto

  • Kuna watu wanaendesha biashara zao binafsi kwa majina ya biashara ambayo hayajasajiliwa
  • Kuna watu wanaonekana biashara ni zao lakini kumbe zina wamiliki nyuma yao ambao ni binafsi nao ni wasimamizi tu kwa lengo la kuendesha biashara.

Hizi ni changamoto kubwa sana wanazokumbana nazo wafanyakazi hasa wale wasio na mikataba ya maandishi.

Ni muhimu sana kwa waajiriwa na waajiri kufahamu sababu na haki ya matumizi ya majina wanayotoa kwa biashara zao. Kumekuwa na mifano mingi ya migogoro ya kazi inafunguliwa na wafanyakazi wakidai kwa kutumia majina ya biashara ya waajiri wao bila kujiridhisha endapo majina hayo ni kweli na yapo kisheria. Wapo watu wana majina ya biashara au shughuli zao wamezipa majina lakini hawajayasajili kisheria.

Pia wapo watu ambao ni wasimamizi wa biashara ambazo zina majina ya biashara na wanaajiri wengine huku wao si wamiliki. Inapotokea changamoto ya mgogoro wafanyakazi hukimbilia kumshtaki msimamizi badala ya kujiridhisha nani ni mmiliki kisheria wa jina la biashara kama lipo.

Hivyobasi una wajibu wa kujua endapo jina la biashara linalotumika katika sehemu ya ajira kama limesajiliwa na endapo muhusika ambaye unataka kufungua mgogoro wa kikazi anahusika moja kwa moja na umiliki binafsi wa biashara hiyo.

Wafanyakazi wengi wamepoteza haki zao kwa kushindwa kujua nani mtu sahihi wa kumshtaki pale mgogoro unapojitokeza. Njia pekee ya kuweza kukusaidia kuepuka adha hii ni kuhakikisha unadai mkataba wa maandishi pindi unapoanza kufanya kazi katika eneo lako la ajira.

Endelea kufuatilia mfululizo huu tunapojibu swali hili la wasomaji wetu katika makala zijazo.

MUHIMU

Ningependa kukukaribisha ndugu msomaji wa Uliza Sheria, ikiwa una maswali yanayohusu suala la KAZI na AJIRA katika sheria, basi karibu kuuliza kwa mawasiliano hapo chini na sisi tutatoa ufafanuzi kunufaisha watu wote. Tuma ujumbe mfupi kwenye namba za simu au barua pepe.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Isaack Zake, Wakili

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 (wats app) (sms) na email zakejr@gmail.com