Sheria Leo. Kujichukulia Sheria Mkononi kwenye Migogoro ya Kifamilia

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Leo kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku.tumekuwa na mfululizo wa makala zinazohusu tabia ya watu kujichukulia sheria mkononi. Katika makala iliyopita tumechambua juu ya eneo la migogoro ya ardhi na tabia za watu kuchukua sheria mkononi. Leo tunaangalia tabia za watu kujichukulia sheria mkononi kwenye Migogoro ya Kifamilia. Karibu tujifunze.

Migogoro ya Kifamilia

Mfumo wa familia katika jamii zetu za kiafrika unafahamika kwa uwepo wa wanafamilia wengi ukihusisha ndugu na jamaa wa karibu. Asili ya familia za kiafrika ni zile zinazohusisha baba, mama, watoto, shangazi, wajomba, babu, bibi n.k. zipo familia ambazo zinajengwa na ndoa za mke zaidi ya mmoja. Hivyo kuzifanya familia kuwa na idadi kubwa ya watu na watoto pia.

Katika jamii yoyote au kundi la watu hapakosi kupishana kauli na mitazamo mbalimbali. Pia katika familia yapo mazingira ambayo yanasababisha mgongano na hatimaye kuzaa migogoro ndani ya familia.

Migogoro inayoibuka mara kwa mara inaweza kuwa baina ya mume na mke au mume na wake zake, wake za mume mmoja, au wazazi na watoto. Pia yapo mazingira yanayojitokeza mgogoro kuibuka katika mahusiano ya kifamilia baina ya mtu na mjomba au shangazi au babu na bibi.

Katika mfumo wa malezi ya kiafrika ni sahihi kwa mzazi kumlea mtoto au mtu aliye chini ya himaya yake na ikibidi kuchukua hatua za kinidhamu dhidi yake ambazo zinaweza kuhusisha adhabu ya fimbo au nyingine itakayofaa.

Kadhalika mfumo wetu wa kitamaduni unaonesha dhahiri kuwa mwanamume anayo nafasi kubwa pia ya kumdhibiti mwanamke akiwa mkewe au mtu mwenye mahusiano naye ikitokea tofauti katika mahusiano yao.

Wengi tumekuwa mashuhuda ya wanawake wakipigwa na waume zao kwa sababu mbalimbali kiasi kwamba wengine wanaona ni utamaduni na ni haki ya wanaume kufanya hivyo. Hali hii ya ukatili katika familia sasa imeenda hata kwa watoto pia. Tumepata taarifa mbalimbali juu ya ukatili wanaofanyiwa watoto adhabu wanazopewa na wazazi au walezi wao kutokana na makosa wanayotuhumiwa kuzidi hata kipimo cha adhabu. Wapo watoto waliofungiwa ndani kwa muda mrefu, wapo waliochomwa moto na wazazi na wapo wale ambao kwa adhabu waliyopewa hawakuweza kustahimili na kupoteza maisha.

Hali ya ukatili iliyozidi katika jamii yetu ni matumizi mabaya ya madaraka ya wazazi au walezi katika familia. Maamuzi haya ya kujichukulia sheria mkononi inaathiri hata katika familia. Kutokana na maamuzi haya ya kujichukulia sheria mkononi madhara makubwa yamejitokeza;

  • Kusababisha ulemavu au mauaji kwa wanafamilia wasio na hatia kutokana na adhabu kubwa wanazopewa au mateso ndani ya familia.

 

  • Kuamsha hali ya chuki kubwa ndani ya familia na jamii yote kutokana na matendo ya ukatili ndani ya familia

 

  • Kuvunjika kwa ndoa na misingi bora ya malezi ya watoto na kuibua tatizo la makuzi ya watoto kitu ambacho kinaathiri jamii ya baadae.

 

 

Hatua za kuchukua kuepusha watu kuchukua sheria mkononi katika migogoro ya kifamilia

  • Kujenga maadili mema ya malezi ya watoto kwenye familia kwa kuhakikisha wanapata maelekezo na endapo kuna sababu ya adhabu basi iwe ya kiasi kusaidia mtoto kuelewa makosa yake na kujirekebisha

 

  • Wazazi kuwa mfano wa kutafuta suluhu katika tofauti zozote zinazojitokeza baina yao. Kama wazazi watakuwa watu wa ugomvi na kupigana kila siku basi watoto wataiga mfumo wa vurugu katika jamii.

 

  • Serikali kuongeza nguvu katika sheria zinazohusiana na masuala ya familia na utekelezaji wake katika ngazi zote za kijamii.

 

Migogoro ya kifamilia imesababisha matatizo makubwa sana katika jamii zetu katika siku za karibuni. Tumeona hata wazazi wengine wakiingia tamaa ya kimwili dhidi ya watoto wao. Tunapaswa kama jamii kuwa na muda na familia zetu kusaidia kuwalea watoto katika misingi ya kiimani zaidi na kujitahidi kukabiliana na nguvu ya mitandao ambayo ina kasi kubwa ya kuharibu maadili yetu. Wakati huu kila mtu amekuwa akikimbizana na masuala ya kifedha lakini tunasahau wajibu mkubwa wa kuilea familia kwenye mfumo bora wa maadili. Tunajikuta watoto au familia inapata kila kitu ambacho fedha inanunua lakini wanakosa tabia ya utu wa mtu ambayo ndio msingi wa maisha ya kijamii. Makosa tunayoyafanya kama walezi tunajikuja tuna jamii iliyolowea kwenye madawa ya kulevya, ugomvi, tabia za uharibifu kwa watoto wa kiume kuishi kama wanawake na nyingine nyingi kwa kukosa muda wa kufuatilia mienendo ya nyumba zetu. Kazi hii inahitaji ushirikiano mkubwa wa wanafamilia wote.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

 

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili