Utetezi wa kisheria kutokana na Umri
Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji wa makala za Sheria Leo ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Katika makala za tumeendelea kukuelimisha katika nyanja za kisheria. Pia tuligusia kidogo kwenye masuala ya jinai na kuangalia msingi wa sheria za kijinai. Leo tunakuletea Utetezi wa Kisheria Kutokana na Umri mdogo (Defense of Immaturity).
Msingi wa Utetezi katika Mashitaka ya Kijinai
Sheria ya Kanuni ya Adhabu pamoja na kuainisha makosa mbali mbali imeainisha pia aina za utetezi ambapo mtuhumiwa anaweza kutumia kujitetea pale anaposhitakiwa mahakamani. Mtuhumiwa kwenye makosa ya jinai ana haki ya kuleta hoja za utetezi ambazo zinaweza kumwondolea tuhuma zinazomkabili.
Hoja ya utetezi umri mdogo ni mojawapo wa sababu za kuweza kumsaidia mtuhumiwa kutotiwa hatiani kwa kosa analoshitakiwa nalo.
Katika makala ya Sheria Leo.36 tuliangalia mojawapo ya aina ya utetezi unaoitwa Dai la Haki kwa Uaminifu. Rejea makala hiyo upate kujifunza.
Maana ya Utetezi wa Kisheria kwa mujibu wa Umri
Huu ni aina ya utetezi unaohusiana na umri mdogo wa mtu anayetuhumiwa kutenda kosa la kijinai. Hatahivyo, utetezi huu hauwezi kutumika na watoto wote kwa kigezo cha kuwa chini ya miaka 18 kama Sheria ya Mtoto ya 2009 inavyotoa tafsiri ya mtoto.
Kutokana na tafsiri ya mtoto kwenye Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inaeleza kuwa mtoto ni mtu aliye na umri chini ya miaka 18. Hata hivyo kwa mujibu wa sheria ya Kanuni za Adhabu inaonesha kuwa si watoto wote wanaondolewa uwezekano wa kushtakiwa ikiwa wapo chini ya umri wa miaka 18.
Sheria ya Kanuni ya Adhabu imeweka mazingira ya mtoto anayeweza kutumia umri kuwa kigezo cha utetezi dhidi ya makosa au mashitaka ya kijinai katika mtazamo wa aina 3 kama ifuatavyo;
- Mtoto chini ya miaka 10 hawezi kutenda kosa la kijinai
Kifungu cha 15 (1) cha Kanuni ya Adhabu Sura 16 kinaeleza msingi na maana ya utetezi huu
Mtu mwenye umri chini ya miaka kumi anachukuliwa kuwa hawezi kuwajibika kijinai kwa kutenda au kutotenda kosa.
Sheria ya Kanuni ya Adhabu inaanisha kwamba mtu yeyote ambaye ana umri chini ya miaka 10 anachukuliwa hawezi kuwajibika kwa makosa ya kijinai. Hii ina maana ngazi ya msingi ya utetezi kwa makosa yanayofanywa na watoto wadogo ni kuangalia umri wao. Huwezi kumpeleka mahakamani mtoto yeyote chini ya miaka 10 kushitakiwa kwa jambo lolote alilotenda au aliloacha kutenda.
Sheria ya makosa ya kijinai inachukulia umri huu kuwa mtoto hawezi kufahamu asili ya makosa au kujengeka fikra za kutenda kosa lolote la kijinai.
- Mtoto chini ya miaka 12 anaweza kuwajibishwa ikidhibitika ana ufahamu juu ya makosa aliyotenda
Mtu mwenye umri wa chini ya miaka kumi na mbili hatawajibika na kosa lolote la kijinai kwa kutenda au kutotenda jambo, isipokuwa kama itathibitishwa kwamba wakati wa kutenda au kuacha kutenda kitendo hicho alikuwa na uwezo wa kujua kwamba hapaswi kukitenda au kuacha kukitenda.
Sheria haimwajibishi kimashitaka mtoto mwenye umri chini ya miaka 12 endapo atatenda kosa au kutuhumiwa kwa kosa lolote. Hata hivyo dhana hii inakanushika endapo itadhibitika kuwa mtoto husika wakati anatenda kitendo cha kijinai alikuwa na ufahamu juu ya kile anachotenda kwamba ni kosa.
- Mtoto wa kiume chini ya miaka 12 hawezi kutuhumiwa kwa makosa ya kujamiiana.
Mwanaume mwenye umri wa chini ya miaka kumi na mbili atachukuliwa kuwa hawezi kufanya tendo la ndoa.
Mtoto wa jinsia ya kiume chini ya miaka 12 hawezi kuwajibishwa kijinai kutokana na makosa ya kujamiiana. Sheria inamchukulia mtoto wa umri chini ya miaka 12 hawezi kuwafanya tendo la ndoa na mtu yeyote kutokana na umri wake kuwa mdogo.
Kwa kutazama utetezi huu wa kisheria ambao upo kwa ajili ya watoto na kupima hali halisi ya jamii zetu tunaweza kuona kuna utofauti mkubwa wa kile sheria inachoeleza na uhalisia wa jamii yetu.
Kwa siku za karibuni watoto wadogo hata wa umri chini ya miaka 10 wamehusika kwa sehemu kubwa katika kutekeleza matukio ya uhalifu hata makubwa sana ikuhusisha na mauaji. Tumeshuhudia mmomonyoko wa maadili na watoto wetu kuwa na uwezo mkubwa wa kutenda makosa na hasa wakiweza hata kudanganya kwa sehemu kubwa juu ya uhalisia wa maisha yao.
Zipo sababu nyingi zinazosababisha kile sheria inachosema kuwa tofauti na uhalisia wa watoto wetu.
- Maendeleo ya sayansi na teknolojia; hii ni sababu kubwa sana ambayo watoto wadogo wameitumia kukuza fikra zao kuliko umri wao. Kwa sasa maendeleo katika kujifunza kupitia simu na television kwa watoto wanajifunza mambo mengi sana katika umri mdogo ikiwa ni mambo mazuri au mabaya.
- Nafasi ya malezi kuwa finyu; wazazi wa sasa tunatumia muda mwingi sana katika kutafuta masuala ya kiuchumi kuhusiana na familia zetu kiasi cha kuacha uangalizi na malezi ya watoto chini ya walezi wa nyumbani yaani ‘house girls’. Kwa kuangalia mfumo wa maisha ya hawa walezi wa nyumbani tunajikuta watoto wetu wanakusa msingi mzuri wa kukua kimaadili kwani wanaowalea pia ni watoto wenzao na wanawalea kwa kufuata mkumbo wa maisha ya mjini.
- Ongezeko la watoto wa wasio na makazi maalum; hawa jamii yetu imewapachika jina la ‘watoto wa mitaani’ ingawa hakuna mtaa unaozaa watoto bali wanazaliwa kutokana na baba na mama zao ambao kwa njia moja au nyingine wameacha kutimiza wajibu wa malezi. Tunakutana na watoto wadogo sana wakiwa barabarani wanaomba fedha. Katika mazingira haya ni wazi tabia za kijinai zinaweza kujijenga tangu wakiwa wadogo.
Hitimisho
Leo tumeangali utetezi kutokana na umri mdogo yaani chini ya miaka 12 ambapo mtoto anaonekana hawezi kutenda makosa ya kijinai. Hatahivyo mfumo wa kijamii kwa sasa unadhibitisha vinginevyo. Ni vyema sheria zikatazamwa upya na kuona namna bora ya kuweka mazingira ya watoto vizuri na hasa jukumu kubwa la kisheria linapaswa kuwa kwa wazazi endapo mtoto ataonekana katika umri mdogo anatenda matendo yanayoashiria jinai basi mzazi au mlezi awajibike katika vyombo vya kisheria. Hii itasaidia sana kutukumbusha wajibu wa kuwalea watoto kwenye maadili mema na kujiwekea akiba ya jamii ya baadae ya kulijenga taifa.
Ni rai yangu pia kwa wazazi na walezi hata na watu wengine katika umri wa utu uzima kuwalinda watoto kutokana na mitandao , vipindi vya televisheni na pia kujiepusha na kuwatendea makosa mbalimbali kama kuwadhulumu utu wao, kuwaingilia na kufanya vitendo viovu dhidi yao kwani tunawajengea taswira mbaya sana katika mustakabali wa maisha yao ya baadae.
Mtoto aliyefanyiwa mambo ya ukatili katika maisha yake ya utoto ikiwa ni kupigwa, kunyanyaswa kwa sababu ya jinsia yake, kubakwa, kulawitiwa ni wazi mtazamo wake akiwa mkubwa utakuwa hivyo hivyo juu ya watoto wengine na atashiriki kutenda hayo hayo.
‘Tuwalinde watoto wetu kwa malezi bora kwa kutokomeza vyanzo vyote vya tabia za kijinai kwenye malezi yao’
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.
Muhimu
Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .
‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’
Nakutakia siku njema.
Wako
Isaack Zake, Wakili