Utetezi wa kisheria kutokana Ugonjwa wa Akili

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa makala zetu ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Katika makala iliyopita tumezongumzia Utetezi wa kisheria kutokana na Umri Mdogo. Leo tunakwenda  kuangalia Utetezi wa Kisheria unaotokana na Ugonjwa wa Akili.

Dhana ya Utimamu wa Akili kwa watu wote

Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 imebainisha kuwa ipo dhana inayokanushika kwamba wato wote wana akili timamu kwa wakati wote. Dhana hii inabainishwa katika kifungu cha 12 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ikisema

Kila mtu atachukuliwa kuwa na akili timamu, na atachukuliwa kuwa na akili timamu wakati wote mpaka pale itakapothibitishwa vinginevyo.

Dhana hii ya kisheria ni muhimu sana katika kusaidia watu wengi kujitetea kuwa wakati anatenda kosa hakuwa vizuri kimawazo au alikuwa amechanganyikiwa. Hivyo endapo kosa litafanyika mahali na mtuhumiwa kukamatwa atachukuliwa kuwa alikuwa na akili timamu wakati ule wa kutenda kosa alilotenda.

Utetezi wa Kisheria kwa Ugonjwa wa Akili

Sheria inatambua mazingira ambayo mtu anaweza kutenda jambo fulani ambalo kisheria ni kosa lakini mazingira ya utendaji wa kosa hilo alikuwa ameathiriwa na ugonjwa ambao unaathiri akili yake katika kufikiri. Hapa ni lazima ithibitike mbele ya mahakama kuwa mtuhumiwa alikuwa na tatizo la kiakili wakati anatenda kosa husika.

Kifungu cha 13 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania kinaeleza

13.-(1) Mtu hatawajibika kwa kutenda kosa la kijinai kwa kitendo au kuacha kutenda iwapo wakati wa kutenda kitendo hicho au kuacha kutenda alikuwa katika hali ya ugonjwa wowote unaoathiri akili yake ambapo:-

 

  • hawezi kujua kitu anachokitenda;

 

  • hawezi kutambua kwamba hapaswi kutenda au kufanya jambo husika; au

 

 

  • hana uwezo wa kuzuia kitendo au kuacha kutenda.

Ufafanuzi

Ugonjwa wa akili kwa mtuhumiwa unaweza kutumiwa kama utetezi wa kisheria dhidi ya mashitaka ya kijinai kama ilivyobainishwa katika kifungu cha 13 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu. Ili mtuhumiwa aweze kutumia utetezi huo na kufanikiwa dhidi ya mashitaka husika ni lazima ugonjwa huo uweze kudhibitisha mojawapo  wa vigezo vilivyowekwa kisheria;

  1. Kwamba wakati wa kutenda kosa husika mtuhumiwa hakuwa na uwezo katika akili yake kujua kitu anachotenda.

Ni lazima idhibitike mbele ya mahakama kuwa mtuhumiwa alikuwa ana ugonjwa ambao umeathiri akili yake kiasi cha kushindwa kujua kitendo gani alitenda. Tunaona mifano mingi barabarani ambapo wapo wagonjwa wa akili na wanaweza kutenda vitendo vingi vya uhalifu ikiwepo kupiga watu au kuharibu mali n.k. mtu wa aina hii endapo atakamatwa na kufikishwa mahakamani kwa makosa yale ikadhibitika katika maneno yake na hasa vipimo vya madaktari juu ya uwezo wa akili yake kuwa hakuwa anajua kile anachofanya basi anaweza kuachiliwa kutokana na utetezi wa ugonjwa wa akili.

  1. Kwamba wakati wa kutenda kosa husika mtuhumiwa hakuwa na uwezo wa kutambua kuwa kile anachotenda ni kosa.

Ugonjwa wa akili pia unaweza kumwathiri mtuhumiwa kwa kiwango cha kupoteza au kutokuwa na uwezo wa kujua kile anachotenda ni kosa kisheria. Mara kadhaa tumesikia juu ya watu wenye ugonjwa wa akili akibaka mtu hadharani, au kufanya kitendo ambacho kwa kawaida si rahisi mtu aliye timamu anaweza kufanya. Hii ni kwa sababu ugonjwa huo unakuwa umeathiri uwezo wake wa kutambua kile anachofanya ni kosa kisheria.

  1. Kwamba wakati wa kutenda kosa husika mtuhumiwa alikosa uwezo katika akili yake kujizuia kutenda kitendo husika.

Ugonjwa wa akili unaweza kuwa sababu ya utetezi wa kisheria ambapo umeathiri uwezo wa mtuhumiwa kushindwa kujizuia kutenda jambo fulani ambalo ni kosa kisheria. Sheria inaweza kuwa imekataza mathalani watu kutembea bila nguo, lakini kutokana na ugonjwa wa akili mtu anaweza kujikuta anatembea pasipo kuvaa nguo, hivyo mtuhumiwa husika anakuwa ameshindwa kujizuia kufanya kitendo ambacho kimekatazwa na sheria.

Hitimisho

Leo tumeangalia juu ya utetezi wa kisheria kutokana na ugonjwa wa akili ambapo mtuhumiwa anaweza kuutumia endapo itadhibitika kuwa wakati anatenda kosa alikuwa katika hali ya ugonjwa huo. Ifahamike kuwa, kabla ya mahakama kuukubali utetezi huu wa ugonjwa wa akili ni lazima mtuhumiwa akapimwe na wataalam wa magonjwa ya akili nao wapate nafasi ya kutoa maoni yao kuhusiana na uwezo wa mtuhumiwa wakati wa kutenda kosa. Pia ni muhimu kufahamu kuwa wapo watu wana athiriwa na ugonjwa wa akili katika vipindi fulani na wapo wengine ni wagonjwa wa moja kwa moja.

Ndio maana ni muhimu kwetu kama wananchi kufuata utaratibu wa kisheria wakati tunasughulikia masuala ya uhalifu kwani tunaweza kuadhibu mtu kutokana na makosa aliyofanya pasipo kujua kuwa wakati mtu huyo anatenda makosa hayo alikuwa katika hali gani ya kiafya kwenye akili yake. Ni mchakato wa kimahakama pekee unaoweza kutusaidia kufahamu hasa kiini cha tatizo lililosababishwa na mtuhumiwa endapo lilisabashwa akiwa na akili timamu au la.

‘Anzisha na fuata mchakato wa kisheria katika kushughulikia masuala ya uhalifu katika jamii’

Kumbuka kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili

2 replies

Comments are closed.