Sheria Leo. Kujichukulia Sheria Mkononi kwenye Uhalifu wa Mali
Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Leo kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku.tumekuwa na mfululizo wa makala zinazohusu tabia ya watu kujichukulia sheria mkononi. Katika makala iliyopita tumechambua juu ya eneo la migogoro ya ardhi na tabia za watu kuchukua sheria mkononi. Leo tunaangalia tabia za watu kujichukulia sheria mkononi kwenye Uhalifu wa Mali. Karibu tujifunze.
Makosa yatokanayo na Uhalifu wa Mali
Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria inaeleza kwa kina tafsiri sahihi juu ya aina mbalimbali za uhalifu unaohusiana na mali. Katika kuzungumzia kwenye makala hii tunalenga hasa uhalifu wa wizi au uporaji au ujambazi unaofanyika kwa watu ikiwa ni majumbani, ofisini au njiani.
Aina hii ya uhalifu imezoeleka sana ndani ya jamii na matukio yanaripotiwa kila mara. Watu wanavamiwa aidha kwa kutumia silaha au kundi la watu na kupora mali ya mtu na hata wakati mwengine kumjeruhi mhanga na kumsababishia kifo ikibidi.
Uhalifu wa aina hii unazidi kukua kwa kasi nyingi na matukio haya yamesambaa maeneo mengi. Wahalifu wameendelea kubuni kila njia inayoweza kuwasaidia kutekeleza uhalifu husika na kutokomea. Katika siku za karibuni wahalifu wamekuwa wakitumia vyombo vya usafiri mathalani boda boda kufanya uhalifu huo kwa urahisi zaidi.
Hali hii ya uhalifu na madhila yanayowapata wananchi imewafanya nao kuchukua kila aina ya taadhari na namna bora ya kukabiliana na wahalifu hawa. Kwa sasa maeneo mengi wanapomkamata mwizi au jambazi basi hawana mjadala wowote juu yake isipokuwa kuua kwa kupiga au/na kuchoma moto kabisa. Hivi karibuni nimeshuhudia tukio la mtuhumiwa wa wizi kwa kutumia boda boda akiwa amechomwa moto karibu kabisa na maeneo ninayoishi.
Mtazamo wa jamii kuhusiana na adhabu hii wanayopewa watuhumiwa ni kuwa kwa kuwaua na kuchoma moto basi itasababisha hofu kwa wengine wasijitokeze katika eneo husika. Sijafanya tafiti za kutosha kuweza kudhibitisha dhana hii ikiwa ni ya ukweli ama la, lakini hizi ni fikra ambazo zipo ndani ya jamii na inawezekana hata wewe ndugu yangu unayesoma ukawa na mtazamo huu.
Hata hivyo yapo madhara ya uamuzi wa kuchukua sheria mkononi katika makosa ya uhalifu wa mali
Hapa nitaeleza baadhi ya madhara hayo;
- Kusababisha mauaji ya mtu au watu waliohusika wanaotuhumiwa na uhalifu wa mali. Katika kuua tunapoteza fursa ya kujua chanzo cha uhalifu na kuweza kupata mtandao mzima ambao unahusika na uhalifu huo.
- Nafasi ya kufanya makosa kwa kuadhibu asiye mhalifu. Zipo shuhuda nyingi zinazoweza kudhibitisha kuwa wapo wanaoweza kuitiwa kelele za mwizi wakati si wezi bali ni raia wema kabisa ila kwa visa vya watu wengine basi wanajikuta katika matatizo hayo na hata kupoteza maisha.
Hatua za kuchukua kuepusha watu kuchukua sheria mkononi katika makosa ya uhalifu wa mali
- Kuimarisha mfumo wa ulinzi katika jamii ili kupunguza matukio ya uhalifu katika maeneo yetu.
- Vyombo vya uchunguzi kuhakikisha wanafanya uchunguzi ndani ya muda mfupi na hatua stahiki zichukuliwe
- Mahakama kuwa na mfumo mzuri wa kushughulikia makosa ya jinai kwa haraka. Ikiwezekana mahakama ziwepo za kijinai zenye kusikiliza na kutoa maamuzi ya haraka na adhabu inayostahili.
- Wananchi kukubali mchakato wa kisheria na kushiriki katika kuukamilisha ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa sahihi na kutoa ushahidi.
Tabia hii ya kuua watuhumiwa wa matukio ya wizi wa mali imeshamiri sana na waathiriwa wakubwa ni hawa wanaotuhumiwa kuiba vitu vidogo vidogo lakini ni jamii hii haikemei wala kuchukua hatua kwa wezi wanaliibia taifa katika miradi mikubwa mikubwa sana sana tunawapa sifa za kufanikisha wizi wao katika nafasi walizopewa. Ni muhimu tuwe watu wa haki na kuchukua hatua stahiki kila mara inapotubidi. Tusimamie jamii zetu vizuri tulaani hata na kuzitaka mamlaka kuchukua hatua zaidi si kwa uhalifu huu mdogo mdogo bali hata hatua kali kwa uhalifu mkubwa ili kujenga jamii inayochukia uhalifu kwa ujumla na si baadhi ya wahalifu tu na wengine tukishirikiana nao kwa kuwasifia kwa uhalifu wao dhidi ya umma.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.
Muhimu
Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .
‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’
Nakutakia siku njema.
Wako
Isaack Zake, Wakili