Sheria Leo.Hatua Dhidi ya Wanaochukua Sheria Mkononi

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Leo kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku.tumekuwa na mfululizo wa makala zinazohusu tabia ya watu kujichukulia sheria mkononi. Leo tunaangalia hatua dhidi ya watu wanaojichukulia sheria mkononi. Karibu tujifunze.

Mfumo wa Kujichukulia Sheria Mkononi

Kwa takribani wiki mbili sasa tumekuwa tukiangalia dhana nzima iliyojengeka katika jamii katika suala la kuchukua sheria mkononi ndani ya jamii. Tumeona maana yake, sababu zinazosababisha jamii kujenga tabia hii, madhara yake na hata maneno ya migogoro mingi ambayo watu huchukua hatua mkononi.

Kwa kiasi kikubwa tumeona kuwa tabia hii imeota mizizi katika jamii yetu na imekuwa ikiongezeka siku kwa siku katika maeneo mbali mbali ya nchi yetu.

Watu wamejenga fikra kuwa hakuna namna yoyote unayoweza kuchukuliwa hatua za kisheria endapo utakuwa umejichukulia sheria mkononi pasipo kufuata utaratibu. Dhana hii si kweli kwani vitendo vyovyote vya kujichukulia sheria mkononi hata kama ilikuwa ni kundi au kwa kufuata mkumbo bado huo ni uhalifu dhidi ya Jamhuri na endapo mtu atapatikana amefanya vitendo hivyo basi hatua zaidi zinaweza kuchukuliwa dhidi yake.

Hatua dhidi ya wanaochukua sheria mkononi

Zipo hatua mbalimbali zinazoweza kuchukuliwa dhidi ya uhalifu wa kujichukulia sheria mkononi. Hatua hizi zipo katika sheria zetu na endapo mtu atabainika basi mchakato wa adhabu dhidi yake unaweza kuanza mara moja. Maeneo makuu mawili ya hatua dhidi ya uhalifu wa kujichukulia sheria mkononi;

  1. Hatua za kijinai

Endapo mtu au watu  watabainika kuwa walichukua sheria mkononi na kutekeleza uhalifu Fulani iwe kumpiga mtu mwengine au kuua au kuharibu kitu chochote basi huo utahesabika kuwa ni uhalifu dhidi ya mtu au mali ambapo mchakato wa kijinai unaweza kuanzishwa dhidi yao. Aliyeathiriwa na vitendo vya mtu au watu waliochukua sheria mkononi anao wajibu wa kutoa taarifa katika kituo cha Polisi na kisha uchunguzi wa tukio zima unaanza mara moja na wahusika kutafutwa na kuhojiwa kisha kupelekwa mahakamani. Watuhumiwa hawa waliojichukulia sheria mkononi watashitakiwa kama watuhumiwa wengine na endapo mahakama itaridhika na ushahidi husika basi watahukumiwa ipasavyo. Pale endapo mwathiriwa wa vitendo vya watu kujichukulia sheria mkononi atakuwa amefariki, basi ndugu zake wanaweza kuanzisha mchakato huo wa kutoa taarifa dhidi ya dhuluma aliyofanyiwa ndugu yao.

  1. Hatua za kimadai

Katika mchakato wa hatua za kimadai, endapo mwathiriwa katika hatua za mtu au watu kujichukulia sheria mkononi atabaini madhara dhidi yake au mali yake basi anayo haki ya kufungua shauri la madai dhidi ya mtu au watu waliomwathiri kwa matendo yao. Hapa shauri linafunguliwa kimadai ambapo mwathiriwa atadai fidia stahiki toka kwa mtu au watu waliojichukulia sheria mkononi dhidi yake au mali zake.

Hitimisho

Katika kuhitimisha mfululizo wa makala hizi za tabia za watu kujichukulia sheria mkononi, nipende kusisitiza kuwa siku zote uhalifu hauwezi kukomeshwa na uhalifu bali na mchakato mzuri wa kisheria na kuwa na jamii ambayo inajitathmini kila mara kufahamu chanzo hasa cha uhalifu ndani ya jamii. Wengi tumekuwa watu wa kuhukumu mara kwa mara pasipo kuchukua muda na kuona ni kwa jinsi gani tumehusika na kushiriki kuijenga jamii iliyopo sasa. Wazazi wengi na wanafamilia wanalaumu vijana kuwa hawana mwenendo mzuri kama wao walivyokuwa vijana. Swali ni juu ya wazazi na walezi kwa jinsi gani wameshindwa kuwapa malezi bora vijana kama waliyopewa wao na wazazi au walezi wao.

Kwa hakika lipo ombwe la kizazi cha sasa na kile kilichopita kiasi kwamba hatusikilizani katika mambo mengi. Hii ni hatari sana kwa jamii yetu ambayo asilimia kubwa inaundwa na watoto na vijana wengi kuliko wazee. Ni vyema kama taifa tukatumia muda kujitathmini na kujitafakari juu ya namna bora ya kujenga misingi ya maadili kwa ajili ya vizazi vya sasa na baadae.

‘Acha kujichukulia sheria mkononi, acha kuchochea tabia hii, huwezi jua kesho inaweza kuwa dhidi yako au kwa mtu wa karibu yako’

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

 

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili