Ujue Mfumo wa Mahakama

Utangulizi

Mahakama ni chombo muhimu sana katika ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla. Mahakama ni nguzo muhimu sana katika kuhakikisha haki ya wananchi na jamii ya ujumla inalindwa na kutekelezwa ipasavyo. Zimekuwepo changamoto nyingi sana kwa jamii kufikia mfumo huu wa mahakama na kupata kutatuliwa shida zao. Hali hii imesababisha watu kudhulumiwa haki zao au kucheleweshewa haki zao ambazo walistahili kuzipata. Hali kadhalika ukosefu wa uelewa au ufahamu jinsi mahakama zinavyofanya kazi kumepelekea watu wengine kujichukulia sheria mkononi na kuleta madhara zaidi kwa jamii.

Hivyobasi, mtandao wako wa Uliza Sheria umeona vyema kuanzisha sehemu maalum ya wasomaji kujifunza zaidi kwa undani namna Mahakama zinavyofanya kazi au kuijua zaidi mifumo ya mahakama ili watu waweze kuchukua hatua stahiki na kufuata utaratibu wa kisheria unaohitajika katika kufuatilia haki zao.

Katika makala ya leo ya utangulizi tunataka kuifahamu vizuri Mahakama ni nini hasa na imeanzishwaje na ipi nafasi yake katika Mfumo wa uendeshaji wa nchi. Karibu sana tujifunze kwa pamoja.

Uanzishwaji wa Mamlaka ya Mahakama

Mahakama kama ilivyo Serikali au Bunge ni chombo cha kikatiba yaani ni zao la Katiba. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 inaeleza wazi kabisa juu ya uundwaji na uanzishwaji wa Mahakama kama chombo au muhimili wa Dola.

Ibara ya 107 A inaeleza wazi juu ya jukumu hili la Mahakama kama ifuatavyo;

‘Mamlaka ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa mikononi mwa Idara ya Mahakama na Idara ya Mahakama ya Zanzibar, kwa hiyo hakuna chombo cha Serikali wala cha Bunge au Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kitakachokuwa na kauli ya mwisho katika utoaji haki’

Ibara hii ya 107 A ni muhimu sana kwa kila mmoja wetu kuifahamu na kuielewa ya kwamba Mahakama ndio chombo chenye kauli ya mwisho katika suala zima la utoaji wa haki ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katiba imeweka wazi ya kuwa Mahakama katika majukumu yake ya utoaji haki haipaswi kuingiliwa na chombo kingine cha Dola iwe Bunge au Baraza la Wawalikilishi au Serikali.

Ikiwa Katiba imeelekeza hivi, hii ina maana ya kuwa mwananchi au raia yeyote anayo haki ya kwenda mahakamani katika suala lolote ambalo anaona hajaridhika nalo kimaamuzi lililofanywa na mtu binafsi au chombo chochote cha Serikali au mamlaka nyingine yoyote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ni muhimu sana kufahamu mgawanyo wa majukumu uliopo kikatiba baina ya vyombo vya Dola. Hii itasaidia sana wananchi kufahamu ni wapi au ni nani au chombo kipi cha Dola kinahusika na kitu gani kwa mujibu wa Sheria na Katiba.

Kwa mujibu wa Katiba ya JMT, utawala wa nchi umegwanywa mamlaka yake katika Mihimili mitatu (Organs of State) yaani;

  • Mamlaka ya Bunge – inahusisha utungaji wa Sheria
  • Mamlaka ya Mahakama – inahusisha kutafsiri sheria na kutoa haki
  • Mamlaka ya Serikali – inahusisha utekelezaji wa sheria

Hivyo ni muhimu sana kwa kila mmoja wetu kufahamu majukumu mahsusi ya kila Mhimili wa Dola ili kutusaidia kuchukua hatua zinazostahili katika utatuzi wa changamoto zetu. Endapo mwananchi anaona amedhulumiwa haki yake basi mahali mahsusi pa kutafuta haki hiyo ni Mahakamani.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi.

Wako

Isaack Zake, Wakili

Makala hii imeandaliwa na Isaack Zake ambaye ni wakili wa Mahakama Kuu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wakili Isaack Zake pia ni mwandishi na anatoa huduma za kisheria kupitia ofisi ya mawakili Zake Advocates. Wakili Isaack Zake amekuwa akitoa elimu ya sheria kupitia mtandao wa www.ulizasheria.co.tz na ameandika zaidi ya makala 250 kwenye maeneo mbalimbali ya sheria ikiwemo ajira, ardhi, biashara, Katiba, mirathi, ndoa na jinai. Wakili Isaack Zake amebobea zaidi katika sheria za Kazi na Ajira. wasiliana naye kwa barua pepe kupitia info@ulizasheria.co.tz  au 0713 888 040.