29.A. Usitishaji wa Ajira kwa Sababu ya Mahitaji ya Uendeshaji

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala za hivi karibuni tumekuwa tukichambua sababu na taratibu mbalimbali zinazoweza kusababisha au kufuatwa ili kusitisha ajira ya mfanyakazi kihalali. Leo tunaendelea aina nyingine wa Usitishaji wa Ajira kwa sababu ya Mahitaji ya Uendeshaji.

Maana ya Mahitaji ya Uendeshaji

Ajira inaweza kusitishwa pia na mwajiri kutokana na sababu ya Mahitaji ya Uendeshaji.

Usitishaji wa ajira kwa Mahitaji ya Uendeshaji kwa lugha ya kiingereza unaitwa ‘Operational Requirements or Retrenchment’. Tumezoea kwa lugha maarufu mahali pa kazi ni ‘Kupunguzwa Kazi’.

Katika siku za karibuni kumekuwa na wimbi kubwa sana la waajiri kupunguza wafanyakazi kwa sababu mbalimbali. Changamoto kubwa ya waajiri ni kutokujua namna ambayo ipo kisheria ya kusaidia zoezi zima la upunguzaji wa wafanyakazi kufanyika kwa mujibu wa sheria. Sehemu kubwa ya waajiri hawafahamu sababu au taratibu zinazopaswa kutumiwa wakati wa kusitisha ajira kwa ‘kupunguza wafanyakazi’.

Hali kadhalika pia wafanyakazi wanaachishwa kazi kwa ‘kupunguzwa kazi’ hawafahamu haki zao za kisheria na namna bora ya kunufaika kimaslahi katika zoezi la kupunguzwa kazi. Wengi wanaishia kulalamika au kukata tamaa pasipo kuchukua hatua stahiki ili kupata haki zao za msingi.

Katika mfululizo wa makala hizi tutaeleza kwa kina juu ya sababu na taratibu ambazo zinapaswa kuzingatiwa na pande zote wakati wa zoezi la kusitisha ajira kwa mahitaji ya uendeshaji.

Sababu za kisheria zinazoruhusu Kupunguza Wafanyakazi

Sheria ya Ajira imeweka mazingira ya kisheria ambayo pekee ndiyo yanaweza kuruhusu mwajiri kuchukua hatua ya kuanza mchakato wa kusitisha ajira kwa mahitaji ya uendeshaji au kupunguza wafanyakazi. Hivyo si kila sababu inaweza kutumiwa na mwajiri kupunguza kazi wafanyakazi bali zile zilizoanishwa na sheria pekee.

Mazingira ambayo yanaweza kumpa mwajiri uhalali wa kupunguza wafanyakazi ni endapo;

  1. Mahitaji ya kiuchumi yanayohusiana na usimamizi wa fedha. Hapa ni endapo inaonekana kuna mzigo mkubwa wa kulipa wafanyakazi kuliko kile shirika inachoingiza.

 

  1. Mahitaji ya teknolojia kwa maana ya kupatikana teknolojia mpya inayosababisha baadhi ya wafanyakazi kutokuwa na kazi ya kufanya. Teknolojia inaweza kusababisha wafanyakazi kupunguzwa mahali pa kazi. Siku hizi kazi nyingi zilizokuwa zinafanywa na watu zimeundwa mashine kurahisisha kazi.

 

 

  1. Mahitaji ya kubadili mpangilio wa shughuli za shirika kutokana na kuunganisha biashara, mabadiliko ya kibiashara, kuhamisha biashara au sehemu ya biashara au njia mbadala ya kufanya biashara kwa tija zaidi n.k

Uwepo wa sababu mojawapo kati ya hizi tatu ambazo zimejadiliwa zinaweza kutoa uhalali kwa mwajiri kuanza mchakato wa kupunguza wafanyakazi.

 

Hitimisho

Ni muhimu kwa wafanyakazi na waajiri kuzingatia sababu ya kupunguza kazi wafanyakazi. Waajiri wengi wanashindwa kuanisha sababu ya kupunguza kazi wafanyakazi na wanatumia sababu za kinidhamu au ugonjwa kuwa sababu ya kupunguza mfanyakazi kitu ambacho ni kinyume cha sheria ya kazi. Kabla ya kuchukua hatua ni lazima ujiridhishe kama unayo sababu ya msingi ya kumpunguza mfanyakazi ndipo ufuate taratibu, kinyume cha hapo unapalilia matatizo ya mbele.

Usiache kufuatilia makala nyingine inayoendelea kufafanua zaidi mchakato mzima wa kupunguza wafanyakazi mahali pa kazi kama sababu ya kusitisha ajira.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili.