29.B. Usitishaji wa Ajira kwa Sababu ya Mahitaji ya Uendeshaji

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala za hivi karibuni tumekuwa tukichambua sababu na taratibu mbalimbali zinazoweza kusababisha au kufuatwa ili kusitisha ajira ya mfanyakazi kihalali. Katika makala iliyopita tuliona utangulizi juu ya usitishaji wa ajira kwa sababu ya mahitaji ya uendeshaji.Leo tunaendelea na sehemu ya pili ya mfululizo huo.

Utaratibu wa Usitishaji kwa Mahitaji ya Uendeshaji

Katika makala iliyopita tulizungumzia kwa kina juu ya sababu za usitishaji wa ajira kwa sababu ya mahitaji ya uendeshaji. Leo tunaendelea katika kuona namna ya utaratibu wa sheria kwa usitishaji wa ajira kwa mahitaji ya uendeshaji.

  1. Notisi kwa wafanyakazi

Jambo muhimu kwa mwajiri mara tu anapoona anayo sababu ya kupunguza wafanyakazi iwe kutokana na masuala ya fedha, teknolojia au mfumo wa uendeshaji wa kampuni ni muhimu kuwasiliana na wafanyakazi husika kwa njia ya notisi.

  1. Kutoa taarifa zote zinazohusiana na upunguzaji wa wafanyakazi

Mwajiri anapaswa kutoa taarifa za kutosha kwa wafanyakazi kuhusiana na zoezi zima la kupunguza wafanyakazi. Iwapo wafanyakazi ni wanachama cha wafanyakazi basi taarifa hizo za kupunguza wafanyakazi. Taarifa hizo ni lazima zieleze yafuatayo;

  • Sababu za kupunguza wafanyakazi
  • Hatua mbadala za kuzuia au kupunguza idadi ya wafanyakazi watakaopunguzwa
  • Idadi ya wafanyakazi wanakusudiwa kupunguzwa kazi
  • Mapendekezo na vigezo vitakavyotumika
  • Muda wa zoezi
  • Mapendekezo ya kiinua mgongo
  • Msaada atakaotoa mwajiri kwa watakaopunguzwa kazi

 

  1. Majadiliano na wafanyakazi

Mwajiri anapaswa kuingia kwenye majadiliano na wafanyakazi au chama kinachowakilisha wafanyakazi kabla ya kusitisha ajira kwa sababu ya mahitaji ya uendeshaji. Kwa njia ya majadiliano pande zote zinaweza kufikia mwafaka juu ya mambo ya msingi yafuatayo;

  • Sababu za kupunguza wafanyakazi
  • Hatua mbadala za kuzuia makali ya kupunguza wafanyakazi kama vile kuwahamishia kwenye kazi nyingine, kustaafu mapema. Kupunguzwa kwa hiari au likizo bila malipo n.k
  • Vigezo vya kuchagua watakaopunguzwa kama vile (LIFO-Last In First Out), uzoefu, stadi maalum, sifa na upendeleo maalum.
  • Muda wa zoezi la kupunguza wafanyakazi
  • Kiinua mgongo
  • Hatua za kupunguza makali ya kukosa kazi kama vile kupewa muda wa kutafuta kazi nyingine.

 

  1. Fursa ya mlisho nyuma (Feedback)

Katika mchakato wa kusitisha ajira kwa njia ya kupunguza wafanyakazi, ni lazima kuwe na nafasi ya kutoa mlisho nyuma kwa wafanyakazi kutoka kwa chama au wawakilishi wao kwenye majadiliano. Mambo ya msingi yanapaswa kuzingatiwa na chama au wawakilishi wa wafanyakazi

  • Kukutana na kuwaarifu wafanyakazi kile kinachoendelea kwenye mashauriano
  • Kukutana na mwajiri au
  • Kuomba, kupokea na kuchambua taarifa muhimu kukiwezesha chama au wawakilishi kuelewa kwa ufasaha taarifa hizo na kushauriana na mwajiri kwa madhumuni ya kufikia makubaliano kuhusu hatua mbalimbali za kushughulikia zoezi hilo.

 

  1. Usuluhishi

Endapo hakuna makubaliano yoyote, suala la usitishaji wa ajira kwa kupunguza wafanyakazi litawasilishwa mbele ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi kwa lengo la kusuluhishwa. Katika kipindi cha siku 30 wakati wa usuluhishi mwajiri hatoruhusiwa kupunguza wafanyakazi. Endapo siku 30 zitaisha na hakuna mwafaka basi mwajiri anaweza kuendelea na zoezi la kupunguza kazi wafanyakazi.

 

  1. Upendeleo wa kuajiriwa upya

Mara nyingi zoezi hili huwa linatoa upendelea kwa wafanyakazi waliopunguzwa kazi kuajiriwa upya endapo nafasi zitajitokeza. Suala hili la kuajiriwa upya inategemea vigezo na masharti yanayoambatana na ajira mpya.

 

Hitimisho

Ndugu msomaji na mfuatiliaji wa uchambuzi wa sheria ya kazi kama tulivyoona katika makala hizi mbili juu ya usitishaji wa ajira kwa kupunguza wafanyakazi kuwa ni lazima ziwepo sababu maalum na utaratibu husika ufuatwe kikamilifu. Wafanyakazi wengi wanapoteza haki zao kwa kutokujua sheria na mwongozo juu ya usitishaji wa ajira kwa kupunguzwa kazi. Ipo mifano mingi sana ya mwajiri kumpunguza mfanyakazi mmoja katika ajira hii ni kinyume na utaratibu wa sheria za kazi.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili.