Sheria Leo.Kujichukulia Sheria Mkononi kwenye Uhalifu wa Kujamiiana

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Leo kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku.tumekuwa na mfululizo wa makala zinazohusu tabia ya watu kujichukulia sheria mkononi. Katika makala iliyopita tumechambua juu ya eneo la migogoro ya ardhi na tabia za watu kuchukua sheria mkononi. Leo tunaangalia tabia za watu kujichukulia sheria mkononi kwenye Uhalifu wa Kujamiiana. Karibu tujifunze.

Makosa yatokanayo na Uhalifu wa Kujamiiana

Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria inaeleza kwa kina tafsiri sahihi juu ya aina mbalimbali za uhalifu unaohusiana na kujamiiana.

Matukio ya makosa ya kujamiiana yamezidi kushamiri sana katika jamii yetu. Kila kukicha tunasikia juu ya makosa ya ubakaji, ubakaji kwa watoto, ulawiti na mengine mengi ya namna hiyo yamezidi sana.

Watoto wadogo wamekuwa wahanga wakubwa sana katika matukio ya aina hii ya uhalifu katika jamii. Changamoto imekuwa kubwa kutafuta namna ya kukomesha vitendo hivi ndani ya jamii. Zimebuniwa njia nyingi ikiwepo kuongeza meno kwa sheria za nchi ili kutoa adhabu kali zaidi kwa watuhumiwa wa makosa haya ikewepo kifungo kisichopungua miaka 30 jela au kifungo cha maisha lakini bado uhalifu huu umeongezeka siku kwa siku.

Kwa msingi huo jamii imeamua kutumia njia nyingine za kusuluhisha tatizo hili kwa kuchukua sheria mkononi ikiwepo kutoa adhabu ya kijamii kwa watuhumiwa husika endapo watakamatwa kutokana na tuhuma hizi za kujamiiana. Tumesikia na kushuhudia baadhi ya adhabu wanazopata watuhumiwa kutoka kwa jamii zikiwa za kutisha zaidi ikiwepo kuuwawa, au kutolewa viungo vyao vya uzazi na ikibidi watu wengine kuwaingilia kinyume na maumbile katika kutoa adhabu dhidi ya makosa haya.

Mtindo huu wa jamii kujichukulia sheria mkononi kwa kuwaadhibu watuhumiwa wa makosa hayo pasipo kufuata mkondo wa sheria ni njia hatari sana kwa jamii kwani badala ya kutatua tatizo kwa namna nyingine tunalipalilia zaidi kwa vizazi vya sasa na baadae.

Kwa kiasi kikubwa yapo madhara ya uamuzi wa kuchukua sheria mkononi katika makosa ya uhalifu ya kujamiiana

Hapa nitaeleza baadhi ya madhara hayo;

  • Kusababisha madhara zaidi kwa jamii kwa kuchukua hatua zisizo za kisheria kwa kupanda mbegu ya kisasi kwa jamii.

 

  • Nafasi ya kuwatuhumu na kuwaadhibu watu wasiohusika. Kumekuwa na matukio mengi kwenye jamii ya sasa ya kutuhumu watu pasipo kuwa na ushahidi juu ya utendaji wa makosa ya aina hii. Ikiwa jamii itachukua hatua pasipo kufanyika uchunguzi, wapo watu wengi wasio na hatia watajikuta wamehukumiwa pasipo kusikilizwa.

 

 

Hatua za kuchukua kuepusha watu kuchukua sheria mkononi katika makosa ya kujamiiana

  • Kuimarisha maadili kwa jamii na wazazi kuwa na muda zaidi na watoto wao ili kujua mienendo yao ya kila siku

 

  • Kwa kuwa matukio ya makosa ya kujamiiana yanafanyika kwa siri ni muhimu sana vyombo vya uchunguzi vikapewa nafasi ya kuchunguza ili yeyote asionewe kwa tuhuma zisizo na ukweli wowote.

 

  • Sheria kurekebishwa na kuongezewa meno kwa adhabu kali wa watu wote wenye kupatikana na hatia.

 

Makosa ya kujamiiana yanaonekana kuongezeka kila kukicha kwenye jamii kiasi ambacho tunaonekana kuelemewa na uhalifu huu. Jamii inapaswa kufanya mjadala mpana sana wa kutafuta suluhu kuliko kuchukua sheria mkononi kwani madhara yake ni makubwa zaidi. Makosa haya wakati mwengine au mara nyingi yanawahusu watu ambao ni ndugu zetu wa karibu sana ambao tunaishi nao katika majumba yetu. Kama familia lazima tuwe na taadhari na kuichunguza mienendo ya wale ambao tunaishi nao katika nyumba zetu kwani tabia zinaweza zisiwe zinafanana.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

 

 

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili