91. Mamlaka ya mwajiri wa ubia au kampuni katika kusitisha ajira

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Tumeendelea kujifunza changamoto mbalimbali zinazotokea katika mahusiano ya kiajira na kuzitafutia ufumbuzi kwa lengo la kuboresha mahusiano ya kiajira. Katika makala iliyopita tumeona juu ya mamlaka ya mwajiri binafsi na changamoto zinazoambatana nazo. Leo tunakwenda kuangalia kwa mfano juu ya ajira ya ubia au kampuni kuwa na mamlaka ya kusitisha ajira. Karibu tujifunze.

Namna ya Kisheria ya kuendesha shughuli au biashara

Kama tulivyoona katika makala iliyopita mtu binafsi anaweza kuwa mwajiri akiwa yeye binafsi au kwa kutumia majina ya biashara. Hatahivyo mfumo wa kuendesha biashara au shughuli unamwezesha mwajiri kuajiri katika hali ya ubia au taasisi au kampuni.

Biashara ya ubia ni aina ya shughuli inayoendeshwa na watu wawili au zaidi mpaka 20 kwa mujibu wa sheria, kwa upande mwengine kampuni ni aina ya biashara inayosajiliwa kisheria kama mtu wa kisheria.

Biashara ya ubia au kampuni inaweza kuajiri watu kwa kutumia majina ya ubia au kampuni au taasisi husika.

Uendeshaji wa biashara ya ubia au taasisi au kampuni upo kwa mujibu wa sheria na kuondoka kwa mbia au kuondoka kwa mkurugenzi wa kampuni hakuwezi kubadili hatma ya mfanyakazi.

Mfano

Mtu binafsi ana duka lake la rejareja amelisajili kwa jina la ‘MWENDOKASI SHOP’ ambapo majina halisi ya muhusika ni ADAM JUMA HASSAN. Katika hali kama hii mwajiri halisi katika biashara hii ya duka endapo kutakuwa na wafanyakazi ni ADAM JUMA HASSAN.

Changamoto

  • Kuna watu wanaendesha biashara zao binafsi kwa majina ya biashara ambayo hayajasajiliwa
  • Kuna watu wanaonekana biashara ni zao lakini kumbe zina wamiliki nyuma yao ambao ni binafsi nao ni wasimamizi tu kwa lengo la kuendesha biashara.

Hizi ni changamoto kubwa sana wanazokumbana nazo wafanyakazi hasa wale wasio na mikataba ya maandishi.

Ni muhimu sana kwa waajiriwa na waajiri kufahamu sababu na haki ya matumizi ya majina wanayotoa kwa biashara zao. Kumekuwa na mifano mingi ya migogoro ya kazi inafunguliwa na wafanyakazi wakidai kwa kutumia majina ya biashara ya waajiri wao bila kujiridhisha endapo majina hayo ni kweli na yapo kisheria. Wapo watu wana majina ya biashara au shughuli zao wamezipa majina lakini hawajayasajili kisheria.

Pia wapo watu ambao ni wasimamizi wa biashara ambazo zina majina ya biashara na wanaajiri wengine huku wao si wamiliki. Inapotokea changamoto ya mgogoro wafanyakazi hukimbilia kumshtaki msimamizi badala ya kujiridhisha nani ni mmiliki kisheria wa jina la biashara kama lipo.

Hivyobasi una wajibu wa kujua endapo jina la biashara linalotumika katika sehemu ya ajira kama limesajiliwa na endapo muhusika ambaye unataka kufungua mgogoro wa kikazi anahusika moja kwa moja na umiliki binafsi wa biashara hiyo.

Wafanyakazi wengi wamepoteza haki zao kwa kushindwa kujua nani mtu sahihi wa kumshtaki pale mgogoro unapojitokeza. Njia pekee ya kuweza kukusaidia kuepuka adha hii ni kuhakikisha unadai mkataba wa maandishi pindi unapoanza kufanya kazi katika eneo lako la ajira.

Endelea kufuatilia mfululizo huu tunapojibu swali hili la wasomaji wetu katika makala zijazo.

MUHIMU

Ningependa kukukaribisha ndugu msomaji wa Uliza Sheria, ikiwa una maswali yanayohusu suala la KAZI na AJIRA katika sheria, basi karibu kuuliza kwa mawasiliano hapo chini na sisi tutatoa ufafanuzi kunufaisha watu wote. Tuma ujumbe mfupi kwenye namba za simu au barua pepe.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Isaack Zake, Wakili

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 (wats app) na email zakejr@gmail.com